Sh20 bilioni kuwalipa walioghushi vyeti feki Tanzania
- Ni wale waliofurushwa kazini mwaka 2017 kutokana na kughushi vyeti mbalimbali vikiwemo vya taaluma kupata ajira
- Mkurugenzi wa PSSSF asema watapewa kipaumbele kupata stahiki zao ndani ya siku 60.
- Watakiwa kufuata taratibu ikiwemo kwenda kwa mwajiri wa mwisho kabla ya kwenda PSSF.
Dar es Salaam. Watu 9,000 waliokuwa wamefutwa kazi na Serikali kutokana na kughushi nyaraka za ajira watapatiwa mafao yao ya Sh20 bilioni, hatua ambayo itawapunguzia maumivu ya kupoteza sehemu ya stahiki zao za hifadhi ya jamii.
Watu hao ni sehemu 9,932 ya waliofurushwa kazi na Serikali ya hayati Rais John Magufuli mwaka 2017 ikiwa ni moja ya hatua ya kuongeza utawala bora ndani ya taasisi za umma.
Wanufaika hao walioondolewa katika utumishi wa umma katika zoezi la uhakiki wa vyeti lililoendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2016 hadi Aprili mwaka 2017.
Hata hivyo, wakati wanafutwa kazi hakupewa fursa ya kupata mafao yao kama wafanyakazi wengine ambao hujiudhulu au kufutwa kazi kwa masuala mengine yakiwemo ya utovu wa nidhamu licha ya kuwa walikuwa wanakatwa mishahara wakati wa utumishi wao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) , Hosea Kashimba amewaambia wanahabari leo Novemba 9, 2022 kuwa hadi sasa watumishi 9,000 wamejitokeza kupata mafao yao baada ya Serikali kuagiza wapewe michango waliyochangia enzi za utumishi wao.
Wiki mbili zilizopita Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia watumishi hao kurejeshewa michango yao waliyochangia kwenye mfuko huo.
Katika mkutano huo na wanahabari jijini Dodoma, Kashimba amesema mfuko huo unatarajia kuwalipa Sh20 bilioni za mafao yao watumishi hao 9,000.
“Tumejipanga ndani ya mfuko kwamba hawa watu tuwape kipaumbele tumejipa muda mfupi sana ndani ya siku 60 watakuwa wamelipwa wote,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema ndani ya siku tisa za utekelezaji wa agizo hilo tayari wameanza kupokea madai za wanuafika hao.
Pia amewasisitiza wanufaika hao kuwasilisha madai yao kwa haraka ili waweze kuhudumiwa kwa haraka.
“Hii hatua ila kamchakato kidogo lazima mfanyakazi aende kwa muajairi wake apewe fomu kisha alete kwetu tulipe,” ameongeza mkurugenzi huyo.
Soma zaidi
-
Serikali yataja mikakati kunusuru mfuko wa NHIF
-
Ndalichako aziwashia moto halmashauri mafao ya wastaafu
Njia ya za kufuata kupata mafao
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amewataka wanufaika wa mfuko huo hatua za kuchukua kupata staahiki ya mafao yao.
“Niwakumbushe wafanyakazi wa kwenye jambo hili nenda kwa mwajiri wako wa mwisho ulikoajiriwa kabla ya kuja PSSSF,” ameongeza Msigwa.
Sambamba na hilo ameyataka makundi yote yaliondolewa kazini kwa kukosa sifa au kwa kughushi vyeti kupeleka madai yao kwenye mfuko huo ili waweze kuliiupwa stahiki zao.
“Kuna wale waliokuwa na vyeti feki na waliofanya udanganyifu kwenye fomu za kupima watumishi wote nendeni,” amesema Msigwa.