Mambo yatakayosaidia kukuza uchumi jumuishi Tanzania
- Ni kuanzisha vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
- Utengaji wa maeneo ya kufanyia biashara na mikopo.
- Ushirikishwaji wa sekta binafsi nao utasaidia.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili dhana ya uchumi jumuishi iweze kutekelezeka kivitendo nchini Tanzania, Serikali na taasisi binafsi zishirikiane kuanzisha vituo vya mafunzo ya uchumi huo na kutenga maeneo maalum kwa wafanyabiashara wadogo.
Amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ni kuiwezesha nchi kuwa na uchumi jumuishi ili kuwezesha makundi yote kwenye jamii kufaidika na ukuaji wa uchumi.
“Anzisheni vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, ambavyo vitatoa huduma za mikopo, mafunzo, urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za masoko na kutoa ithibati ya bidhaa zinazozalishwa,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Viwanda na Baishara, Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na taasisi za elimu za umma na binafsi zitoe mafunzo na ujuzi kwa Watanzania kulingana na mahitaji ya soko la kitaifa na kimataifa.
Amesema mafunzo hayo yatawawezesha wananchi kuzalisha bidhaa bora na kutoa huduma zenye viwango zinazoweza kuhimili ushindani ndani na nje ya nchi.
Ameziagiza halmashauri zote ziweke mazingira wezeshi na ziendelee kutenga maeneo maalumu yatakayowawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kukua, kustawi na kufanya shughuli za kiuchumi.
“Halmashauri zote nchini zihakikishe afua za uwezeshaji wananchi zinatengewa bajeti na kuwajengea uwezo maafisa biashara ili waweze kuratibu kwa ufanisi masuala ya uwezeshaji katika halmashauri zao,” amesema Majaliwa leo Oktoba 4, 2021 katika kongamano la tano la uwezeshaji wananchi kiuchumi, jijini Dodoma.
Mmoja wa vijana wanaotengeneza majiko banifu mkoani Iringa ambayo hupunguza matumizi ya mkaa. Picha| Daniel Samson.
Aidha, amesema viongozi wa mikoa wasimamie uimarishwaji wa majukwaa ya wanawake kwenye mikoa kama ilivyoelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan alipokutana na wanawake jijini Dodoma Juni 8, 2021.
“Taasisi za umma na binafsi zinazosimamia mifuko na programu za uwezeshaji zinazotoa mitaji na ruzuku zihakikishe kuwa zinaweka watumishi kwenye vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili uwepo wa vituo hivyo uwe na maana kwa wananchi wanaokwenda kupata huduma na ziimarishe huduma ili kuwezesha ustawi na kukua kwa uchumi wa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni kwa lengo la kupunguza umaskini na kuchochea shughuli za kiuchumi,” amesema.
Serikali imeweka vipaumbele vitakavyowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ikiwemo uimarishaji wa huduma za afya, hifadhi ya jamii, maji, umeme na utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila ada
Amesema uwezeshaji wa uchumi jumuishi ni msingi wa kuhakikisha kunakuwa na ustawi endelevu kwa watu wote, ambapo Serikali imeandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 ambayo pamoja na mambo mengine imeainisha mazingira wezeshi yatakayowezesha nchi kunufaika kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, kuna vituo 17 vya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mikoa sita ya Geita, Shinyanga, Singida, Rukwa, Dodoma na Kigoma.
Katika kipindi cha mwaka mmoja vimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh24 bilioni 24 kwa wafanyabiashara 3,233 na mafunzo ya ujuzi na biashara kwa watu 1,990.
Latest
