Watanzania wahimizwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya mfumo wa hewa
- Ni kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa hewa ikiwemo Uviko-19.
- Visa vya maambukizi ya Uviko-19 vyafikia 42,111 tangu uripotiwe kwa mara ya kwanza nchini.
Dar es salaam. Ikiwa zimesalia siku nne tu kuumaliza mwaka 2022, Watanzania wamehimizwa kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya hewa ikiwemo Uviko-19.
Taarifa ya salamu za sikukuu za mwisho wa mwaka iliyotolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu imeeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa hewa katika kipindi cha wiki ya kwanza ya Novemba na Disemba.
“Ufuatiliaji wa Wizara umeonesha kuwa visababishi vikuu vya magonjwa haya ni virusi vya Uviko-19 pamoja na virusi wengine wenye kusababisha mafua na kikohozi mfano virusi vya Influenza (Influenza viruses), “ inasomeka taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeonesha watu 71 kati ya 1,294 waliopima walikuwa wanaugua Uviko-19 katika wiki ya pili ya Disemba tofauti na watu 47 kati ya 1,154 waliokuwa wanaugua katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.
Soma zaidi:
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), mpaka leo Disemba 27, 2022 jumla ya Watanzania 845 wamepoteza maisha kwa ugonjwa wa Uviko-19 huku kukiwa na jumla ya visa 42,111 vya maambukizi.
Ummy katika taarifa hiyo pia imesema kuna ongezeko la wagonjwa wa Influenza kutoka asilimia 4.8 mwezi Novemba hadi asilimia 6.5 ambapo katika wiki ya pili ya Disemba, watu 10 kati ya 155, waliopima walikuwa wanaugua ugonjwa huo.
Tahadhari za kuchukua
Hatua za kujikinga na magonjwa hayo ambazo zinahimizwa ni pamoja na kupata dozi kamili ya chanjo ya Uviko-19 kwa ambao hawajachanja, hatua ambayo itawaepusha kupata ugonjwa huo na kifo.
Kuvaa barakoa pindi mtu anapokuwa na dalili za mafua au kikohozi na awapo kwenye mikusanyiko. Kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuzingatia kanuni za afya na usafi binafsi ni miongoni mwa njia za kujikinga.
Kwa mujibu wa WHO, kipindi kama hiki mwaka 2021 watu watatu waliripotiwa kupoteza maisha nchini Tanzania kutokana na Uviko-19 ingawa mwezi huu hakujaripotiwa kifo chochote tangu mwezi Agosti viliporipotiwa vifo vinne.