Njia za kuiokoa Tanzania na janga la kufeli hesabu, sayansi

January 9, 2023 7:54 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Lugha ya kujifunzia na mtindo wa uulizaji maswali vyatajwa ni miongoni mwa sababu zinazofelisha wengi.
  • Wadau wa elimu washauri Serikali kuongeza walimu na kuchunguza  ubora wa walimu wa sayansi waliopo
  • Wazazi watakiwa kuwasaidia watoto wao kufaulu masomo ya sayansi

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine wanafunzi waliofanya mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) mwaka 2022 wameingia kwenye historia ya watoto waliowahi kufanya vibaya zaidi kwenye masomo ya sayansi na hesabu Tanzania.

Katika matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), kiwango cha ufaulu wa watoto hao siyo tu kuwa kimeshuka bali zaidi ya watahiniwa wanane kati ya 10 waliofanya mtihani huo Oktoba 2022 wamefeli Hisabati ama Basic Mathematics kwa kimombo dadi ambayo ni karibu sawa na wanafunzi waliofeli somo la Fizikia.   

Ufaulu wa jumla umeporomoka kutoka asilimia 92 mwaka 2021 mpaka asilimia 85 mwaka 2022 huku ufaulu wa masomo ya sayansi ukiwa chini zaidi ya wastani wa masomo yote. Miaka ya nyuma ufaulu ulikuwa na mwenendo wa kupanda mwaka hadi mwaka. 

Hali pia si shwari kwenye Kemia baada ya wanafunzi takriban saba kati ya 10 au asilimia 66 wakifeli somo la Kemia. Katika somo la Baiolojia nusu ya wanafunzi yaani asilimia 53 ya waliofanya mtihani nao walifeli somo la Baiolojia ambalo ni muhimu katika kufahamu bailojia ya binadamu, wanyama na mimea.

Sayansi, hesabu tatizo sugu

Hii si mara ya kwanza kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kufeli vibaya katika masomo ya hesabu na sayansi jambo linalotishia maendeleo ya Tanzania kupitia sayansi na teknolojia. 

Baadhi ya wadau wa elimu nchini Tanzania wameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa sababu za kushuka ufaulu ni pamoja na ugumu wa lugha ya kujifunzia sekondari ambayo ni Kingereza. 

Mdau wa elimu Mwalimu Richard Mabala amesema kuwa lugha ya kujifunzia pamoja na namna maswali yalivyoulizwa ni miongoni mwa sababu iliyosababisha wanafunzi hao kufeli.

“Wanafunzi hawa hata matokeo yao ya darasa la saba yalionesha ufaulu katika somo la Kiingereza umeshuka sasa sekondari wameenda kukutana na masomo magumu zaidi katika lugha ambayo hawaijui vema lazima wafeli tu, “ amesema Mabala ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu. 

Baadhi ya walimu wanaeleza kuwa mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa uulizaji maswali huenda ni miongoni mwa sababu zilizofanya wanafunzi hao wa kidato cha pili kufeli vibaya sayansi na hesabu. 

Mwalimu wa shule za Agha Khan jijini Dar es salaam Veronica Sarungi ameiambia Nukta Habari kuwa baada ya mtihani huo wa kidato cha pili alizungumza na wanafunzi na kumweleza kuwa mfumo waliokutana nao si ule waliokuwa wamewafundisha watoto hao. 

Lugha ni tatizo? 

“Maswali ni yale yale lakini yalikuwa katika mfumo wa mafumbo zaidi sasa mwanafunzi kwanza haifahamu vizuri hiyo lugha, halafu unamletea mfumo mgumu zaidi bila shaka hawezi kufaulu,” anasema Veronica na kubainisha kuwa mtihani wa mwaka jana una utofauti mkubwa na ile ya mwaka 2021 na 2020.

Wakati wadau hao wa elimu wakieleza hayo, Ripoti ya Uchambuzi wa Matokeo ya Shule ya Msingi ya mwaka 2020 iliyotolewa na Necta inaonesha somo la Kiingereza lilikuwa na ufaulu wa chini zaidi kuliko masomo yote likiwa na wastani wa asilimia 57. 

Hii inamaanisha kwamba ni takriban wanafunzi sita tu kati ya 10 ambao ndio wamefanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2022, walifaulu mtihani wa Kiingereza mwaka 2020 katika matokeo ya darasa la saba.


Zinazohusiana


Mbinu zitakazosaidia kuongeza ufaulu wa sayansi, hesabu

Baadhi ya wadau wa elimu wanaeleza kuwa mwarobaini wa tatizo hilo ni pamoja na Serikali kuongeza miundombinu rafiki kwa ajili ya wanafunzi kuelewa masomo ya sayansi na hesabu na kutazama upya lugha ya kufundishia ambayo mwanafunzi ataelewa.

“Ni wakati wa Serikali kuharakisha ukamilishaji wa sera ya lugha ya kujifunzia ili wanafunzi wasome kwa lugha wanayoielewa. Lugha inayotumika sana ni Kiswahili kwa kuwa hata nje ya masomo ndio hutumika zaidi katika nyanja zote za mwanafunzi huyu,” anasema Mabala ambaye ni mwandishi wa vitabu mbalimbali vikiwemo vinavyotumika shuleni. 

Mabala anaeleza kuwa Serikali inatakiwa kuongeza vitabu vya kiada na ziada vya masomo hayo ya sayansi na hisabati ili watoto wapate wasaa mzuri wa kujisomea na kufanya mazoezi. 

Ongeza walimu wenye ubora

Mbali na lugha ya kujifunzia, wataalamu wengine wanaeleza kuwa tatizo hilo litatuliwa iwapo Serikali itawekeza vilivyo katika kuongeza walimu wenye ubora katika masomo ya sayansi na hesabu. 

Mhadhiri wa Uhandisi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) Aviti Mushi anasema licha ya kwamba idadi ya walimu wa masomo ya sayansi kuwa si ya kuridhisha bado baadhi yao uwezo wao si wa kuaminika.

“Serikali inapaswa kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya sayansi na hesabu lakini lazima kuwe na namna ya kupima ubora wa walimu hawa kabla hawajakabidhiwa jukumu la kufundisha…huenda hata sasa katika walimu kumi wawili au mmoja hawana ubora unaotakiwa, “ anasema Dk Mushi ambaye pia huandika vitabu vya kufundishia shuleni vikiwemo vya fizikia.

Suluhu ya masuala ya shuleni pekee huenda isimalize tatizo. Mwalimu Veronica anashauri kuwa wazazi wanatakiwa kuwa chachu ya kuwahimiza watoto kusoma vema masomo ya sayansi na hisabati badala ya kuwaacha wakate tamaa. 

Wazazi msiwakatishe tamaa watoto

Sarungi amewashauri wazazi kuwa nguzo muhimu katika kuwatia moyo wanafunzi na kuwawezesha kwa vifaa na vitabu pale inapobidi na sio kuwapa kauli zinazowafanya wayachukie masomo ya sayansi na hesabu au kuyaona magumu zaidi.

“Mzazi anamwambia mtoto, umefeli hesabu usijari hata mimi nilifeli, mtoto anaona kumbe ni sawa tu kufeli. Hilo jambo sio sawa. Mzazi anatakiwa kumtia moyo kuwa leo umefeli kesho utafaulu ila ongeza bidii, hivyo ndivyo inavyotakiwa,” amesema Sarungi.


Tangazo:


Enable Notifications OK No thanks