Idadi ya redio yazidi kupaa Tanzania
- Idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 17 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Redio leo Februari 13, 2022, redio ni chombo muhimu ambacho Watanzania wana kitumia kupata habari zinazowawezesha kufanya maamuzi katika maisha yao ya kila siku.
Licha ya kuongezeka kwa changamoto za kifedha zinazoendelea kuvikabili vyombo mbalimbali vya habari duniani, idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 17 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza katika ripoti mpya ya mawasilino ya robo ya mwisho ya mwaka 2021 kuwa hadi Desemba mwaka jana kulikuwa na vituo 210 vya redio nchini kutoka vituo 193 mwaka 2020.
Uchambuzi wa mwenendo wa takwimu za vituo vya redio uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) unaonyesha kuwa vituo vingi vya redio vilizaliwa mwaka 2016 baada ya vituo 42 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.
Hata hivyo, mwaka 2018 ndiyo mwaka ambao vituo vichache zaidi vilianzishwa ndani ya mwaka mmoja kutokana na kuongezeka kwa vituo viwili tu vya redio kutoka 156 mwaka 2017 hadi 158 mwaka 2018.