Bajeti ya Tamisemi yapaa kwa Sh336 bilioni

April 14, 2023 2:00 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeongezeka kutoka Sh9.04 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh9.14 trilioni mwaka 2023/24.
  • Asilimia 38 ya bajeti hiyo kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
  • Wabunge wasema Serikali itoe kwa wakati pesa za bajeti. 

Dar es Salaam. Huenda huduma  na miradi inayotekelezwa chini ya Wizara ya  Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikaimarika na kutoa unafuu kwa wananchi katika mwaka ujao wa fedha, ikiwa Bunge litaidhinisha kiasi cha Sh9.14 trilioni zilizoombwa na wizara hiyo.

Huduma za kijamii kama elimu, afya, na miundombinu zinaweza kuimarika zaidi ikiwa kutakuwa na matumizi sahihi ya fedha zilizoombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kuwa bajeti ya wizara hiyo imeongezeka kwa zaidi ya Sh336 ikilinganishwa na ya mwaka 2022/23.

Waziri wa Tamisemi Angellah Kairuki aliyekuwa akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 leo Aprili 14 2023, amewaambia wabunge kuwa kati ya Sh9.14 trilioni  inayoombwa, Sh3.48 trilioni ni mahususi kwa shughuli za maendeleo sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.

“Jumla ya Sh3.48 trilioni  zinaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo, Sh2.36 trilioni ni fedha za ndani huku Sh1.12 trilioni zikiwa ni fedha za nje,” amesema Kairuki bungeni jijini Dodoma 

Jumla ya Sh218.5 bilioni  imeongezeka katika  fedha  ya miradi ya maendeleo inayoombwa kwa mwaka 2023/24, kutoka Sh3.26 trilioni iliyoombwa mwaka 2022/23  ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 64.


Soma zaidi:


Pamoja na kuongezeka kwa fedha katika miradi ya maendeleo, fungu la matumizi ya kawaida ya wizara nalo limeongezeka kwa Sh146.9 bilioni kulinganisha na Sh 5.51 trilioni  ya mwaka 2022/23.

Matumizi hayo yanahusisha mishahara ya walimu, mishahara ya Ofisi ya Rais Tamisemi pamoja na watumishi wa ngazi ya  halmashauri 184 nchini Tanzania ambayo yatagharimu jumla ya Sh5.65 trilioni.

Vipaumbele vya wizara

Kwa mujibu wa Kairuki baadhi ya vipaumbele vya Tamisemi kwa mwaka 2023/24 ni pamoja na kusimamia utawala bora, kukuza demokrasia, kushirikisha wananchi na ugatuaji madaraka, kuratibu maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuratibu ulinzi na usalama wilayani na mikoani.

Bajeti ya Tamisemi kwa mwaka 2023/24 endapo itapitishwa itakuwa sawa asilimia 20 ya bajeti yote ya Serikali Kuu ya Sh44.4 trilioni.

Waziri wa  Tamisemi Angellah Kairuki akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi  na Mbunge wa Mikumi Dennis Londo mara baada ya kuwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Tamisemi  kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024. Picha l Tamisemi

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi Dennis Londo amesema kamati yake imefurahishwa kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Tamisemi, jambo litakalorahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 

Ameishauri Tamisemi kukamilisha ujenzi wa maboma ya vituo vya afya, zahanati pamoja na shule ambayo wananchi walijitolea ambayo bado hayajamaliziwa kutokana na Serikali kutopeleka fedha kama ilivyoahidi.

“Kamati inaishauri Serikali kupeleka fedha za kumalizia maboma hayo, ili kuepuka hasara inayoweza kutokea ya kuchakaa kwa majengo hayo kabla hayajatumika,” amesema Londo.

Enable Notifications OK No thanks