Ahueni: Wakulima kuanza kununua mbolea kwa bei waliyoizoea

January 1, 2022 7:03 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia asema utaratibu utaanza mapema mwaka 2022.
  • Wakulima walalamika bei ya mbolea kupanda.
  • Mikakati ya kujenga viwanda viwili vya mbolea yaendelea.

Dar es Salaam. Huenda wakulima wa Tanzania wakauanza mwaka 2022 kwa tabasamu baada ya Serikali kuwahakikishia kuwa wataanza kununua mbolea ya kukuzia mazao yao kwa bei waliyoizoea huku ikianisha mipango ya kujenga viwanda vya bidhaa hiyo nchini.

Wakulima kutoka maeneo mbalimbali wamekuwa wakilalamikia ongezeko la bei ya mbolea kuwa linahatarisha shughuli zao za uzalishaji mazao. 

Ongezeko la bei ya mbolea nchini limesababishwa na mabadiliko ya bei ya mbolea katika soko la dunia tangu mwezi Novemba 2020 hali ambayo imeathiri nchi nyingi ikiwemo Tanzania.

Mabadiliko hayo bei yamechangiwa zaidi na janga la Corona (Uviko-19) ambapo baadhi ya viwanda kwenye nchi wazalishaji wakubwa wa mbolea zilipunguza uzalishaji.

Inakadiriwa kuwa mbolea nchini imepanda kati ya asilimia 20 hadi 30.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan jana Desemba 31, 2021 wakati akilihutubia Taifa amesema bei ya mbolea itarejea kama kawaida mwanzoni mwaka 2022, jambo litakalowapunguzia wananchi machungu.

“Tunatambua changamoto ya upungufu wa mbolea ambayo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na kushuka bidhaa hiyo duniani kwa sababu ya Uviko-19. Lakini habari njema ni kwamba mapema mwakani 2022 tunatarajia kupata mbolea ya kukuzia mazao itayouzwa kwa bei ambayo wakulima wameizoea,” amesema Rais Samia.

Pamoja na jitihada hizo, amesema kampuni ya Intro Fertilizer inajenga kiwanda kikubwa cha mbolea jijini Dodoma ambacho kitazalisha tani 500,000 sawa na takriban asilimia 70 ya mahitaji yote kwa mwaka.

“Aidha, kampuni ya Dangote nayo imeonyesha nia ya kuanzisha kiwanda cha mbolea ya Urea kule Mtwara,” amesema Rais Samia kuwa jitihada hizo zote zitasaidia kupunguza upungufu wa mbolea nchini na kuwawezesha wananchi kufaidika na kilimo cha mazao.


Zinahusiana: 


Asilimia 90 ya mbolea inayotumika nchini huagizwa kutoka nje ya nchi huku asimilia inayobaki huzalishwa na viwanda vya ndani kikiwemo cha Minjingu cha mkoani Manyara.

Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) zinaonesha kuwa Upatikanaji wa mbolea msimu 2020/21 ulifikia tani 678,017 sawa na asilimia 94.4 ya mahitaji ya tani 718,051 kwa msimu wa 2020/21.

Suluhisho la muda mrefu

Jukwa la Wadau wa Kilimo Tanzania (ANSAF) linapendekeza kupatikana kwa suluhu ya kudumu ya mbolea kwa kushirikisha wadau zaidi (watunga sera, wafanyabiashara na Wakulima) katika kutengeneza mikakati yakuboresha upatikanaji mbolea kwa bei nafuu na kwa wakati.

“Kuvutia uwekezaji zaidi kwenye viwanda vya mbolea vya ndani na kuimarisha vilivyopo ili kuongeza uzalishaji na upatikanaji mbolea nchini,” limeeleza jukwaa hilo katika uchambuzi wake wa mbolea Tanzania uliotolewa hivi karibuni.

Pia kuwekeza kwenye upimaji wa udongo ili kujua mahitaji halisi ya virutubisho ili kushauri wawekezaji kwenye viwanda vya ndani na waagizaji.

Kufanya utafiti na kuhamasisha matumizi ya mbolea mbadala (mfanoNPS badala ya DAP nk) na kuimarisha masoko ili wakulima wapate soko la uhakika na bei nzuri kumudu gharama za pembejeo.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV