Vijana katikati ya mapambano ya kuachana na dawa za kulevya Tanzania

December 14, 2022 6:03 am · Abdushakur
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakusanywa kwenye vituo maalum vya waraibu kuwasaidia kuacha.
  • Waraibu wapatao 905,902 walijitokeza kupata tiba ya uraibu wa dawa za kulevya mwaka 2021.
  • Waeleza ugumu wanaoupata kuacha kutumia dawa za kulevya. 

Mwanza. Naianza safari kutoka nembo kuu ya Jiji la Mwanza maarufu kama Round about ya Samaki iliyopo magharibi mwa Ziwa Victoria.

Nasonga mbele kwa mwendo wa dakika 27 kumaliza kilomita 2 kuelekea Kituo cha Vijana Wanaojitolea Kupambana na Tabia Hatarishi (Yovaribe)  kilichopo Mtaa wa Mission kata ya Furahisha Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Nikipiga hatua ya pili kutoka lango kuu la kuingilia kituoni hapo, nashangazwa kuona vijana nane wameketi mkao wa matumaini kuwa ipo siku watafikia dhamira yao ya kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa muda wa dakika tano nikisubiri taratibu za kiofisi, vijana wasiopungua 10 wanaingia. Wanne kati yao wanaingia kwa mwendo wa kudunda dunda ikiwa ni ishara kuwa miili yao tayari imeathirika na utumiaji wa dawa za kulevya.

“Nimetumia madawa ya kulevya takriban miaka 19 tangu nipo shule, dozi yangu kwa siku ilikuwa ni gramu 10 sawa na Sh90,000 na kila siku ilikuwa ni lazima kuipata kwa namna yeyote ile,” anasema Khalfan Kofii, mmoja wa vijana wanaopata tiba katika kituo hicho. 

Khalfan (jina siyo halisi) kwa uchungu ananijuza matarajio yake baada ya kupata nafuu dhidi ya matumizi ya dawa hizo.

“Lengo langu ni kumaliza tiba nikiwa salama, nioe, niwe na familia na nirudishe heshima yangu katika jamii,” anasema kijana huyo. “Kituoni hapa napata malezi mazuri yanayonijenga na kunihamashisha kuachana kabisa na dawa za kulevya.”

Khalfan ni miongoni mwa vijana 300 katika kituo cha Yovaribe  wanaoendelea kutumia dawa aina ya “Methadone” kwa lengo kuu la kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Methadone huzuia Arosto na kupunguza au kuondoa utegemezi wa dawa za kulevya. Hutolewa kama tiba na hupewa kwa wale wenye utegemezi wa dawa za kulevya ambapo ni mbadala salama wa dawa za kulevya wazotumia kama vile ‘heroin.’

Pia inawaweka huru kutoka kwenye kulazimika kutafuta dawa za kulevya na kuwapa fursa ya kuboresha maisha yao.

Akivalia shati zuri la mikono mirefu lenye mchanganyiko wa mistari yenye rangi nyeupe na nyekundu likinipa tafsiri  ya mabadiliko yake kimuonekano Khalfan ananijuza namna wanavyopata malezi bora kituoni hapo.

Dawa za kulevya zimekuwa zikikatisha ndoto za vijana. Elimu na msaada wa kisaikolojia unaweza kuwasaidia kutokuingia katika mtego huo. Picha | Clouds Media.

Khalfan anasema kuwa wanapata elimu ya kijamii na ujasiriamali, ili kujijenga kimawazo na kutambua fursa za kiuchumi zilizowazunguka.

Kabla ya kufika mbali ananijuza utofauti wa maisha kabla na baada ya kupata malezi imara kuelekea kukamilisha lengo lake la kuachana na utumiaji wa dawa za kulevya.

“Nimepoteza vitu vingi, uaminifu, jamii inakutenga, sikuweza kujitambua mwenyewe kuhusu usafi wangu lakini sasa muonekano wangu ni tofauti, uaminifu umerudi kati ya mimi na jamii inayonizunguka…,” anasema Khalfan.


‘Ni kusaidiana, kujitolea’

Kituo cha Yovaribe kimefanikiwa kuhudumia Waraibu 600 jijini Mwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2020.

Muathirika mwingine wa dawa za kulevya, Poyo Rashid (jina siyo halisi), anasema baada ya kupata tiba anafanya kila jitihada kuhakikisha anawasaidia wenzake wanafanikiwa kuachana na utumiaji wa dawa za kulevya.

“Furaha yangu kubwa ni kuendelea kuhakikisha wenzangu wanaoendelea kutumia watoke kule waje huku, wawe kama mimi kwa sababu kama ndiyo kwanza naanza yote niliyofanya nyuma yamefutika,” anasema Poyo, ambaye naye anapata matibabu katika kituo hicho.

Poyo ni miongoni mwa vijana wa mwanzo kusajiliwa na kupata dozi ya methadone kituoni hapo, na kutokana na malezi bora aliyopata amefanikiwa kuachana kabisa na matumizi ya dawa za kulevya.

“Dozi yangu kwa siku ilikuwa ni G mbili (gramu 20) sawa na Sh180,000 nilishiriki kazi haramu ili kupata pesa ya kumpa pusha (muuzaji wa dawa za kulevya), natamani angekuwa ananitunzia pesa zangu ili anirudishie,” anasema Poyo.

“Mwisho wa uteja ni sehemu kuu tatu taasisi (Sober House), jela ama kifo, tasisi ndiyo sehemu yetu kwa sababu jela haina faida, sehemu sahihi waje kwenye umoja wetu,”  amesisitiza Poyo.


Zinazohusiana;



Hali halisi kitaifa

Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2021 iliyotolewa Juni 2022 na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imesema ingawa hakuna takwimu halisi ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini waraibu wapatao 905,902 walijitokeza kupata tiba ya uraibu wa dawa mbalimbali za kulevya nchini katika mwaka 2021.

Tatizo la dawa za kulevya nchini, limeonekana kuwa kubwa katika maeneo ya ukanda wa Pwani na miji mikubwa kama vile Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Tanga, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mbeya.

“Hali hii inadhihirishwa na watumiaji wanaojitokeza kutafuta tiba katika vitengo vya afya ya akili katika hospitali za wilaya, mkoa na rufaa, nyumba za upataji nafuu (sober houses), vituo vinavyotoa tiba saidizi kwa waraibu wa heroin kwa kutumia dawa – MAT na asasi za kiraia,” imeeleza taarifa hiyo. 

Mwaka jana, dawa za kulevya zilizotumika zaidi ni bangi, dawa za kulevya jamii ya afyuni, cocaine, dawa tiba zenye asili ya kulevya, dawa mpya za kulevya (New Psychoactive Substances – NPS) na dawa za kulevya jamii ya amphetamine (ATS).

Matumizi ya dawa za kulevya husababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo ya akili, uraibu, moyo, ini na mapafu. Matumizi ya dawa za kulevya yanapojitokeza katika jamii husika huondoa utulivu na kusababisha; kukithiri kwa vitendo vya kihalifu katika jamii kama vile wizi, ukahaba, utapeli na uporaji.


Hatua zinazochukuliwa

Katika kipindi cha mwaka 2021, Tanzania imeendelea kukabiliwa na tatizo la dawa za kulevya ambazo ni bangi, mirungi, heroin, cocaine, methamphetamine na dawa tiba aina ya morphine.

DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imeendelea kukabiliana na biashara na uzalishaji wa dawa haramu za kulevya nchini kwa kufanya operesheni mbalimbali za ukamataji, uteketezaji, maboresho ya sheria, kufuatilia uendeshaji wa mashauri ya dawa za kulevya na kutoa ushahidi mahakamani. 

Pia, mamlaka kwa kushirikiana na Mamlaka zingine za udhibiti imefanya kaguzi ili kuzuia uchepushaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Mamlaka hiyo pia iliweza kubaini mitandao ya kihalifu ya ndani na nje ya nchi inayojihusiha na usafirishaji wa dawa za kulevya.


Tangazo:


Nini kifanyike?

Mratibu wa Yovaribe jijini Mwanza Sauly Ngwiki akizungumza na Nukta Habari ametoa wito kwa jamii kushiriki malezi kwa wanaopambana kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

“Mara nyingi tunakuwa na wazazi ili kumuwezesha kujua mabadiliko yanawezekana na matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuisha,” anasema Ngwiki huku akihimiza elimu kutolewa kwa jamii ya namna ya kuwasaidia waraibu na wengine kutokuingia katika matumizi ya dawa hizo.

“Elimu bado ni ndogo sana kwa watu ambao wanaishi na watu wanaotumia madawa ya kulevya,” anasema Ngwiki.

Maimuna Juma, mkazi wa Kata ya Luchelele, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza anashauri wazazi na walezi kurejesha imani kwa vijana waliokubali kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Maimuna, mama wa watoto watatu anasema kuwa kufanya hivyo kutawalea kifikra na kufanya kundi kubwa kukubali kubadilika dhidi ya jambo hilo huku mwenzake Rashid Abdallah, mkazi wa kata hiyo hiyo anashauri kuongezwa kwa idadi ya vituo vya kuwalea waraibu wa dawa za kulevya na kutanua wigo wa malezi kwa ajili yao.

Elimu ikitolewa ipasavyo jamii itazidi kuhamasika, kuwaamini na kuishi vyema na walio kwenye jitihada za kuachana na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Daktari Mariam Kahabi kutoka hospitali ya Rufaa Bugando  jijini Mwanza katika mazungumzo yake na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) amesisitiza umuhimu wa kutomtenga mtu wa kundi lolote wakiwemo waraibu.

“Unyanyapaa unaweza ukampelekea akawa na mawazo tofauti tofauti,  mawazo ya kujiua, kuonekana kama hafai, kufanya vitendo vya ajabu.

“Mtu akinyanyapaliwa kwa kila kitu kuna namna atajitengenezea mazingira kujiona kila kitu hawezi katika maisha yake, kila kitu kina kasoro kwake mwisho wa siku itampa changamoto kwenye akili,” anasisitiza Dk Kahabi.

Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza Oktoba 14, 2022 mkoani Kagera katika Wiki ya vijana Kitaifa alisema biashara na matumizi sugu ya dawa za kulevya nalo ni tatizo linaloendelea kuwaathiri Watanzania na kuilazimu Serikali kutumia fedha nyingi kwa matibabu ya waathirika.

“Hapa ndugu zangu pana gharama mbili kubwa. Gharama moja ni fedha inayotumiwa na Serikali kutibu watu hawa lakini gharama ya pili ni upotevu wa nguvukazi ya Taifa,” alisema Rais Samia.

Kutokana na hali hiyo alishauri kuongeza juhudi za malezi ili kuwanusuri vijana kuingia katika mtego huo huku mikakati ya kuwasaidia waraibu kuimarishwa ili kuwarejesha katika hali ya kawaida.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV