Faida za kufanya mazoezi kwa wajawazito
- Hupunguza uwezekano wa kupata kifafa cha mimba, kisukari cha ujauzito, shinikizo la damu la ujauzito.
- Huzuia tatizo la sonona baada ya kujifungua, kupunguza uwezekano wa kupata matatizo wakati wa kujifungua.
Dar es Salaam. Kipindi cha ujauzito kwa mwanamke huambatana na mabadiliko mbalimbali ya kiafya ikiwemo kuchoka mara kwa mara.
Hata hivyo, mama mjamzito anatakiwa kufanya mazoezi ili kuweka mwili sawa na mtoto aliyepo tumboni.
Faida za kujishughulisha na mazoezi wakati na baada ya ujauzito hupunguza uwezekano wa kupata kifafa cha mimba, kisukari cha ujauzito, shinikizo la damu la ujauzito na kuongezeka uzito wakati wa ujauzito.
Pia kuzuia tatizo la sonona baada ya kujifungua, kupunguza uwezekano wa kupata matatizo wakati wa kujifungua kama vile kuchelewa kujifungua na uwezekano wa kuzaa watoto njiti, watoto wenye uzito mdogo au mkubwa kupindukia au mtoto kufia tumboni.
Mwongozo huu wa kuushughulisha mwili na kuepuka tabiabwete wa mwaka 2021 uliotolewa na Wizara ya Afya unaeleza kuwa mama mjamzito anatakiwa kuendelea kujishughulisha au kufanya mazoezi wakati wote wa ujauzito endapo daktari hajashauri kinyume
“Inashauriwa kujishughulisha au kufanya mazoezi ya kiwango cha kati hadi cha juu kwa muda usiopungua dakika 150 wiki nzima (masaa mawili na nusu kwa wiki),” umeeleza mwongozo huo.

Wajawazito waliokuwa wakifanya mazoezi au kushughulisha mwili kabla ya ujauzito wanashauriwa kuendelea na mazoezi hayo katika kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua. Picha | JHU Hub.
Mazoezi yanayoshauriwa
Mazoezi hayo ni pamoja na kutembea kwa haraka, kuendesha baiskeli, kufanya shughuli za nyumbani, kulima au kufanya mazoezi maalumu kwa wale wenye fursa ya kufanya hivyo.
Hata hivyo, mwongozo huo umeeleza kuwa mazoezi hayo yafanyike kwa kuzingatia ushauri wa daktari.
Wizara ya Afya imeeleza kuwa kuushughulisha mwili na kufanya mazoezi kwa kiwango chochote ni bora kuliko kutokufanya kabisa.
Dondoo za afya
Kuushughulisha mwili na kufanya mazoezi kwa kiwango chochote ni bora kuliko kutokufanya kabisa.
Endapo wajawazito na waliojifungua hawatafikia kiwango cha kujishughulisha na mazoezi kinachoshauriwa, kuushughulisha mwili na kufanya mazoezi kwa kiwango chochote kuna faida
Wajawazito wanashauriwa kuanza kufanya mazoezi taratibu taratibu na kuongeza kadiri wanavyozoea. Mazoezi ya nyonga yafanyike kila siku ili kuimarisha njia ya uzazi na kuzuia tatizo la mkojo kutoka bila ridhaa.
Soma zaidi:
Epuka haya
Mjauzito anashauriwa kuepuka kufanya mazoezi au kuushughulisha mwili kwenye mazingira ya joto kali hususani kwenye mazingira ya unyevu nyevu na epuka kufanya mazoezi ukiwa umelala chali baada ya miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.
Kunywa maji ya kutosha kabla, wakati na baada ya kufanya mazoezi ili kuwa na maji ya kutosha mwilini. Epuka mazoezi na shughuli zinazoweza kukusababishia kugongana, kuanguaka, au kufanya mazoezi sehemu za miinuko endapo wewe si mkazi wa sehemu hizo.
Wanawake ambao kabla ya ujauzito wao walikua wanafanya mazoezi ya kiwango cha juu au ambao walikua wanashughulisha mwili, wanaweza kuendelea na vitendo hivyo wakati wa ujauzito na pia baada ya kujifungua.
Latest