Kwanini usherekee sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na familia?
- Ni pamoja na kuimarisha mahusiano ya kindugu na kupunguza msongo wa mawazo.
Dar es Salaam. Msimu wa sikukuu ndiyo kipindi pekee ambacho baadhi ya familia hukutana na kusherekea pamoja huku wakipanga mipango mbalimbali ya mbeleni.
Hata hivyo, kuna wale ambao hupenda kusherehekea kivyao kwa kusingizia wingi wa gharama za kusafiri kuzifikia familia zao, majukumu ya kikazi au kwa sababu yoyote wanayoona ina mashiko.
Baadhi ya vijana hususan mabachela huona kama kusheherekea pamoja na familia ni jambo lililopitwa na wakati bila kujua wanapoteza faida kede kede ambazo zingewafaa katika maisha yao.
Ni zipi basi faida za kusherekea pamoja na familia? Zifuatazo ni dondooo chache tulizokuandalia ambazo pengine zinaweza kubadili mawazo yako na kukufanya uungane na familia yako katika msimu huu wa sikukuu.
Soma zaidi:Namna ya kupunguza gharama za manunuzi ya vyakula, vinywaji msimu wa sikukuu
Kuimarisha mahusiano ya kindugu
Kwa baadhi ya watu majukumu ya kila siku huwafanya washindwe kuonana na ndugu zao kwa muda mrefu sana, hivyo msimu wa sikukuu huwa ni kipindi pekee ambacho ofisi za Serikali pamoja na taasisi binafsi hutoa likizo fupi kwa wafanyakazi wao kujumuika na familia zao.
Kwa baadhi ya watu kama Evelyn Shayo mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye ni mwenyeji wa mMkoa wa Kilimanjaro, umbali ni sababu nyingine inayomzuia kuwa karibu na ndugu zake hivyo hutumia sikukuu za mwisho wa mwaka kuungana nao.
“Ndiyo maana mimi napenda kwenda nyumbani (Kilimanjaro) kila mwisho wa mwaka kule nakutana na ndugu zangu wote hususan wale waliopo mikoa ya mbali…
…Tunazungumza, tunafurahi, napata kusikia mipango yao na kama kuna changamoto au migogoro pia tunasuluhisha,” amesema Shayo.
Kupunguza msongo wa mawazo
Kwenye maisha kuna kupanda, kushuka na misukosuko ya hapa na pale ambayo wakati mwingine huweza kusababisha msongo wa mawazo ambao usipokuwa makini unaweza kukaa nao kwa muda mrefu na kukusababishia magonjwa ya afya ya akili.
Usilolijua ni kwamba kusherekea sikukuu pamoja na familia kunaweza kupunguza msongo wa mawazo na kukufanya kuanza mwaka mpya kwa kishindo.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (Unicef) kutenga muda wa kufurahi pamoja na familia huufanya mwili kuzalisha kemikali ya endorphin ambayo hupunguza msongo wa mawazo.
Mwanasaikolojia Susan Sanka, ameiambia Nukta Habari kuwa kushehereka pamoja na familia hutoa wasaa kwa watu kueleza matatizo yao na kupata suluhu jambo ambalo hupunguza msongo wa mawazo waliokuwa nao kwa muda mrefu.
“Kupitia familia baadhi ya watu wanaweza kupata suluhisho la matatizo yao ambayo yalikuwa yanawapa stress (msongo wa mawazo) au wengine ile kukaa tu pamoja na ndugu wanakuwa na furaha na kupata mbinu za kumanage(kuzuia) hiyo stress,” anafafanua Sanka.

Kusherekea pamoja na familia kunaongeza furaha na kukupa namna bora ya kukabiliana na mambo mapya.Picha|Shuterstock.
Kurithisha tamaduni na desturi za kifamilia
Baadhi ya makabila wana tamaduni na desturi zinazofaa ambazo ni ngumu kuziendeleza ikiwa hawana mazoea ya kukutana pamoja na kufundisha vijana na watoto wao.
Ukifuatilia kwa makini, vijana wengi hivi sasa hawajui tamaduni muhimu za asili yao ikiwemo lugha au miiko, kwa kiasi fulani hali hiyo inachangiwa na wanafamilia kutokutana kwa muda mrefu zaidi ambapo watu wangeweza kujifunza vitu mbalimbali kuhusu asili yao.
Kwa mujibu wa Evelyn ambaye ni mchaga, kila sikukuu familia yake ina utaratibu wa kupika vyakula na vinywaji vya asili ya kabila lao ambapo vijana hufundishwa jinsi ya kuviandaa.
“Kila sikukuu hapa nyumbani tunapika ‘macharali’ (ndizi) yenye nyama nyingi bila kusahau ‘mbege’(kinywaji kinachotengenezwa na ndizi mbivu, ulezi na maji) mpya mpya ambayo haina kilevi ili kila mtu aweze kunywa …
…Hii kazi hufanywa na wakina baba na wakinamama na wakati wote vijana wanakuwepo karibu kusaidia na kujifunza,”ameongeza Everln.
Kujifunza zaidi kuhusu maisha
Kuishi kwingi ni kuona mengi, kupata fursa ya kujumuika na wazee au watu wazima katika jamii fulani ni fursa tosha ya kujifunza mambo mengi kuhusu maisha.
Hii inaweza kuhusisha, namna bora ya kuishi na watu, majukumu na ujuzi mbalimbali kuhusu maisha ni miongoni mwa madini unayoweza kuyachota kutoka kwa watu waliokuzidi umri.
“Unakuta wengine huko nje hawaaminiki katika kufanya majukumu fulani lakini ile kukutana kwa familia na kupewa majukumu ya kufanya kunamfanya ajifunze zaidi na kutengeneza ile hali ya kuwajibika ndani yake,”amesema Suzy.
Ili kuendelea kujichotea faida hizi na nyingine nyingi ni vyema kujijengea utamaduni wa kutembelea ndugu, jamaa na marafiki mara kwa mara ili kuwajulia hali na kuimarisha mahusiano baina yenu.
Latest