Kamera tano bora za ulinzi majumbani, ofisini

June 30, 2022 9:27 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Zinahusisha matumizi makubwa ya teknolojia.
  • Licha ya bei kuwa juu zipo zenye unafuu.
  • Ni pamoja na Ring stick up, Google Nest na Wyze Cam V3.

Dar es salaam. Unahitaji kufunga kamera ya ulinzi nyumbani au ofisini kwako ili kurekodi na kufuatilia kinachoendelea kwa ajili ya usalama wako na wanaokuzunguka? Huenda unajiuliza ni kamera gani inafaa.

Jarida la ZDnet ambalo huandika habari za teknolojia kutoka nchini Marekani  wametoa orodha ya kamera za ulinzi kwa  kuzingatia ubora wa kamera, sifa za ulinzi za kamera hiyo, urahisi wa matumizi pamoja na bei ya kamera husika. 


1.Ring stick up 

Hii ni kamera inayofanya kazi kwa kutumia mionzi ya jua (umemejua), kamera hii ina njia mbili za kusafirisha sauti. Hurekodi picha jongefu kwa ubora wa hali ya juu wa pikseli 1080 ambayo huleta picha yenye muonekano angavu. 

Kamera hii inaweza kutumika maeneo ya nje na ndani na inaweza kuunganishwa na vifaa vingine vya kielektroniki kama vile simu na kompyuta mpakato na kukuwezesha kufuatilia kinachorekodiwa ukiwa popote pale. 

Kamera hii inaweza kuwekwa pia kwenye maeneo ya jangwa au msituni hata kama hakuna chanzo cha umeme kwani huja na paneli ya sola yenye betri pamoja na betri ya ziada.

Ikiwa utaamua kutumia kamera hii basi jiandae kusubiri kwa muda mrefu kwa sababu hutengenezwa kwa oda maalum na usafirishaji wake unaweza kuchukua muda.

Kamera moja inapatikana kwa Dola za Marekani 149 sawa na Sh347,617.

Kamera husaidia kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali ya nyumbani na ofisini. Picha| Suleman Mwiru.

2.Google Nest 

Kamera nyingine inayotajwa kuwa ni bora ni hii kutoka kampuni ya Google. Inakupa machaguo matatu ya rangi na imeunganishwa na programu saidizi za sauti kutoka Google pamoja na Amazon Alexa huku ikiwa na uwezo wa kurekodi picha jongevu katika nyuzi 135.

Kamera hii inafaa zaidi kwa matumizi ya ndani kuliko nje hasa kwa wale ambao wanatumia mifumo ya nest. Katika ulinzi wa majengo inaweza kutumika ndani na nje na uangavu wa picha zake ni pikseli 1080. 

Ubora wa picha hizo siyo mchana tu bali hata usiku na watengenezaji wanakupa machaguo mawili yaani  inayotumia waya kunganisha kwenye umeme na inayotumia batri za kuchaji.

Zote zinaweza kuunganishwa na vifaa vingine vya kielekitroniki na kukuletea taarifa punde tu zinaporekodi jambo la kutia mashaka. 

Kama zilivyo bidhaa nyingine kutoka kampuni ya Google basi ukitaka kununua kamera hiyo mfuko uwe umenona. Gharama yake kwa kamera moja ni Dola za Marekani 100 sawa na Sh233,300.


Zinazohusiana: 


3.Wyze Cam V3

Kama unataka kuingia kwenye ulimwengu wa intaneti ndio kila kitu pamoja na teknolojia ya hali ya juu ya vifaa vya ulinzi wa majumbani fikiria kuhusu kamera ya Wyze V3, miongoni mwa bidhaa inayopatikana kwa unafuu.

Kamera hii ina uwezo wa kutambua sauti pamoja na mijongeo lakini pia imewekewa uwezo wa kuhifadhi matukio yenye ukubwa wa gigabaiti 32 bila kusahau uwezo wa kurekodi matukio nyakati za usiku. 

Uangavu wa picha zake ni pikseli 1080. Teknolojia iliyotumika kutengeneza kamera hii unaiwezesha kufanya kazi kwa ubora ule ule hata wakati wa mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo mvua, tetemeko la ardhi bila kuathirika. 

Inafaa kwa matumizi ya ndani na nje, ina njia mbili za sauti, na ina uwezo wa kurekodi kwa ubora na inapatikana kwa bei nafuu zaidi katika orodha hii ambapo inauzwa kwa Dola za Marekani 36 sawa na Sh83,988.

Kamera hii  inaweza kutumika kwa matumizi tofauti tofauti kutokana na udogo wake pamoja na unafuu wake. Changamoto yake ni ukomo wa kuhifadhi vitu kwani gigabaiti 32 zikishajaa haitaweza tena kuendelea kuhifadhi matukio mengine. 


4.Arlo Pro 4

Hii ni kamera bora zaidi katika maeneo ya kazi. Inaweza kukuza picha kwa ukaribu zaidi mara 12 ( 12x zoom), kutumika maeneo ya ndani na nje, kumudu hali zote za hewa pamoja na uwezo wa kutambua sauti na picha jongevu.

Zinapatikana katika rangi nyeupe au nyeusi. Inaweza kufanya kazi mchana na usiku unaweza kuiweka dukani, nje ya jengo au hata kwenye kiwanda. Imeunganishwa pia na programu saidizi ya Google pamoja na Alexa bila kusahau Apple. 

Watumiaji wanaweza kupokea taarifa punde tu pale inapotambua mjongeo au sauti. Uangavu wa picha zake ni wa juu zaidi ukifikia pikseli 2000 na huwa na betri inayodumu  kwa muda wa  miezi sita na itakulazimu kutoa Dola za Marekani 180 sawa na Sh419,940 kwa kamera moja.


Tangazo


5.Simplisafe 

Hii inafaa zaidi kwenye nyumba za kupanga, inaweza kurekodi matukio kwenye nyuzi 120 na umbali wa futi 1000. 

Kamera hizi zinaweza kuunganishwa na intaneti pamoja na vifaa vingine vya kielektroniki ili kukupatia mwenendo halisi wa matukio yanayorekodiwa, kamera nyingi za mtindo huu hutumia umeme japo zipo zinazotumia betri. 

Baadhi ya kamera za muundo huu huwa na vihisi moshi au maji pamoja na kengele ambayo hutoa mlio ili kutoa taarifa pale inaporekodi jambo la kutilia mashaka. 

Pamoja ya kuwa ina mvuto lakini utaipata kuanzia Dola za Marekani 270 ili kupata seti moja ya kamera hizi sawa na Sh629,910 za kitanzania. 

Nini cha kuzingatia unapotaka kununua kamera za ulinzi?

Mahitaji ya kamera za ulinzi yanatofautiana. Mahitaji ya nyumbani hayawezi kuwa sawa na ofisini au maeneo ya shughuli za kibiashara japo zote huwa na lengo moja. 

Mambo ya kuzingatia ni namna gani kamera hiyo itafungwa na bajeti yake kuanzia ununuzi mpaka ufungaji na maeneo ambayo unapenda ifungwe.

Wewe utachukua kamera ipi kati ya hizo hapo juu? 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW