Saba waripotiwa kuugua kipindupindu Mwanza
- 18 wawekwa chini ya uangalizi maalumu.
- Wananchi wakumbushwa kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kuosha mikono.
Mwanza. Watu saba wameripotiwa kuugua ugonjwa wa Kipindupindu huku wengine 18 wakichunguzwa afya zao baada ya kuishi na watu wenye ugonjwa huo kwenye maeneo mbalimbali Jijini Mwanza.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Dk. Sebastian Pima aliyekuwa akizungumza kwenye kikao cha kamati ya afya ya msingi jijini humo amesema mgonjwa wa kwanza alibainika Januari 4, 2024 baada ya kupokea mgeni kutoka Bariadi mkoani Simiyu.
“Watu hao walikuja Mwanza kuchukua mzigo Kwa ajili ya biashara, baadae walianza kujisikia vibaya wakaenda hospitali na baada ya vipimo walibainika kuwa na ugonjwa huo,” amesema Dk. Pima.
Dk. Pima amebainisha kuwa walifanya ufuatiliaji kwenye maeneo mengine kujua iwapo kuna wagonjwa wengine ambapo walibaini visa vingine kutoka eneo la Mkolani ambapo vilibainika visa viwili na vitatu vimetokea Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
“Hadi sasa tangu Januari 4 mwaka huu tulipopata mlipuko wa kipindupindu tumeshapata wagonjwa saba ambao wamelazwa kwenye kituo chetu cha matibabu,” ameongeza Dk. Pima.
Soma zaidi : Ugonjwa wa kipindupindu waripotiwa Kagera, wanne wafariki
Aidha, Dk. Pima amebainisha kuwa wamefanya ufuatiliaji kwa familia waliokutana na wagonjwa kwa watu 18 ambao mpaka sasa hawajaonesha dalili za ugonjwa huo ingawa wanaendelea na uchunguzi zaidi kwa kuwa wagonjwa hao wamekutana na watu wengi.
Hii si mara ya kwanza ugonjwa wa kipindupindu kuripotiwa nchini Tanzania, hususan Kanda ya Ziwa, Disemba 4 2023, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwasa alitangaza watu wanne kufariki kuutokana na ugonjwa huo huku wengine 18 wakichukuliwa sampuli kwa vipimo zaidi.
Chanzo, tahadhari vyatolewa
Akizungumzia chanzo cha ugonjwa huo, Dk Pima amesema unaambukizwa kwa kula chakula, kinywaji au kitu chochote chenye vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu na mara nyingi unakuwa na mchanganyiko wa kinyesi chenye vimelea.
Dk. Pima Ameitaka jamii kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni wakati wote baada ya kujisaidia, pamoja na kula chakula cha moto.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Thomas ameagiza uwepo wa wataalamu katika maeneo ya shule, taasisi na masoko kuwe na wataalamu wataotoa elimu kuhusu ugonjwa huo.
Latest
