‘Shetani’ na wenzake wapandishwa kizimbani
- Wafikishwa mahakamani ikiwa zimepita siku nne tangu wakamatwe
- Kesi yahairishwa mpaka Februari Mosi, 2024.
Mwanza. Watu watano akiwemo Mtingwa Kilimanjaro maarufu kama Shetani (42), wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wakituhumiwa kufanya mauaji ya watu wawili.
Watuhumiwa hao wamepandishwa kizimbani ikiwa zimepita siku nne tu tangu Jeshi la Polisi litangaze kuwatia nguvuni Januari 15 mwaka huu kwa makosa ya mauaji, kughushi nyaraka na kusafirisha dawa kulevya.
Mwendesha mashtaka wa Polisi Martha Chacha, aliyekuwa akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Tumsifu Barnabas, leo Januari 19, 2024 amesema washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Oktoba 12, 2023 huko Lwenge wilayani Sengerema.
Soma zaidi:Tamaduni zinavyodumaza vipaji wa wasichana mkoani Mwanza
Matha ameiambia Mahakama kuwa washtakiwa hao walimuua Sophia Maduka (61) na mumewe Mathias Lusesa (73), wote wakazi wa Lwenge wilayani humo kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Mbali na ‘Shetani’ washtakiwa wengine waliopandishwa kizimbani kwa kosa hilo ni pamoja na Majaliwa Damasi (18), Mkazi wa Masumbwe, Emmanuel Damasi (34), Mkazi wa Bulungwa, Selina Mchele (49) na Maneno Mashauri (19) wote wakazi wa Lwenge mkoani Mwanza.
Baadhi ya watuhumiwa wa mauaji wakirudishwa rumande baada ya kusomewa mashtaka katika Mhakama ya Wilaya ya Sengerema.Picha.|Mariam.
Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote baada ya kusomewa mashtaka hayo na kurejeshwa rumande kutokana na Mahakama hiyo kukosa mamlaka kisheria ya kusikiliza shauri hilo.
Kutokana na jambo hilo, Hakimu Barnabas ameahirisha kesi hiyo hadi Februari Mosi, 2024 itakapotajwa tena.
Kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao kunatoa taswira chanya ya kumalizika kwa vitendo vya uhalifu mkoani Mwanza jambo litakaloongeza ulinzi wa raia na mali zao mkoani humo.