Masomo ya sayansi yalivyowatoa jasho watahiniwa wa kidato cha pili 2023
- Asilimia 7 ya watahiniwa somo la Fizikia wafaulu huku asilimia 80 wakifeli.
- Wachambuzi wa elimu waeleza uhaba wa walimu ni miongoni mwa sababu.
Dar es Salaam. Huenda Serikali pamoja na wadau wa elimu wakatakiwa kuchochea zaidi juhudi za kuongeza ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati nchini kutokana na kuendelea kuwa miongoni mwa masomo yenye ufaulu wa chini zaidi katika matokeo ya mitihani.
Matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta) Dk. Said Mohamed jana Januari 7, 2024 yanaoyesha kuwa masomo ya Sayansi na Hisabati ndiyo yenye ufaulu wa chini zaidi kuliko masomo mengine.
“Masomo ya Physics, Chemistry, Agriculture na Basic Mathematics yana ufaulu ulio chini ya wastani ambao ni kati ya asilimia 19.06 hadi 39.24,” amesema Dkt.Mohamed.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, somo la Fizikia ndilo liliongoza kwa kuwa na ufaulu wa chini wa asilimia 7.2 huku asilimia 80.9 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo mwezi Oktoba na Novemba 2023 wakifeli.
Soma zaidi:Tizama hapa matokeo ya kidato cha pili, darasa la nne 2023
Somo la Kemia limepata ufaulu wa asilimia 28.1 ulioshuka kwa asilimia 5.8 kutoka asilimia 33.4 ya watahiniwa waliofaulu mwaka 2022.
Wakati ufaulu ukishuka, asilimia 71.8 sawa na wanafunzi 493,285 waliofanya mtihani huo wamefeli somo la Kemia katika matokeo ya mwaka 2023 ikiongezeka kutoka asilimia 66.5 ya wanafunzi waliofeli somo hilo mwaka 2022.
Idadi hiyo ni sawa na kusema wanafunzi saba kati ya 10 waliofanya mtihani wa Taifa wa kidato cha pili wamefeli somo la Kemia.
Kwa somo la Hisabati ambalo limekuwa likiwatoa jasho watahiniwa wa mitihani ya Taifa, mwaka huu limepata ufaulu wa asilimia 21 ukiongezeka kiduchu kutoka asilimia 16.5 iliyorekodiwa mwaka 2022.
Aidha, waliofeli katika somo hilo wamepungua kidogo kwa asilimia 4.5 kutoka asilimia 83.4 iliyorekodiwa mwaka 2022 jambo linalotoa matumaini kiduchu kwa watahiniwa na wadau wa elimu katika somo hilo nchini.
Masomo mengine ya Sayansi ikiwemo Biolojia na Kilimo bado mambo ni magumu kwa kuwa licha ya ufaulu kuongezeka kiduchu bado wastani wake uko chini ya kiwango ikiashiria juhudi za dhati zinatakiwa ili kupandisha ufaulu wa masomo hayo muhimu.
Soma zaidi:Ufaulu waongezeka kiduchu matokeo kidato cha pili, darasa la nne 2023
Wachambuzi wa elimu waeleza sababu
Gerutu Gerutu mchambuzi wa elimu na Mhadhiri katika Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), ameiambia Nukta Habari kuwa chanzo cha wanafunzi wa sekondari kufeli mitihani ya Taifa ni kutokutengenezewa msingi tangu shule za msingi.
Gerutu amebanisha kuwa uhaba wa walimu wa sayansi katika shule za msingi husababisha baadhi ya wanafunzi kutoyapenda masomo hayo huku mazingira duni ya kufundishia yakichangiza zaidi hali hiyo.
“Serikali isipeleke walimu ila waweke mazingira wezeshi kwanza walimu wenyewe watake kwenda kufanya hicho kitu kwa sababu wanakipenda na mazingira ni mazuri…” amesema Gerutu.
Aidha, Gerutu amesisitiza kuwa ili kuongeza ufaulu wa masomo hayo ni vyema Serikali na wadau wa elimu wakaanzisha programu ambazo zitabadilisha mtazamo wa wanafunzi wanaoona masomo ya sayansi kama fani ngumu au ya watu wachache.