Majaliwa atoa maagizo mazito fedha za IMF mikoani
- Wakuu wa mikoa watakiwa kuzingatia uwajibikalji na uwazi.
- Hatapewa posho kusimamia matumizi ya fedha hizo.
- Ataka miradi iliyobuniwa itekelekezwe ndani ya miezi tisa.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakuu wa mikoa yote nchini wanapaswa kusimamia kwa karibu ya Sh1.3 trilioni zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuhakikisha zinatumika kama zilivyopangwa.
Tanzania ilipata kiasi hicho kama mkopo ambao unapaswa kutumika kwa miezi tisa ili kukabiliana na athari za ugonjwa wa Corona (Uviko-19) katika sekta mbalimbali.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Oktoba 21, 2021ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma wakati alipokutana na mawaziri na makatibu Wakuu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia miradi ya fedha za kuimarisha huduma za jamii za IMF.
Majaliwa ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, amesema Kamati za Ulinzi za Mikoa (KUU) zitakuwa na jukumu la kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo na kama kutakuwa na suala la rushwa wataingia na kuchukua hatua.
“Katika kipindi cha miezi tisa, tunatakiwa tuwe tumekamilisha hii miradi,” amesisitiza.
Amesema timu hiyo ndiyo itawajibika kwenda maeneo ya vijijini kuona kama kazi inafanyika kwa viwango vinavyotakiwa kwani kuna baadhi ya miradi utekelezaji wake unapaswa uwe umekamilika ndani ya miezi mitatu.
“Mkoa utaamua ni mfumo gani utumike kusimamia utekelezaji miradi kwenye wilaya zake. Waheshimiwa Mawaziri lazima mwende kukagua miradi hii kulingana na sekta zenu na mkifika mkoani ni lazima muambatane na afisa mhusika kutoka mkoani,” amesema.
Amesema makatibu wakuu wa wizara pia wanapaswa kwenda kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo lakini kwa kupeana zamu na mawaziri wao.
“Hii ndiyo kamati inayosimamia hizi fedha, kwa hiyo tunatakiwa tusimamie miradi yote ya kisekta ili ikamilike ndani ya miezi tisa kama ilivyopangwa. Mheshimiwa Rais ameshasema, sisi kazi yetu ni kuhakikisha kwamba inakamilika. Tusipokwenda hakuna ambaye atawajibika,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema watendaji wa vijiji na kata nao wana wajibu wa kusimamia miradi hiyo huko huko waliko na kusisitiza kuwa wahandisi wahakikishe viwango vya majengo vinaendana na fedha zilizotolewa.
Aidha, ameagiza mafundi wanaoajiriwa wapewe mikataba ili wasikimbie kazi.
Kuhusu manunuzi ya vifaa vitakavyotumika katika miradi hiyo, Waziri Mkuu amewataka wahakikishe wanatumia vitabu maalum vya kumbukumbu (ledger).
“Kwenye miradi hii, wakinunua vifaa kuwe na daftari la makabidhiano baina ya mnunuzi na Kamati ya Usimamizi. Vifaa vikishanunuliwa ni lazima vikabidhiwe kwa kamati,” amesisitiza.
Kuhusu posho, Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa amesema “hakuna mtu anayepaswa kudai posho katika hii kazi. Tukifanya hivyo, hii miradi haitakamilika. Hata sisi hapa kwenye Kamati hii, Mheshimiwa Rais hajatoa posho, sana sana ametuongezea majukumu.”
Mapema, akiwasilisha mchanganuo wa Dh1.3 trilioni 1zilitolewa na IMF, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema fedha hizo zimetolewa kulingana na sekta.
Sekta hizo ni maji, afya, elimu, utalii, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hifadhi ya jamii ambako kuna Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ( TASAF), vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ya Kitaifa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Wenye Ulemavu; Waziri wa Fedha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia; Waziri wa Maji, Waziri wa Maliasili na Utalii; Waziri wa Viwanda na Biashara;pamoja na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.
Latest
