Sababu TRA kuvunja rekodi ya mapato 2024/25
- Mapato yaongezeka kwa asilimia 16.7, rekodi nne zavunjwa.
- Lengo jipya la 2025/26 lafikia Sh36.07 trilioni.
Dar es salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeandika rekodi mpya katika historia yake ya ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha 2024/25 baada ya kukusanya Sh32.3 trilioni.
Kiasi hicho cha makusanyo kwa TRA ni kikubwa kuwahi kufikiwa, kikiwa kinazidi lengo la makusanyo kwa asilimia 3.9 ambapo ililenga kukusanya Sh31.05 trilioni kwa mwaka huo.
Kiasi hicho cha makusanyo ni sawa na ongezeko la asilimia 16.7 ikilinganisha na Sh27.6 za mwaka 2023/24.
Katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2024/25 kuanzia Aprili hadi Juni 2025 TRA ilikusanya kiasi cha Sh8.2 trilioni dhidi ya lengo la Sh7.8.
Hii inafanya ongezeko la asilimia 15.8 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2023/24 ambapo jumla ya makusanyo ilikuwa Sh7.09 trilioni.
Nini siri ya mafanikio?
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, mafanikio haya yamechangiwa na ushirikiano imara na walipakodi kutimiza wajibu wao.
Ameahidi kuendelea kuimarisha mazingira rafiki ya kibiashara pamoja na kutoa elimu ya kodi kwa makundi yote kwa kusimamia usawa katika ulipaji kodi.
Mwenda ameeleza kuwa kuimarika kwa ufanisi wa watumishi wa TRA kwa kusimamia nidhamu, uwajibikaji, na ubunifu kazini kwa kuzingatia matumizi mazuri ya mifumo ya kisasa ya ushuru wa forodha (TANCIS) na kodi za ndani kumechagiza ongezeko hilo la kodi.

Sababu nyingine aliyotoa Mwenda ni watumishi wa TRA wamekuwa wakitoa muda wa ziada na kusikiliza walipa kodi kila alhamisi pamoja na kushughulikia kwa usahihi marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), taarifa na kodi za zuio (PAYE).
Mwenda ameainisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi na biashara uliochangiwa na kuimarika kwa huduma bandarini na forodha pamoja na kuongezeka kwa shehena ya mizigo inayoingia nchini kumechangia ukusanyaji wa mapato hayo.
Kuimarika kwa uhusiano na waendeshaji waliothibitishwa wa shuguli za kiuchumi (AEO’s) kumechangia ongezeko la mapato pia.
Malengo ni yapi kwa mwaka 2025/26?
Ili kuhakikisha kuwa hawarudi nyuma katika ukusanyaji wa mapato,TRA imesema ina lengo la kukusanya Sh36.07 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambapo mikakati ya kufikia hatua hiyo ni pamoja na kukamilisha utekelezaji wa Mfumo Shirikishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS).

Pia TRA imepanga kuendeleza ushirikiano na viongozi wa wafanyabiashara na wadau wa kodi pamoja na kuendeleza ushirikiano na timu ya maboresho ya kodi iliyoundwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan bila kusahau kufuatilia kwa karibu utendaji na maadili ya watumishi wake wote.
Latest



