Bodaboda 400 hufariki dunia kila mwaka kwa ajali za barabarani Tanzania
- Aagiza elimu itolewe zaidi kwa bodaboda.
- Awataka wananchi kufuata sheria.
- Askari watakiwa kuwa rafiki kwa wananchi.
Mwanza. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema zaidi ya vijana 400 wanaoendesha bodaboda hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwemo ulevi, mwendekasi na kutova kofia ngumu.
Vijana wengine 800 hujeruhiwa kwenye ajali hizo na kuepeleka kukazwa kwenye hospital mbalimbali nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani iliyofanyika leo Novemba 23, Rais Samia amewataka askari kikosi cha usalama barabarani kuelekea nguvu kubwa kwenye kundi hilo la waendesha bodaboda ili kujipatia elimu ya kujikinga na ajali.
Rais Samia pia amesisitiza nidhamu za utumiaji wa barabara ili kujikinga na ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu ambazo ni zaidi ya asilimia 90.
“Bado waendesha bodaboda ndiyo chanzo cha ajali hizi, niombe wakati baraza la usalama barabarani likiwa linatoa elimu libaki na kundi hili kwa kuwa ndiyo waathirika wakubwa, bado hawazingatii sheria, hawavai kofia ngumu na uendeshaji usiozingatia sheria, ” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amewataka wananchi kuhakikisha wanafuata sheria bila shurutu na kuwa mlinzi kwa mwenzake ili kuweza kudhibiti ajali.
Aidha, Rais Samia ameelekeza Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na makundi mbalimbali kupitia vipindi vya radio, television lakini pia midahalo na iwe ajenda za kitaifa.
Ameagiza kufanya utafiti wa kimfumo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa usalama barabarani na vyuo ili kuja na mipango ya kupunguza ajali hizo huku polisi wakitakiwa kuwa msaada na rafiki kwa wananchi.
“Na hapa naomba nisistize zipo tabia za baadhi ya askari wa usalama barabarani kushikilia leseni za madereva, madereva kulazimishwa kulipa deni alilokamatwa nalo papo hapo, pamoja na ukamataji wa vyombo vyao kwa muda mrefu, suala hili liangaliwe upya ili kupunguza hizo kero ndogo ndogo,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa na wakazi waliohudhuria uzinduzi wa wiki hiyo leo Novemba 23, 2021 jijini Arusha.
Rais Samia Suluhu Hassan, ashiriki katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha leo Novemba 23, 2021. Picha| Ikulu.
Mengine hapana…
Akijibu maombi ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kuhusu tozo zinazotozwa kwa wanaobanika kuwa na makosa zitumiwe kuboresha baraza hilo, Rais Samia amesema hataruhusu hilo litokee kwa kuwa ndiyo litakuwa chanzo cha mapato.
Amesema ni kweli kwamba baraza hilo kwa muda mrefu halina bajeti lakini hawataruhusu fedha za tozo zinazotokana na makosa kuwa sehemu ya bajeti yao.
“Hili la kukosa bajeti nimeliona na nimelisikia lakini sitaruhusu nusu ya tozo zitumike kwa kuwa mtaacha kazi yenu ya kupiga faini ili kudhibiti ajali badala yake itakuwa chanzo cha mapato,” amesema.
Rais Samia amesema Serikali itahakikisha inalipatia baraza hilo vifaa vya kisasa vya ukaguzi zitakavyosaidia katika mapambano ya ajali lakini pia vitasaidia katika kuuza stika na hivyo kuongeza pato la Taifa.
Awali Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mtafungwa aliomba Serikali kuliwezesha baraza hilo kupatia vifaa vya kisasa vya kukagua magari mabovu ambayo yamekuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani.
Mtafungwa ameiomba pia Serikali kufunga kamera maalum za barabarani (CCTV) zitakazosaidia kudhibiti na kuongeza uwazi na kurahisisha ufuatiliaji wa kesi za makosa ya barabarani.
Kamera hizo pia kwa mujibu wa katibu mtendaji huyo zitapunguza wingi wa askari wa kikosi cha usalama barabarani na kusaidia katika ufuatiliaji wa ajali zinapotokea huku akiomba kamera hizo pia zifungwe katika barabara kuu za mikoa.
Latest
