Maisha mapya baada ya ahueni ya Teleza Kigoma
- Wakazi wa kata ya Mwanga Kusini wanasema wana zaidi ya miezi sita hawajasikia visa hivyo.
- Serikali na asasi za kiraia zatoa msaada wa kisaikolojia kwa waathirika.
Kigoma. Usiku mmoja mwaka 2018 akiwa amelala, Christina Rashid, alishtuka na kujikuta amekaribiwa na mwanaume aliyekuwa uchi na kujipaka oili chafu ndani ya chumba alichokuwa amepanga katika mtaa wa Simu ndani ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Mwanaume huyo asiyefahamika, aliingia ndani mwake licha ya kuwa wakati wa kulala Christina alikuwa amefunga mlango na madirisha.
“Baada ya yule Teleza kuingia, nilishtuka na kuhamaki, sikupiga kelele alivyoona hivyo alikimbia bila kunifanya chochote,” anasema Christina.
Teleza, kwa mujibu wa viongozi na wakazi wa kata ya Mwanga Kusini, walikuwa ni wahalifu wanaojipaka mafuta mwilini au oili chafu wakiwa uchi na kuingia kwenye nyumba za akina mama wajane, wasioolewa au ambao waume zao wamesafiri kisha kuwabaka, kuwaibia mali au kuwajeruhi pale wanapojitetea na ukatili huo.
Umaarufu wa jina hilo ulikuja kwa kuwa baada ya kufanya uhalifu huo, ilikuwa ni vigumu kwa wanawake waliofanyiwa ukatili kumshika kutokana na mwili wake kuteleza kiasi cha kumruhusu akimbie bila kukamatwa akiwa mtupu.
Maumivu ya Teleza
Christina (23) anayekaa kata ya Mwanga Kusini kilomita chache kutoka katikati mwa manispaa hiyo anasema baada ya mwezi mmoja Teleza alirejea kwenye nyumba yake tena.
Hata hivyo, ni ngumu kwa Christina kufahamu iwapo aliyekuja awamu ya pili katika chumba chake alikuwa yule yule wa awali ama mpya.
“Alikuja mara ya pili tena usiku nikiwa nimelala, siku hiyo nilikuwa nimetoka kazini. Baada ya purukushani alifanikiwa kuniibia Sh55,500,” anasema binti huyo anayekaa pekee yake.
Binti huyo angalau ana ahueni ya kuibiwa, wapo wanawake ambao walibakwa ama kuumizwa na mapanga na Teleza kiasi cha kuwaachia maumivu ya mwili na kisaikolojia.
Teleza ni moja ya matatizo sugu yaliyokuwepo tangu mwishoni mwa mwaka 2016 katika kata ya Mwanga Kusini kiasi cha kufanya wanawake wajane na wanaoishi peke yao kukosa raha kila ulipokuwa ukiingia usiku.
Baadhi ya wakazi wa kata hii wameiambia Nukta Habari (www.nukta.tz.co) kuwa baada ya kuingia katika nyumba, Teleza walikuwa wakiwaonya wanawake wasiseme kwa kuwa wangewarudia jambo lililofanya baadhi ya wanawake wasiripoti matukio hayo ya ukatili.
Hadi sasa kuna zaidi ya wanawake 58 ambao wameunda kikundi cha kupeana msaada wa kimawazo na kisaikolojia baada ya kufanyiwa vitendo hivyo, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kikundi cha waathirika wa vitendo hivyo, Ramla Hamisi.
Huenda idadi hiyo ikawa kubwa zaidi ya waliothirika kwa kuwa baadhi walikuwa hawaripoti kwa vyombo vya dola.
Wakati naingia kwa Ramla wanawake 10 wengine walikuwa wakifanya kikao cha kikundi chao cha waathirika wa Teleza ikiwemo kupeana msaada wa kimawazo.
Hata hivyo, kwa sasa vitendo hivyo vimetoweka na sehemu kubwa ya wakazi wa kata hii ya Mwanga Kusini wanasema hawajasikia vitendo hivyo tangu mwaka jana huku wengine wakisema angalau kwa miezi sita sasa.
Teleza ilivyoangamizwa
Mtendaji wa Mtaa wa Mwanga Kusini, Joachim Hore anasema mara ya mwisho kuripotiwa kesi za Teleza ilikuwa ni kati ya mwaka 2019 na mwanzoni mwa mwaka 2020 baada ya watu wawili kuripoti kuwa walikuwa wameingiliwa na wahalifu hao.
“Kwa sasa hali ni shwari baada ya kuundwa ulinzi shirikishi. Tulipata elimu ya ulinzi shirikishi kutoka polisi makao makuu ambao walikuja kutoa semina,” anasema.
Ili kuhakikisha akina mama wanakuwa salama, Serikali na baadhi ya asasi za kiraia zikiwemo Voice of Change na Tamasha zilikuwa zinawaelimisha wanawake namna ya kujilinda na Teleza.
Kwa wengi waliokuwa wanasikia habari za Teleza kwenye vyombo vya habari huenda wasiamini habari hizi lakini mmoja ya walinzi shirikishi katika kata ya Mwanga Kusini, Joseph Amon (28) anasema wahalifu hao walikuwepo lakini kwa sasa hawajasikia kesi mpya kwa muda mrefu.
“Kuna siku tulimshika Teleza mmoja mtaa wa Rusimbi usiku…alivamia nyumba wakati watu bado hawajalala, tulianza kumshughulikia bahati nzuri mwenyekiti wa mtaa alipiga simu polisi na kumuokoa,” anasema Amon ambaye amekuwa akishiriki doria kwa zaidi ya mwaka sasa.
“Mambo sasa ni shwari na ni mazuri sana…mara ya mwisho kusikia habari za matukio ya Teleza ni muda sasa, sijasikia tena. Tunachopata taarifa sana kwa sasa ni wizi kwa kutumia bodaboda na vibaka wanaoiba mali za watu usiku.”
Mtendaji wa Kata ya Mwanga Kusini Mariam Abdi anasema “Teleza ilishaisha” na kwamba tangu aingie madarakani Machi mwaka huu hajapata kesi yeyote licha ya kuwa kuna wakati kulikuwa na matukio yaliyodaiwa ni teleza lakini baada ya uchunguzi ilibainika siyo.
Wanaharakati na waraghabishi waliochangia katika kupaza na kuripoti matukio hayo wanaona kuna ahueni kubwa kwa akina mama wa manispaa hiyo.
‘Sasa hali ni shwari’
“Hali ya sasa inaridhisha sana japo siwezi kusema kuwa tatizo limeisha kabisa kwa sababu huenda vitendo hivyo vinaendelea lakini watu wanaogopa kusema kuhatarisha maisha yao,” anaeleza Sinaraha Andrea (30) maarufu kama mpambanaji na kuwa tangu uanze mwaka 2021 hajasikia matukio ya Teleza.
Uongozi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji unaeleza kuwa siku za nyuma kulikuwepo na uhalifu wa Teleza ambao ulijenga hofu kwa wakazi wa Mwanga Kusini.
“Baada ya kupata taarifa hizo kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Manispaa tulihimiza ulinzi shirikishi jamii na jambo hilo tulilitokomeza,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Frednand Filimbi.
Mara ya mwisho kupokea taarifa zinazohusiana na masuala ya teleza, anasema, ni zaidi ya miezi sita iliyopita.
“Polisi hawatoshi kumlinda kila mtu hivyo ulinzi shirikishi kila mtaa ilikuwa ni suluhu,” anaeleza.
Serikali yatoa msaada wa kisaikolojia
Kwa sasa, Filimbi anasema maofisa wa ustawi wa jamii wanaendelea kuwapatia msaada wa kisaikolojia waathirika wa ukatili huo ili waendelee na maisha ya kawaida.
Kupungua kwa vitendo hivyo angalau kunawapa wanawake na wasichana katika manispaa hiyo uhuru wa kulala kwa amani japo wapo baadhi hawaamini kuwa Teleza imetoweka kabisa.
“Kama binti ilikuwa inaniogopesha sana,” anasema Nasra Sudan (21), mkazi wa kata hiyo ya Mwanga Kusini.
Kwa Nasra na baadhi ya waathirika wenzie wa vitendo hivyo taarifa za hivi miezi mitatu iliyopita kuwa kuna matukio matatu yalitokea yakihusishwa na Teleza bado yanawapa hofu licha ya kukiri kuwa “kwa zaidi ya silimia 80” teleza wamepungua.
‘There is no teleza’ (Hakuna Teleza)
“There is no teleza (hakuna teleza) ni masuala ya miaka ya zamani wengine tulikuwa hatujafika hapa. Hakuna “anymore” (hakuna tena), hakuna tena aliyeripoti,” anasema Alchelaus Mutalemwa, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma.
Kuhusu matukio mapya ya uhalifu ambayo baadhi wana hofu huenda ni teleza, Mutalemwa anasema polisi hawajapata taarifa hizo.
“Mtu anapata tatizo anaenda kwenye NGO (asasi ya kiraia) ile siyo sehemu yake,” anasema huku akizituhumu baadhi ya asasi za kiraia kuwa zinawalipa baadhi ya watu wadai bado kuna teleza na kwamba wanaendelea kuzichunguza.
Hata hivyo, Mutalemwa anasema wanaendelea kutoa elimu kuhusu ulinzi shirikishi ikiwemo namna bora ya ukamataji wahalifu na ufanyaji doria na wametoa namba za viongozi wote wa polisi kuripoti matukio yeyote ya uhalifu.
Latest
