Mate, jasho la mgonjwa aliyepona havisambazi virusi vya Ebola
- WHO wasema mgonjwa aliyepona Ebola hasambazi virusi hivyo.
- Hata hivyo, bado kuna ulazima wa kuchukua tahadhari juu ya gonjwa hilo.
Dar es Salaam. Hata wakati makali ya ugonjwa wa Ebola yakiendelea kupungua kwenye nchi nyingi zilizokumbwa na ugonjwa huo ikiwemo Uganda, bado taarifa za uzushi kuhusu ugonjwa huo zinaendelea kusambazwa na kuathiri watu.
Moja ya uzushi huo ni mate na jasho la mgonjwa aliyepona Ebola kusambaza virusi vya ugonjwa huo, jambo halina uthibitisho wa kitabibu.
Kwa mujibu wa Daktari Patrick Otim Ramadan kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Ofisi ya kanda ya Afrika, mate, jasho na damu ya mgonjwa aliyepona Ebola haviwezi kusambaza virusi hivyo.
“Mpaka mgonjwa wa Ebola akiruhusiwa kutoka wodini inamaanisha virusi havipo tena kwenye damu hivyo haviwezi kurudi kwenye mate au jasho,” amesema Dk Ramadhan.
Kwa wakati huo wanafamilia na jamii inayomzunguka mgonjwa huyo aliyekwisha kupona hawapo tena kwenye hatari ya kupata maambukizi mapya ya ugonjwa huo, kinyume na uzushi unaoendelea kusambazwa.
Hata hivyo, ikiwa mgonjwa wa Ebola ambaye bado hajapona vizuri au bado anaumwa anaweza kueneza vizuri hivyo kwa watu walio karibu naye kupitia damu, mate au jasho.
“Mtu ambaye bado anaumwa Ebola yupo kwenye hatari ya kuwaambukiza wengine na wala siyo mgonjwa aliyepona kama inavyoaminika,” amesema mtaalam huyo.
Soma zaidi:
- Tanzania na Uviko-19: Maambukizi yaongezeka kwa asilimia 62
- Watanzania wahimizwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya mfumo wa hewa
Njia za kujikinga na Ebola
Ili kuzuia maambukizi ya Ebola, WHO inawataka wahudumu wa afya kuvaa vifaa vya kujikinga wakati wa kumuhudumia mgonjwa wa Ebola pamoja na kuosha mikono baada ya kumuhudumia mgonjwa au kumtembelea.
Kuepuka kula nyama ambayo haijapikwa vizuri, kula nyama mbichi au mizoga na kugusa wanyama wenye maambukizi.