Jinsi ya kukabiliana na fikra za kujiona duni
- Fahamu kuwa vigezo vya uzuri na urembo vimewekwa na wanadamu.
- Jifunze kujikubali na kujinenea mazuri.
- Kama kuna kitu kinakunyima raha, tafuta wa kuzungumza naye.
Dar es Salaam. Kuanzia umbo la mwili, rangi ya ngozi, michirizi, chunusi, nywele na mambo mengine mengi yanayoambatana na jinsi mtu alivyo, kwa mtu binafsi yanaweza kuonekana ni mapungufu.
Wapo watu ambao wanalazimika kuvaa mawigi kila siku kwa sababu wanaona ni warembo zaidi wakiwa hivyo huku wengine wakilazimika kuvaa kofia kila waendapo kwa kuhisi wanaficha visivyopendeza kuonekana kwa watu. Hayo kwao, ni mapungufu ya miili yao.
Hali hiyo kwa baadhi inawafikisha katika hatua ya kufikiri hawajatimia kwa kujilinganisha na wengine. Wanatamani ngozi zao zingelikuwa nyeupe zaidi, pua zichongoke na midomo iwe minene kiasi.
Muulize rafiki yako, utashangaa akikueleza kitu anachofikiri kuwa ni mapungufu au kinampatia kile kwa kimombo kinaitwa “insecurity”.
Hata hivyo, mambo yote hayo yanayohisiwa kuwa ni insecurities, ni utofauti tu kati ya binadamu mmoja na mwingine na kama yanakutesa, huenda dondoo hizi zikakusaidia kuona kuwa thamani yako haipimwi na kile unachofikiri hakijatimia kwenye mwili wako.
Kwa lolote unalohisi ni mapungufu, fahamu kuwa ni upekee wako. Picha| Shutterstock.
Vigezo vya ubora vimewekwa na binadamu
Hivyo vigezo vya urembo na ubora unavyohisi hauna, ni mambo ambayo yamechorwa na jamii. Kigezo cha kuwa ngozi yako siyo nzuri, umbo lako siyo zuri au kitu ulichonacho hakitoshi ni mambo ambayo jamii imeyaweka kwenye uso wa dunia.
Mraghabishi wa masuala ya afya ya uzazi, Lilian Mwakyosi amesema zamani alikuwa anaona rangi ya ngozi yake siyo inayoweza kuhusishwa na urembo. Kukua katika jamii ambayo ilipendekeza ngozi nyeupe ndiyo kipimo cha urembo ilikuwa ni ngumu kwake mwenye ngozi nyeusi.
“Nilikuwa nikijihisi siyo mrembo mbele ya wasichana weupe lakini nilikuja kujua kuwa yote hiyo ni mitazamo tu. Nilijikubali na nashukuru siku hizi hata vyombo vya habari vinalipigia swala hilo kelele,” amesema Mwakyosi.
Mtaalamu huyo wa masuala ya urembo anashauri kufunguka pale mtu anapokunenea mabaya, kujiamini na kufanyia kazi mtazamo wako juu yako.
“Vile watu wanakuona siyo muhimu. Muhimu zaidi ni vile wewe kama wewe unavyojiona,” amesema Mwakyosi.
Zingatia furaha yako
Kinachokufanya ujione mdhaifu kwa kujilinganisha na wengine ni kimoja lakini yapo mengi zaidi yanayokupa nguvu ambayo unaweza kujivunia na Mungu amekujalia.
Mwanamuziki Zipporah Zealot, awali alihisi mwili wake kuwa ndiyo udhaifu wake. Tangu akiwa mdogo alikuwa akijihisi ana upungufu mbele ya wasichana wembamba kwa kuwa yeye ana umbo kubwa.
“Ujue kuna mahala unaweza shindwa kusimama kwa kuwa unaona wenzio wote wana miili midogo wewe ukaona ukae tu. Lakini saizi ah! Nimejikubali na najiona ni wa pekee,” amesema Zealot.
Kwa mwanadada huyo aliamua kujifua zaidi kimuziki na mengine ambayo yanampatia nguvu kuliko mwili wake.
“Nimefocus (nimejielekeza) kwenye muziki wangu na mengine ambayo yananijengea kujiamini. Hilo moja linaloninyima raha nimetupa kule,” amesema Zealot.
Fahamu kuwa uumbaji wa Mungu umekamilika na haujakosewa. Picha| CNN.
Kama linarekebishika, lifanyie kazi
Yapo mengine ambayo unaweza kubadili kwa jitihada zako binafsi. Ni kuamua tu kama kweli kwako yana umuhimu.
Mjasiriamali Jessica Mshama alikuwa hana amani na muondoko wake kwani ulimfanya kuharibu viatu na kukosa amani pale anapotembea mbele ya umma.
Hata hivyo, kukabiliana na hali hiyo ilimlazimu kufanyia kazi jinsi anavyotembea kwenye viatu vyake na kwa sasa ana amani kabisa na anaweza kukatiza popote akiwa amevalia kiatu chochote.
“Niliamua kujijali na kujifanyia kazi mimi mwenyewe kwani nililokuwa naona ni kama tatizo linaweza kubadilishika,” amesema Mshama.
Mwanadada huyo ameshauri watu kuridhika na uumbaji wa Mungu kwani kila mtu ana kitu chake cha pekee.
Weka mipango ya kuyakataa mapungufu hayo kama inawezekana
Kwa wanaume, huenda yapo mapungufu mengi yanayozunguka kwenye vichwa vyao. Kuanzia mitazamo ya jamii juu ya jinsia hiyo na vile unatakiwa kuonekana.
Kwa Mkazi wa Mbeya, Eli Elisante, kushindwa kumsaidia mpenzi wake kwenye mahusiano ni jambo ambalo litamnyima raha. Mara nyingi inamlazimu hadi kukopa fedha kwa rafiki zake ili tu atimize haja ya ampendaye.
“Hapa nimetoka kuombwa iPhone X juzi na alikuja kwangu kuniomba baada ya kuibiwa simu yake ya zamani. Hapa navyokwambia nina deni la 200,000 maana sikuweza kusema neno “sina”,” anasema Elisante.
Kutatua changamoto hiyo, Elisante anatakiwa kujifunza kueleza hisia zake pale anapokuwa hawezi kutimiza jambo fulani bila hofuya kuumiz hisia za wengine.
Kwa lolote unalohisi ukijiweka kwenye mzani halitimii, fahamu kuwa kila mtu ana utofauti wake na kilicho na maana zaidi ni mtazamo wako juu yako, kama Lilian alivyosema.
Wewe ni mzuri, unatosha, unaweza kufanya au kuwa chochote.
Latest