Hapana: Tanzania haidaiwi zaidi ya Sh10 trilioni na benki ya Umoja wa Ulaya
- Baadhi ya watu wasambaza uzushi kuwa Tanzania inadaiwa kiasi hicho cha pesa.
- Serikali yasema siyo sahihi ikishindwa kutaja kiwango inachodaiwa na benki hiyo.
Dar es Salaam. Wizara ya Fedha na Mipango nchini Tanzania imewataka wananchi kupuuzia taarifa zinazoenea kupitia mitandao ya kijamii kuwa Serikali inadaiwa Dola za Marekani bilioni 4.1 za Marekani (zaidi ya Sh9.594 trilioni) na Benki ya Umoja wa Ulaya (EIB).
Kupitia ukurasa wa Twitter unaotambulika kama Tanzania Abroad Tv, Machi 4 mwaka huu ulichapisha taarifa hiyo ikiwa imeambatana na barua kutoka EIB inayoonesha madai hayo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja katika taarifa yake aliyoitoa Machi 6 mwaka huu amesema mara kwa mara ukurasa huo umekuwa ukitoa taarifa za uzushi, upotoshaji na uzandiki kuhusiana na wizara hiyo na Serikali kwa ujumla.
“Tunawaomba Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa mpuuze taarifa hizo, ambazo hazina ukweli wowote na kwa vyovyote zinalenga kupotosha umma na kuleta taharuki zisizo na msingi, “ inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa pamoja na kuwa EIB ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini na ina mahusiano mazuri na Serikali haina mkopo wa kiasi kilichotajwa ma mtandao huo.
Mwaipaja amewakumbusha na kuwaonya wamiliki na watoaji wa habari kupitia mitandao ya kijamii kuepuka kuchapisha habari za uzushi, na potofu kwani ni kinyume na Sheria ya Vyombo ya Habari ya mwaka 2016.
KANUSHO: IPUUZENI? pic.twitter.com/eFXNUM1yY5
— Ministry of Finance Tanzania (@mofURT) March 6, 2023
Zinazohusiana:
-
Hapana: Serikali haijatangaza kazi za ukarani sensa ya watu na makazi
-
5G inasambaza corona? Hapana, ni uzushi
Hata hivyo Nukta Fakti imefanya uchunguzi na kubaini barua hiyo ni feki kutokana na sababu zifuatazo:
Haina mwandiko rasmi
Barua zote rasmi huwa na aina moja ya mwandiko (font) ambayo huteuliwa na taasisi husika na kupitishwa kutumika katika shughuli zake zote ambapo katika barua hiyo imetumika miandiko mitatu tofauti na barua rasmi za benki ya EIB.
Lugha isiyo rasmi
Pamoja na mwandiko, barua hutumia lugha rasmi kwa sababu ndiyo nguzo muhimu ya mawasiliano. Uchunguzi wetu umebaini kuwa licha ya barua hiyo kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza bado haikufuata taratibu za kiuandishi wala kutumia lugha rasmi tofauti na barua za taasisi hiyo kubwa ulimwenguni.
Kufutwa futwa kwa baadhi ya maneno
Neno ‘confidential’ ambalo humaanisha siri, katika barua hiyo limefutwa futwa katika maeneo ambayo sentensi za barua hiyo zinapita. Hiyo inaongeza wasiwasi wa uhalali wa barua hiyo kwani neno hilo huwa kama kivuli ambapo maneno mengine huandikwa juu yake bila shida.
Kutokana na sababu hizo Nukta Fakti imebaini habari hiyo ni potofu na ya kupuuzwa, licha ya kuwa Serikali haijaweka wazi ni kiasi gani inadaiwa na benki hiyo.
Latest