Aliyekamatwa kwa kumiliki kiwanda cha mawese aibua mjadala Tanzania

January 18, 2022 1:04 pm · Wilson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Halifa Issa mkazi wa Kibaha.
  • Anatuhumiwa za kuendesha kiwanda bubu cha kuchakata mafuta ya mawese.
  • Watumiaji wa mitandao ya kijamii watoa maoni tofauti, wengine wataka asaidiwe kupata vibali.

Dar es Salaam. Mjadala mpana umeibuka katika mitandao ya kijamii baada mkazi wa Kongowe Wilayani Kibaha, Halifa Issa kukamatwa kwa tuhuma za kuendesha kiwanda bubu cha kuchakata mafuta ya mawese, huku baadhi ya watu wakisema hatua hiyo inarudisha nyuma juhudi za vijana kujikwamua kimaisha kupitia sekta ya kilimo.

Mjadala huo ambao umepata nguvu tangu jana Januari 18, 2022 katika mtandao wa Twitter baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kumkamata Issa (42) kwa madai kuwa anamiliki kiwanda hicho bila ya kuwa na kibali na kinyume cha sheria.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Wankyo Nyigesa akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuwa wanamshikilia mtu mmoja aitwaye Halifa Issa dereva mwenye umri wa miaka( 42) kabila Muha mkazi wa Kongowe Wilayani Kibaha amekamatwa akiendesha Kiwanda Cha kuchakata afuta hayo ya Mawese bila ya kuwa na kibali.

RPC Wankyo alisema kuwa Issa alikamatwa Februari 16 mwaka huu majira ya saa saba mchana katika maeneo ya Ungindoni Kata ya Kongowe Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.

“Jeshi la Polisi likiwa katika majukumu yake ya kila siku walimtia mbaroni Halifa Issa mwenye umri wa (42) mfanyabiashara na mkazi wa Kongowe anaendesha Kiwanda Cha kuchakata mafuta ya Mawese pasipo na kibali chochote kutoka serikalinj upelelezi wa tuhuma dhidi ya muhusika umekamilika na atafikishwa mahakamani,”alisema RPC Wankyo.

Kufuatia kusambaa kwa taarifa za kukamatwa kwa Issa, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa na maoni tofauti huku baadhi wakisema kijana huyo alitakiwa kupewa elimu ya namna ya kubapa vibali vya kuendesha kiwanda chake kutoka kwa Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo Tanzania (SIDO) lakini siyo kumkamata.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema mamlaka zinapaswa kuwaonyesha njia za kupata vibali na siyo kuwakamata watu wanaofanya uwekezaji ili kujipatia kipato.

“Wananchi wanatafuta njia zao za kujipatia kipato. Bwana Halifa Issa anapaswa kusaidiwa kuonyeshwa njia za vibali na sio kukamatwa,” amesema Zitto katika ukurasa wake wa Twitter.

Wachangiaji wengine katika mjadala huo wamesema, ni vema elimu ikatolewa na siyo kutumia nguvu wakatio wote hasa kwa wajasiriamali wanaotatu changamoto za jamii.

“Yani badala ya kupeleka SIDO na TBS wamfanyie tasmini awezeshe, mnapeleka polisi arafu….. ameandika  el Profesor  katika mtandao. 

jimmy Lihende ametoa ushauri kuwa “Wanahitaji kujifunza namna ya kuwezesha hicho kiwanda ili kuendeleza uzalishaji…wakisajili na maisha yaendelee Halmashauri iweke hisa 50% na huyu mbunifu pia awe na hisa 30% walau…kunazo sababu za  ububu huo, tufanye utafiti pia.” 

“Mtu kama huyo si wa kumkamata bali apewe usajili na wataalamu. Huyo ni mtu muhimu aliyedhubutu,” amesema Bakari Seif.


Soma zaidi:


Hata hivyo, baadhi ya watu wamesema Jeshi la Polisi limetekeleza wajibu wake kwa sababu kuna utaratibu maalum wa kupata vibali kabla mtu hajaanza kufanya uzalishaji kwenye kiwanda.

Mtumiaji wa Twitter, Maguzu Maguzu (@NgoshaKugema) amesema “anatakiwa kufuata utaratibu: mamlaka ya chakula na dawa wajue, mkemia mkuu ajue anatumia chemical gani kuchakata mafuta yake! Kumbuka hili ni suala la afya ya jamii !acha kuwa emotional !tunaenda kwa utaratibu.”


Serikali yaingilia kati 

Kufuatia mjadala huo, Serikali imesema inalifuatilia suala hilo ili kupatikana kwa suluhu kwa sababu lengo ni kuwawezesha watu kuongeza thamani ya mazao ikiwemo mbegu za mafuta.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema tayari amewasiliana a Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri ili kumsaidia mjasiriamali huyo ili asajili kiwanda chake SIDO.

“Nashukuru kwa Taarifa hii nimewasiliana na Mh DC wa kibaha nimemuomba amtafute huyu mwananchi na kumsaidia kupitia SIDO  na wizara ya Kilimo tuna promote “Value addition” through backyard processing (tunakuza “Ongezeko la Thamani” kupitia usindikaji) hana tofauti na wale wa alizeti wanaouza barabarani ni jukumu letu kuwasaidia,” amesema Bashe wakati akichangia mjadala huo.

Uzalishaji wa mafuta ya mawese Tanzania

Serikali imelipa kipaumbele zao la michikichi kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, hivyo ufufuaji zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya ndani na ziada itakayobakia itauzwa nje ya nchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  mwaka 2020 aliwataka wananchi hasa vijana kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa upo uhakika wa kupata mbegu bora na pia zao hilo litawakwamua kiuchumi na kuwaondolea umasikini wa kipato.

Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zenye mazingira mazuri ya uzalishaji wa michikichiki lakini inakadiriwa kuwa inaagiza tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese na hutumia takriban Sh600 bilioni kila mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi ili kufidia pengo la uhaba wa mafuta.

Licha ya changamoto za uzalishaji wa zao hilo ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, mbegu bora na soko, uzalishaji wa mawese umekuwa ukiongezeka kila mwaka jambo linalotoa matumaini kwa Serikali na wadau wa zao hilo kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji.

Hali ya hewa ya Tanzania inaruhusu michikichi kustawi kwa wingi hasa katika mikoa ya Kigoma, Mbeya (Wilaya ya Kyela) na Pwani ambayo ina hali ya kitropiki hasa joto la wastani na mvua za kutosha.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW