Majaliwa aingilia kati sakata kelele zilizopitiliza nyumba za ibada

May 7, 2023 6:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Aagiza suala litatuliwe na Jumuiya ya Maridhiano na Amani.

Dar es Salaam. Kufuatia malalamiko kuhusu kuongezeka kwa kelele katika nyumba za ibada zinazoleta usumbufu kwa watu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala hilo liachwe litatuliwe na Jumuiya ya Maridhiano na Amani.

Maeneo mengine ambayo yanalalamikiwa kwa kelele na mitetemo ni pamoja na  nyumba za starehe na kumbi za burudani.

Majaliwa amesema shughuli za dini ziendelee kufanyika kama kawaida na suala la uratibu wa jambo hilo katika nyumba za ibada liendelee kuratibiwa na viongozi wa dini wenyewe kupitia Jumuiya ya Maridhiano na Amani.

“Serikali itaendelea kushauriana na jumuiya ya maridhiano na amani katika kuona namna bora ya kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia mahitaji ya jamii na kulinda afya za Watanzania,” amesema Majaliwa Mei 6, 2023 kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 101 ya hayati Mwalimu Nyerere lililofanyika mkoani Dodoma.

Tamko hilo la Serikali limetolewa wakati Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashughulikia malalamiko kuhusu ongezeko la kelele na mitetemo zikiwemo zile zinazotoka katika nyumba za ibada. 

NEMC imekuwa ikichukua hatua ikiwemo kuzifungia baadhi ya nyumba za starehe zinazokiuka utaratibu na kuzipiga faini.

Wiki hii baa za wazi za Rainbow na Chako ni Chako Pub za Jiini Dodoma zilifungiwa baada kukuta kelele zilizo kinyume cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 20 va mwaka 2004 na kanuni ya viwango vya udhibiti wa kelele na mtetemo ya mwaka 2015.

Katika kudhibiti kelele na mitetemo kutoka katika kumbi za starehe, Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa maelekezo mahususi yaliyolenga kudhibiti mitetemo iliyopitiliza katika kumbi za starehe hapa nchini. 

Maelekezo hayo yameainisha jinsi uratibu unavyopaswa kufanyika katika nyumba za ibada kwa kuwaomba viongozi wa dini kupitia kamati za amani kujadili suala la kelele na mitetemo iliyopitiliza kutoka kwa baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuendesha shughuli zao. 

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dk Samuel Gwamaka Machi 10, 2023 alizitaka kumbi za burudani na nyumba za ibada kutumia vidhibiti sauti ili kuepuka kelele chafuzi za Mazingira.

“Kelele za muziki zilizoruhusiwa kisheria na kwa mujibu wa kipimo ni decibel 40, na haitakiwi kuzidi, ikizidi hapo inaleta athari kwa jamii inayozunguka eneo hilo hasa ukiziwi,” alisema Dk Gwamaka.

Aidha amewataka wananchi kutoa ushirikiano katika utoaji wa taarifa za kelele zinazozidi viwango na kuleta usumbufu kwenye jamii ili kwa pamoja tuweze kutatua kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

Enable Notifications OK No thanks