Wanafunzi 4 kati ya 10 wanafundishwa masomo kwa lugha wasiyoielewa
Elimu kwa lugha mama huwezesha wanafunzi kuziba pengo ya maisha kati ya nyumbani na shuleni. Picha | UNISFA.
- Unesco yasema asilimia 40 ya wanafunzi hawafundishwi kwa lugha wanayoifahamu.
- Yashauri hatua za kimataifa zichukuliwe kuwasaidia wanafunzi.
Dar es Salaam. Wakati mjadala wa Kiingereza na Kiswahili, ni lugha ipi ya hizo inafaa kufundishia Tanzania, imebainika kuwa wanafunzi wanne kati ya 10 duniani wanafundishwa masomo kwa lugha ambayo hawaielewi vizuri, jambo linaloathiri katika kupata maarifa na ujuzi utakaosaidia kuboresha maisha yao.
Baadhi ya wadau wa elimu wamekuwa wakihamasisha matumizi ya Kiswahili kufundishia kwa sababu ni lugha mama na inaeleweka na watoto wengi nchini. Hata hivyo, wengine wanaeleza kuwa Kiingereza ni lugha ya kimataifa hivyo kuna umuhimu wanafunzi kuitumia katika masomo yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Audrey Azoulay katika ujumbe wake wa siku ya lugha mama duniani hii jana amesema asilimia 40 ya wanafunzi duniani kote bado hawana fursa ya kufundishwa darasani kwa lugha yao wanayozungumza au wanayoelewa zaidi.
Amesema hali hiyo inadumaza kujifunza, kujieleza kitamaduni na kujenga mahusiano ya kijamii na vile vile kudhoofisha urithi wa lugha.
Kwa mujibu wa Azoulay, ni muhimu suala la lugha mama lipatiwe kipaumbele katika marekebisho ya mfumo wa elimu.

UNESCO imesema elimu inayotolewa kwa lugha nyingi ambayo hutokana na lugha mama hurahisisha ufikiaji na ujumuishwaji katika kujifunza kwa makundi ya watu wanaozungumza lugha zisizo za utawala, lugha za makundi madogo na lugha za asili.
Shirika hilo limesema sharti hili kwanza linahitaji ukusanyaji bora wa takwimu, ambazo zitafanya iwezekane kuchukua hatua maalum.
Zaidi ya yote, hata hivyo, UNESCO inasema inahitaji ufahamu wa jumla zaidi wa thamani isiyoweza kubadilishwa lakini dhaifu ya lugha na tamaduni mbalimbali ulimwenguni.
“Kila moja ya lugha zaidi ya 7,000 zinazozungumzwa na wanadamu hubeba ndani yake mtazamo wa kipekee wa ulimwengu wa vitu na viumbe, njia ya kufikiri na hisia kiasi kwamba kila kutoweka kwa lugha kunaleta hasara isiyoweza kurejeshwa,” amesema Azoulay.
Siku ya kimataifa ya lugha mama inatambua kwamba lugha na wingi wa lugha vinaweza kuendeleza ushirikishwaji na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya kutomwacha mtu yeyote nyuma.
Unesco inahimiza na kuchagiza elimu kwa lugha mbalimbali kulingana na lugha mama au lugha ya kwanza.
“Ni aina ya elimu inayoanzia katika lugha ambayo mwanafunzi huimiliki zaidi na kisha kutambulisha lugha nyingine hatua kwa hatua. Mbinu hii huwawezesha wanafunzi ambao lugha yao mama ni tofauti na lugha ya kufundishia ili kuziba pengo kati ya nyumbani na shuleni, kugundua mazingira ya shule katika lugha iliyozoeleka, na hivyo, kujifunza vizuri zaidi,” imeeleza Unesco.