Karanga: Kinara mazao mbegu za mafuta Tanzania
- Zao hilo liliongoza kwa kuvuna mwaka 2019/20
- Zao la mafuta lililolimwa Zanzibar ni karanga pekee.
- Wakulima watakiwa kuongeza uzalishaji kupata soko.
Dar es Salaam. Kilimo kinatajwa kuwa uti wa mgongo wa taifa huku sekta hiyo ikitajwa kuajiri maelfu ya Watanzania.
Katika kilimo hicho, wapo waliojikita kwenye kilimo cha mazao ya chakula na ya biashara zikiwemo mbegu  mbalimbali za mafuta kama alizeti, ufuta na karanga.
Ripoti ya Sensa ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2019/20 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza kuwa mbegu za mafuta zilizolimwa nchini mwaka huo ni pamoja na alizeti, ufuta, karanga na michikichi.
Nani kipenzi cha Wakulima?
Kati ya mazao hayo manne, zao la mafuta lililolimwa zaidi ni karanga ambapo jumla ya hekari 484,730 zilivunwa kwa kipindi hicho cha kilimo.
Kwa upande wa uzalishaji, tani 621,697 za karanga zimezalishwa kwa mwaka huo na kufanya zao hilo kuwa lililozalishwa zaidi ikilinganishwa na mengine.
Idadi hiyo ni jumla ya mavuno ya Tanzania bara na Zanzibar.
Karanga ni zao pekee la mbegu za mafuta lililolimwa Tanzania bara na Zanzibar. Picha| Global.
Hata hivyo, karanga ndiyo zao pekee linalolimwa Tanzania bara na visiwani ambapo Tanzania ilipata mavuno ya asilimia 99.8 ya mavuno huku zanzibar ikivuna hekari 1,017 kati ya mavuno ya nchi nzima.
Zao la mbegu za mafuta linalofuata kwa kuvunwa zaidi ni mbegu za mafuta ya alizeti ambazo kwa mwaka 2019/20, tani 503,032 zilizalishwa na mavuno yakaishia tani 495,377.
Alizeti imevunwa zaidi kwenye kipindi cha mvua za msimu mfupi ambapo asilimia 97.2 ya mavuno yalitokana na msimu huo. Kwenye kipindi cha mvua za msimu mrefu, ni hekari 13,736 za alizeti ndiyo zilivunwa.
Takwimu hizi ni za Tanzania bara pekee.
Mbegu za ufuta pia hazikubaki nyuma kwenye kilimo cha mbegu za mafuta. Jumla ya hekari 392,481 za zao la ufuta zilivunwa nchini zikifuatiwa na zao la michikichi ambalo hekari 7,067 zilivunwa zao hilo.
Kwa mujibu wa NBS, mwaka 2019/20, hekari 1.3 milioni za Tanzania zilivuna mazao ya mbegu za mafuta.
Unangoja nini kuwekeza katika kilimo cha mbegu za mafuta ili kujipatia soko na kupunguza mafuta ambayo Tanzania inaagiza nje ya nchi?
Latest