TRA yavunja rekodi makusanyo ya kodi
- Yafikia asilimia 99 ya lengo la kukusanya Sh12.48 trilioni mwaka 2022/23.
- Disemba yavunja rekodi ya kukusanya mapato mengi zaidi tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996.
Dar es salaam. Nusu ya mwaka wa fedha wa 2022/23 inaisha vizuri kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mara baada ya kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh12.46 trilioni sawa na asilimia 99 ya lengo la makusanyo.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022/23, mamlaka hiyo ilijiwekea lengo la kukusanya Sh12.48 trilioni.
Makusanyo hayo ya fedha huenda yakarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama elimu, afya na maji ambazo hutegemea fedha kutoka Serikalini.
Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata katika taarifa yake iliyotolewa Januari Mosi mwaka huu ameeleza kuwa kiasi kilichokusanywa ni ongezeko la Sh1.35 trilioni ikilinganishwa na kiwango kilichokusanywa kwa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2021/22.
“Ongezeko hili ni sawa na ukuaji wa makusanyo wa asilimia 12.2,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Zinazohusiana:
-
Namna ya kupunguza gharama za manunuzi ya vyakula, vinywaji msimu wa sikukuu
-
Mzazi fanya haya kumuandaa mtoto na muhula mpya wa masomo mwaka 2023
- Namna bora ya kupanga, kutimiza malengo yako mwaka 2023
Kwa mujibu wa TRA, mwezi Disemba imekusanya Sh2.77 trilioni kati ya lengo la kukusanya Sh2.60 sawa na ukuaji wa asilimia 10.3 ukilinganisha na makusanyo ya mwezi Desemba 2021.
“Pamoja na makusanyo haya kuvuka lengo la mwezi Desemba 2022, ndicho kiwango cha juu zaidi kukusanywa kwa mwezi tangu kuanzishwa kwa mamlaka mwaka 1996, “ amesema Kidata katika taarifa hiyo.
Makusanyo haya ya nusu ya mwaka wa fedha 2022/23 ni sawa na nusu ya mapato ya kodi na yasiyo ya kikodi yaliyopangwa kukusanywa na TRA katika bajeti ya fedha ya mwaka 2022/23.
Mfumo wa bajeti wa mwaka 2022/23 uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango unaonesha kuwa TRA inapaswa kukusanya Sh23.65 trilioni.