Rais Samia awataka wananchi Mwanza kutoa ushirikiano

June 14, 2023 3:14 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
  • Miongoni ni daraja la Kigongo- Busisi na meli ya MV- Mwanza.
  • Kukamilika kwake kutafungua nchi kiuchumi.

Mwanza. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi mkoani Mwanza kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kukamilisha miradi ya maendeleo inayojengwa kwa kuwa itasaidia kuifungua nchi kiuchumi.

Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), daraja la Kigongo-Busisi pamoja na meli ya Mv Mwanza inayotarajiwa kufanya mageuzi ya usafiri wa majini katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo ya maendeleo jijini Mwanza leo Juni 14,2023 amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuifungua nchi kiuchumi na kukuza pato la Taifa na mtu mmoja mmoja.

“Tunajenga meli, tunajenga bandari, tunajenga reli, tunajenga mabarabara. Haya yote sio mapambo, haya yote yatumike tufungue uchumi wetu Tanzania,” amesema Rais Samia.

Kutokana na miradi hiyo ya inayoendelea mkoani Mwanza Rais Samia ametoa wito kwa wakazi mkoani humo kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mazao ya kutosha yatakayotumia miundombinu hiyo kuwafikia walaji.

“Ningesimama tu ningewaambia zalisheni mngeniuliza tunauza wapi … miundombinu hii sasa inakwenda kupeleka sokoni kila kinachozalishwa Tanzania,” ameongeza Rais Samia.

Leo ni siku ya pili Rais Samia akiwa jijini Mwanza, ambapo alianza kwa kuzindua tamasha la ngoma za asili za Jamii ya Kisukuma maarufu kama Bulabo, na anatarajiwa kukagua mradi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa jijini Mwanza unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kesho Juni 15, 2023. 


Soma zaidi


Daraja Kigongo-Busisi kukamilika 2024

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mohamed Besta, mradi huo wenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.6 unatarajiwa kukamilika Februari 24, 2024 kwa gharama ya Sh716 bilioni. 

“Gharama hizi zinajumuisha Sh699.3 bilioni gharama ya mkandarasi, Sh11.1 bilioni gharama ya mhandisi mshauri, Sh3.14 bilioni fidia zilizolipwa kwa wananchi na Sh2.8 bilioni kwa ajili ya usanifu,” amesema Besta

Mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 75 ikiwa ni mwaka wa tatu tangu utekelezaji wake uanze mwaka 2020 chini ya mkandarasi kutoka nchini  China ambapo umechelewa kukamilika kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo janga la Uviko-19, ongezelko la kina cha maji Ziwa Victoria na hali ya jiolojia.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks