Lhrc yajitosa mchakato usioridhisha upatikanaji wa haki mahakamani

Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda amesema kuna watu wengi waliopo magerezani kwa muda mrefu kwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ambao baadhi yao ni masheikh na viongozi wa dini ya kiislamu bila kupata haki zao. Picha | Daudi Mbapani.
- Ni baada ya watuhumiwa wa kesi ya ugaidi kusota gerezani kwa miaka 7 bila kusikilizwa.
- Yatoa wito kwa Serikali kufuta mashtaka yaliyopo kwa muda mrefu.
Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (Lhrc) kimepinga mchakato usioridhisha wa upatikanaji wa haki mahakamani unaosababisha baadhi ya watuhumiwa kutumia muda mrefu gerezani na wengine kupoteza maisha kabla ya kuhukumiwa.
Hayo yamejiri ikiwa ni siku chache mara baada ya kifo cha Sheikh Said Mohamed Ulatule (80) aliyetuhumiwa kosa la ugaidi na kuwekwa mahabusu katika gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam kwa miaka saba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Lhrc, Anna Henga aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 15, 2023 jijini Dar es Salaam amesema kitendo hicho ni kinyume na haki za binadamu na ikiwa mtuhumiwa anakosa basi ashtakiwe na mujibu wa sheria.
“Sio kwamba tunatetea uwepo wa ugaidi lakini ugaidi usitumike kama kigezo cha kuvunja haki za baadhi ya watu…tunachokikataa ni mtuhumiwa kukosa haki ya kusikilizwa mahakamani,” amesema Wakili Henga.
Kwa mujibu wa kituo hicho, marehemu Sheikh Ulatule aliyekuwa mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani pamoja na watu wengine sita kutoka kwenye familia hiyo walikamatwa kwa kutuhumiwa kujihisha na ugaidi miaka saba iliyopita.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda amesema kuna watu wengi waliopo magerezani kwa muda mrefu kwa wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ambao baadhi yao ni masheikh na viongozi wa dini ya kiislamu bila kupata haki zao.
“Watu waliowekwa ndani kwa muda mrefu wengi ni masheikh wa kiislamu na viongozi wa dini ambao wamekaa gerezani kwa zaidi ya miaka sita wakituhumiwa kuwa magaidi,” amesema Sheikh Ponda.
Viongozi wa dini wanaotuhumiwa kwa makosa ya ugaidi ni pamoja na masheikh pamoja na waumini wao 70 waliopo kwenye gereza la Ukonga, 23 waliopo Tanga, 23 waliopo Arusha pamoja na wengine waliopo mikoa ya Mwanza, Mtwara na Tabora.
Soma zaidi
Lhrc yatoa wito kwa Serikali
Lhrc kwa kushirikiana na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania kimetoa wito kwa Serikali na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kufanya jitihada mbalimbali kuboresha haki za wafungwa ikiwemo kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuwakamata watuhumiwa na kufuta mashtaka yaliyopo kwa muda mrefu.
“Serikali iwaachilie huru au iwape haki ya kujitetea mahakamani watuhumiwa wote waliokaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja bila ya mashauri yao kusikilizwa ikiwemo familia ya Ulatule,” amesema Henga.
Pia kituo hicho kimetaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina (Inquest) juu ya chanzo cha kifo cha marehemu Sheikh Ulatule na watuhumiwa wengine wanaopoteza maisha wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Pamoja na hayo Lhrc imetoa wito kwa Kamati ya Haki Jinai inayoendelea na zoezi la kukusanya maoni nchini kupendekeza kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuachiwa huru kwa watuhumiwa wote wa makosa ya ugaidi waliokaa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Baadhi yao hivi sasa wamefikisha miaka 10 bila kesi zao kusikilizwa, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) awaachie huru hasa kwa vile viashiria vingi vinaonesha uwepo wa uonevu badala ya ukweli,” amesema Henga aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo hayo.