Rais Samia awatembelea wahanga Hanang, aagiza kufanyika kwa uchunguzi wa chanzo cha mafuriko

December 7, 2023 3:07 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Atembelea kijiji cha Katesh, kambi ya wahanga na hospitali ya wilaya Tumaini.
  • Aagiza kikosi cha  ukoaji kujinoa, Serikali kutafuta chanzo cha mafuriko.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewatembelea wahanga wa mafuriko ya matope yaliyotokea katika Wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kuagiza kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha mafuriko hayo.

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea Rais Samia leo Disemba 7, 2023 ni pamoja na kijiji cha Katesh, kambi ya wahanga iliyowekwa katika shule ya msingi Katesh pamoja na hospitali ya wilaya ya Tumaini iliyopo Hanang.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Katesh Rais Samia amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi hao hadi pale watakapopata makazi rasmi.

“Nimekuja kama mkuu wa nchi kuona kilichotokea, nimekuja kuwapa faraja…kama Serikali tupo nanyi tangu jambo lilipotokea tutakuwa nanyi mpaka tukahikishe kila mmoja amekaa mahali anapostahili,” amesema Rais Samia.

Rais Samia akizungumza na wahanga wa mafuriko ya matope wilayani Hanang.Picha|IkuluMawasiliano

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama aliyekuwa akitoa tathmini ya madhara ya mafuriko hayo amesema idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko hayo imefikia 76 huku majeruhi wakiwa 117 kutoka kaya 1,150 zenye watu 5,600. 

Mbali na vifo pamoja na majeruhi mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa ekari 750 za mashamba, shughuliza kicuhumi imiwemomaduka na mapsoko amoja na vifo vya  mifugo

Rais Samia atoa maagizo kwa wizara, wakuu wa mikoa

Kufuatia madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo Rais Samia ameagiza kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo hatarishi pamoja na fanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha mafuriko hayo.

“Taarifa za uchunguzi za kupata kiini lakini na kina cha janga hili ziharakishwe zipatikane kwa mapema ili tujue tunachukua hatua zipi,” ameagiza Rais Samia.


Soma zaidi:Umemejua unavyookoa maisha ya wajawazito Iringa


Aidha, Rais Samia ameagiza kitengo cha maafa na uokoaji kilichopo chini Waziri Mkuu kujinoa zaidi ili kuongeza uwezo wake katika kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoweza kutokea nchini.

“Tuhakikishe sasa tunaongeza uwezo wetu wa kukabiliana na maafa kwa vifaa na utaalamu…

…Hili liwe funzo kwetu Serikali tujipange mapema…wote muwe na taarifa kamili ili kuepuka majanga hayo yasitukute tukiwa hatujajitayarisha    angalau tukijua kuna dalili hizo tunawea kuchukua  hatua za mapema “

Huduma za maji, afya, chakula na malazi ni maeneo mengine ambayo kiongozi huyo wa nchi amepaza sauti kwa viongozi wa Serikali kuhakikisha zinapatikana kwa uhakika ili kuimarisha afya za wahanga wakati wote wawapo kwenye kambi hizo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW