Kitaeleweka: Wafanyabiashara wasubiri soko jipya kwa miaka mitatu Dar

December 23, 2021 2:25 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni soko la Kigilagila lililopo Kiwalani lililoanza kujengwa mwaka 2019.
  • Wafanyabiashara wachoshwa na soko la muda.
  • Serikali yaahidi kukamilisha ujenzi kwa wakati.

Dar es Salaam.  Alitarajia baada ya miezi minne tu ujenzi wa soko ungekamilika ili apate eneo zuri la kufanyia biashara lakini mambo yamekuwa tofauti na matarajio yake.

Soko hilo la Kigilagila lililopo Kiwalani jijini Dar es Salaam lililovunjwa na kuanza kujengwa upya tangu mwaka 2019, ujenzi wake haujakamilika mpaka sasa.

Mfanyabiashara Neema Charles na wenzake 58 waliokuwa wakiuza bidhaa katika soko la zamani walihamishiwa soko la muda lilipo umbali wa kilomita moja ili kupisha ujenzi.

Hata hivyo, Neema anakaribia kukataa tamaa ya kurudi katika soko jipya kwa sababu hafahamu ni lini ujenzi utakamilika.

“Tumekaa muda mrefu mazingira siyo rafiki. Hayafurahishi. Kama hivi unaona mifereji inapita humu humu, tuliambiwa tutapisha ujenzi kwa muda wa miezi minne lakini hadi leo ni miaka mitatu,” anasema Neema.

Neema ambaye pia ni Mwenyekiti wa soko hilo anasema soko la muda walilohamishiwa halina miundombinu rafiki ikiwemo mitalo ya kupitisha maji, barabara, jambo linalohatarisha afya zao na wateja wanaokwenda kununua bidhaa.

“Kwa miaka mitatu tumeathirika kwa kweli. Kutokana na mazingira mabovu, huwezi kumwaga mzigo vizuri na vizimba vyenyewe hapa tumejijengea wenyewe, hivyo vinavuja,” anaeleza mwanamke huyo huku akionyesha baadhi ya vibanda vya miti walivyojenga.

Wafanyabiashara wakifanya shughuli zao katika soko la muda wakati wakisubiri soko jipya la Kigilagila lililopo Kiwalani jijini Dar es Salaam. Picha | Gift Mijoe.

Wafanyabiashara hao wanalalamika kuwa soko la muda liko mbali na makazi ya watu, jambo linalofanya mauzo ya bidhaa kushuka na wakati mwingine mazao kuharibika kwa kukaa muda mrefu bila kupata wateja.

“Biashara hakuna hapa. Tunafanya tu tupate japo 200 ila lile lingine likikamilika itakua ahueni kwa upande wetu,” anasema Mary Elias, mfanyabiashara wa mbogamboga katika soko la Kigilagila.

Hali hiyo inawaathiri zaidi wafanyabiashara wanawake ambao wanategemea biashara ya sokoni ili kujikomboa kiuchumi na kuepukana na ukatili kijinsia ambao umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo yao. 

“Tulivyokua kwenye soko letu kule tulipopisha ujenzi, biashara ilikua inaenda kwa sababu tulizungukwa na makazi ya watu. Sasa hivi tumezungukwa na makaburi na barabara, biashara inakuwa ngumu kidogo,” anasema Mary.

                         

Soko jipya litakidhi matakwa ya wafanyabiashara?

Hadi Julai 2020, ujenzi wa soko hilo ulikuwa umekamilika hadi kuwekewa paa isipokuwa sehemu chache ambazo ujenzi ulikuwa unaendelea. 

Wakati ujenzi wa soko hilo jipya ukiendelea, baadhi ya wafanyabiashara wamesema hawaridhishwi na muonekano wa soko wakidai ujenzi haujakidhi mahitaji yao kama wafanyabiashara. 

“Ujenzi wa eneo tunalotarajia kurudi sasa hivi lina changamoto nyingi kwa wafanyabiashara wote, tumeshawasilisha malalamiko kwa viongozi tofauti tofauti ikiwemo mkuu wa masoko, wahandisi na mtendaji kata kuangalia changamoto hizi,” anasema Jumbe.

Jumbe ambaye pia ni mfanyabiashara wa samaki katika soko hilo, anasema kwa upande wao wafanyabiashara ya samaki soko jipya halijakidhi mahitaji yao kwa sababu maeneo la kukaangia samaki na kuuzia yako tofauti.

Pia wanadai kuwa miundombinu ya soko hilo haitaruhusu matumizi ya kuni na mkaa, hivyo huenda gharama za kutumia gesi zikaongezeka kwa sababu awali hawakufikiria kutumia nishati hiyo.

Mwonekano wa soko jipya la Kigilagila lililopo Kiwalani jijini Dar es Salaam ambalo ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2019. Soko hilo bado linajengwa. Picha | Gift Mijoe.

“Japo changamoto hizi hazijapatiwa ufumbuzi, kuna mwelekeo ila hatujui utaishia wapi,” anasema Jumbe akiamini malalamiko yao yatasikilizwa.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wana matumaini kuwa soko hilo litawapa ahueni na kuwaongezea kipato kwa sababu watakuwa karibu na wateja wao.

“Huku tulipo hali ni ngumu, hakuna biashara. Tunategemea tutakaporudi tulipokua angalau tutapata wateja wawili watatu.” anasema Salma Ngoma, mama lishe sokoni hapo.

 Serikali imesema haiwezi kutoa tamko lolote juu ya soko hilo mpaka pale ujenzi utakapokamilika na wafanyabiashara kuruhusiwa kufanya biashara.

“Hatuwezi kuzungumzia chochote juu ya soko la Kigilagila kwa sasa mpaka soko litakapokamilika lote,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Tabu Shaibu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW