Rais Samia: Tanzania, India, kufungua ushirikiano maeneo ya kimkakati

October 9, 2023 12:09 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema ziara yake ni uthibitisho wa kuimarisha ushirikiano uliopo.
  • Baadhi ya maeneo ya ushirikiano ni pamoja na ulinzi na usalama, elimu, afya, kilimo na maji.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake imepanua wigo wa ushirikiano na India katika maeneo ya kimkakati ili kuchochea zaidi uwekezaji na kukuza biashara baina ya mataifa hayo mawili.

Rais Samia aliyeziarani nchini India kwa mwaliko wa Rais wa taifa hilo Droupadi Murmu, amewaambia wanahabari leo Oktoba 9, 2023, kuwa India imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo nchini Tanzania tangu kuasisiwa kwa ushirikiano baina yao takribani miongo sita iliyopita.


Soma zaidi: Rais Samia atoa miezi sita kutokomeza mgao wa umeme Tanzania


“Tunatarajia mengi kutokana na ziara hii, tumepanua zaidi wigo wa ushirikiano, kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi pamoja na ya kisiasa…tumekubaliana kupanua zaidi mawanda ya ushirikiano wetu katika maeneo ya kimkakati,” amesema Rais Samia.

Baadhi ya maeneo ya kimkakati yaliyoainishwa na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, mapema hii leo baada ya hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ushirikiano ni pamoja na ulinzi na usalama, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji, na kilimo.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa ushirikiano baina ya mataifa haya mawili mwanzoni mwa miaka ya 1960, Tanzania imenufaika katika masuala ya usambazaji wa maji safi na salama, ulinzi na usalama pamoja na biashara ya mazao ya kilimo.

Kwa mujibu wa Rais Samia, India inashika nafasi ya tatu kwenye mapato ya biashara baina ya Tanzania na India yakiwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na Sh7.76 trilioni za Tanzania.

Aidha, India imesajili jumla ya miradi 630 ya uwekezaji nchini Tanzania yenye thamani ya Dola  za Marekani bilioni 3.7 sawa na Sh 9.26 trilioni za Tanzania na kuifanya India kushika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini.

Aipongeza India kuipigia debe Afrika G20

Sambamba na hayo, Rais Samia ametumia fursa hiyo kuipongeza India kwa kuwa wenyeji wa mkutano wa Umoja wa Nchi zilizoendelea kiviwanda (G20) ambapo India iliipigia chapuo Afrika kupata uanachama kwenye umoja huo.

Rais Samia anatarajiwa kuhitimisha ziara yake kesho kutwa  Oktoba 11, 2023 ambapo ameahidi kurejea nchini humo katika mkutano wa India na mataifa ya Afrika ambapo tayari Rais Samia amethibitisha ushiriki wake.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW