Vyakula vyachangia kushusha mfumuko wa bei Tanzania
- Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Mei 2023 imeshuka hadi asilimia 4 kutoka asilimia 4.3 iliyorekodiwa.
- Kushuka huko kumechangiwa na kushuka kwa bei za bidhaa za chakula na zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini imepungua hadi asilimia 4% katika mwaka ulioishia Mei 2023 kutoka asilimia 4.3 iliyorekodiwa Aprili mwaka huu ikichangiwa zaidi na kushuka kwa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Kuendelea kushuka kwa kasi ya mfumuko wa bei angalau kunaenda kutoa ahueni kwa walaji ambao walikuwa wakilazimika zaidi kutoboa mifuko yao ili kuweza kumudu gharama za msingi za bidhaa na huduma kama chakula.
Kiwango hicho cha mfumuko wa bei kilichorekodiwa Mei ni kidogo zaidi kuripotiwa ndani ya mwaka mmoja kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Mara ya mwisho kasi ya mfumuko wa bei wa taifa wa asilimia 4 iliripotiwa katika mwaka ulioishia Mei 2022 na tangu wakati huo mfumuko wa bei ilikuwa ukipanda mwezi hadi mwezi.
Kiwango cha juu zaidi cha mfumuko wa bei kuwahi kuripotiwa tangu Mei 2022 ni kile kilichorekodiwa Oktoba na Novemba 2022 na Januari mwaka huu cha asilimia 4.9.
“Kasi ya mfumuko wa bei wa vyakula na vinywaji visivyo vya kilevi ya Mei 2023 ilishuka hadi asilimia 8.5 kutoka asilimia 9.1 ambayo ilirekodiwa Aprili 2023,” inasomeka sehemu ya taarifa ya NBS iliyotolewa leo Juni 9, 2023.
Zinazohusiana:
Malengo ya Tanzania kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika mwaka wa fedha wa 2022/23 yalikuwa ni kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei hauzidi kasi ya asilimia 5.4%.
NBS inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa zote na huduma bila kujumuisha vyakula na vinywaji visivyo vya kilevi kwa mwaka unaoishia Mei 2023 pia ulishuka hadi asilimia 2.1 kutoka asilimia 2.3 ilirekodiwa Aprili 2023.
Mfumuko katika nchi nyingi ulimwenguni umekuwa ukipanda mwezi hadi mwezi ukichagizwa zaidi na madhara ya Uviko-19 na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine ambavyo kwa pamoja viliathiri mnyororo wa thamani wa sekta ya uchukuzi.
Baadhi ya bidhaa zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei katika mwaka ulioishia Mei 2023 ni pamoja na ngano kutoka asilimia 7.7 hadi asilimia 5.3, mchele (kutoka asilimia 31.2 hadi asilimia 23.8), ulezi (kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 1.3) na mahindi kutoka asilimia 44.8 hadi asilimia 36.0.
Latest



