Mfahamu mfua vyuma tegemeo la wachimbaji wadogo wa dhahabu Dodoma
- Ni Kennedy Iyasi katika mgodi wa dhahabu wa Chikoa.
- Amekuwa kiungo muhimu kwa wachimbaji wadogo mkoani humo.
- Anaingiza Sh50,000 hadi Sh200,000 kwa siku.
Dodoma. Wakati wa kuingia katika eneo hilo huwezi kukosa kumuona akiwa katika kibanda kidogo kilichoezekwa kwa miti, majani pamoja mifuko ya plastiki.Katika hali ya utulivu huku akitumia nyundo kuponda vyuma vilivyo juu ya chuma kingine chenye umbo la pembe nne, kijana huyu bila shaka ni mfua vyuma.
Vyuma hivyo vimetolewa muda si mrefu kwenye moto wa mkaa uliopo mita moja na eneo alipo tayari kwa kuvichonga ili viwe na makali ya kuweza kutoboa ardhi yenye mawe.
Huyo siyo mwingine bali ni Kennedy Iyasi, mfua vyuma katika mgodi wa dhahabu wa Chikoa uliopo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Iyasi ndiye mtu pekee anayetegemewa na wachimbaji wadogo kujipatia vyuma vya ukubwa tofauti kwa ajili ya kutumia kuchimba madini ya dhahabu ndani ya miduara iliyopo mgodi hapo.
“Mgodi huu ulipofunguliwa mwezi Machi mwaka huu, mimi niliona fursa nikajenga kakibanda haka na kuanza kufua vyuma ili nipate hela ya kula,” anasema Iyasi huku akiendelea kuponda chuma.
Pembeni yake, yuko mwenzake, Paul Lameck ambaye amekaa chini huku akizungusha gurudumu la chuma la baiskeli lililoegeshwa juu ya vyuma viwili na kuunganishwa na mpira ambao nao umeelekea kwenye mashine ndogo ya kuzalisha upepo.
Mashine hiyo ya bati ndani yake ina mota inayotumika kuzalisha upepo ambao hukoleza moto wa mkaa kupasha na kulainisha vyuma mbalimbali.
“Tuko hapa tunasogeza siku kwa kutengeneza hivi vyuma tupate pesa ya kutunza familia,” anasema Lameck anayezungusha gurudumu hilo ambalo ndiyo chanzo kikuu cha kuufanya moto uwake wakati wote.
Kennedy Iyasi akiponda chuma kilichotolewa kwenye moto ili kukipa makali. Picha| Daniel Samson.
Namna wanavyafua vyuma
Iyasi ambaye ni mkazi wa jijini hapa anasema mashine hiyo inayopata nguvu kwa kuzungusha gurudumu la baiskeli ina mapango boi yanayozalisha upepo unaokoleza moto ili kukilainisha chuma kabla hakijachongwa.
“Ndiyo maana hapa tuko wawili, mmoja anazungusha hili tairi kuhakikisha mkaa unaendelea kuwaka wakati wote chuma kikiwa ndani ya mkaa,” anasema Iyasi kuwa chuma kinakaa kwenye moto kwa dakika 10 ndiyo kinakuwa kimelainika.
Iyasi ambaye ana uzoefu wa kufua vyuma kwa zaidi ya miaka mitano anasema vyuma hivyo viko katika maumbo tofauti kulingana na mahitaji ya wateja wake ambapo vingine viko kama sururu ambayo inaunganishwa na mti.
“Gurudumu hili linazalisha upepo wa kuunda chuma (ponchi) ya kuchimbia miduarani,” anasema Iyasi.
Shughuli hiyo pia huusisha kufanyia marekebisho ponchi za wachimbaji ambazo zimeisha makali ili kuziongezea ufanisi wa kuchimba miamba.
Hata hivyo, teknolojia anayotumia Iyasi na mwenzake inawalazimu kutumia nguvu nyingi na muda kuyeyusha na kuvichonga vyuma, jambo linalowafanya wachoke sana huku tija ikiwa ndogo.
Anasema wakati mwingine mahitaji yanakuwa ya juu mgodini hapo kwa sababu wachimbaji wanakuwa wengi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, sekta ya wachimbaji wadogo inatoa ajira za moja kwa moja kwa takriban watu milioni 1.2 na ajira zisizo za moja kwa moja kwa watu milioni 7.2 sawa na asilimia 90 ya nguvu kazi katika sekta ya madini nchini.
Wachimbaji hao ambao hufanya shughuli zote za uchimbaji madini ikiwemo uchorangaji wa miamba na uchenjuaji wa dhahabu hufanyika katika maeneo 300 nchini hasa katika mikoa ya kanda ya Ziwa ikiwemo Geita na Mara.
Mmoja wa wachimbaji katika mgodi huo, Meshack Nathaniel anasema mfua vyuma huyo amekuwa akiwasaidia kupata vyuma vyenye uwezo mkubwa wa kuchimba miamba ili kujipatia dhahabu.
“Hapa yuko peke yake, asipokuwepo inakuwa changamoto kazi zinasimama…,” anasema Nathaniel.
Mmoja wa wafanyakazi wa Iyasi akizungusha gurudumu la baiskeli ili kuzalisha umeme kwa ajili ya kukoleza moto unaolainisha vyuma vya kuchimbia madini. Picha| Daniel Samson.
Shughuli hiyo inalipa?
Kwa mujibu wa mfua vyuma huyo, kazi hiyo inamlipa kwa kiasi chake ikizingatiwa kuwa hakosi pesa ya kutunza familia na kusomesha watoto.
“Hapa nipo peke yangu, wachimbaji hawapungui 20 hapa. Kila wiki lazima nifanye kazi ya kufua vyuma,” anasema.
Bei ya ponchi hizo hutofautiana kulingana na umbo, ukubwa na uwezo wake katika uchimbaji, ambapo ponchi moja inauzwa kati ya Sh10,000 hadi Sh30,000.
“Kwa siku unaweza kupata Sh50,000 kama mgodi umechangamka lakini kama umefua vyuma vingi unaweza kupata Sh200,000 kwa siku,” anasema Iyasi kuwa fedha hiyo haipati kila siku kwa sababu ziko siku ambazo anaambulia patupu.
TANGAZO
Jiunge nasi kwa kiunganishi hiki https://t.me/nuktahabari

Matarajio aliyonayo
Iyasi bado ana ndoto kubwa ya kukuza biashara yake. Maono yake ni kuwa na vifaa vya kisasa vya kufua vyuma na eneo zuri ikizingatiwa kwa sasa anaendesha shughuli zake kwenye kibanda ambacho mvua ikinyesha hawezi kufua vyuma.
Anaangazia siku zijazo atumie mashine inayotumia nguvu ya gesi ili kutengeneza vyuma vingi kwa wakati mmoja kwa sababu mgodi huo unakua kila siku hivyo ana uhakika wa kupata wateja wengi.
“Kama ningekuwa na moto wa gesi ningetengeneza zaidi,” anasema Iyasi.
Kijana huyo ni miongoni mwa vijana wengi wabunifu katika sekta ya madini Tanzania ambao wamekuwa wakitumia ubunifu wa kujiajiri na kutoa suluhu ya changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.
Hata hivyo, wanahitaji kusaidiwa hasa kupata mitaji na teknolojia za kisasa kufanikisha shughuli zao.
Mtaalam wa mazingira kutoka Tume ya Madini Tanzania, Mhandisi Abel Madala anasema wanafanya kazi kwa karibu na wachimbaji wadogo wa madini ili kuboresha maeneo yao ya kufanyia kazi kwa sababu wana mchango mkubwa katika upatikanaji wa mapato ya Serikali.
Sera ya Madini ya mwaka 2009 imeagiza kuwatambua na kuwasaidia wachimbaji wadogo na kuhamasisha uchimbaji endelevu wa madini ili kuongeza tija na mchango wa sekta ya wachimbaji wadogo katika uchumi na pato la Taifa.