Rais Samia aingilia kati sakata la polisi kudaiwa kuua mfanyabiashara Mtwara

February 4, 2022 1:42 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ashari saba wanatuhumiwa kumuua mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis.
  • Rais Samia asema Jeshi la Polisi haliwezi kujichunguza lenyewe.
  • Aagiza kuundwa kamati huru kuchunguza tuhuma hizo.

Dar es Salaam. Sakata la askari polisi saba ambao wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis limechukua sura mpya baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda kamati huru kuchunguza tuhuma za mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mtwara ACP Mark Njera,  Mahembe askari ha wanatuhumiwa kutekeleza mauaji ya Hamisi (25), mkazi wa kijiji cha Ruponda Wilaya ya Nachingwea mkoani humo na kisha kumpora Sh70 milioni.

Watuhumiwa hao saba waliofikishwa Mahakamani Januari 25, 2022 ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara,  Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara,  Charles Onyango na Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Nicholaus Kisinza. 

Wengine ni Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Msuya Mganga, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salimu Juma Mbalu.

Imeelezwa kuwa tukio la mauaji ya kijana huyo walilitekeleza Januari 5, 2022 na mwili wa marehemu waliutupa katika kitongoji cha Majengo, Kijiji cha Hiari wilayani Mtwara.

Sakata hilo limezidi kuchukua sura mpya baada ya Rais Samia kuingilia kati na kusema kwa mazingira ya tuhuma zilivyo, Jeshi la Polisi haliwezi likajichunguza lenyewe kwa sababu waliohusika na ni askari wake.

“Kuna mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizopo, Jeshi ndilo lililofanya mauaji. Kwa maana hiyo, taarifa niliyonayo ni kwamba, Jeshi limetengeneza kamati ya kufanya uchunguzi alafu walete taarifa, haiwezekani Jeshi lifanye mauaji, Jeshi lijichunguze lenyewe,” amesema Rais.

Kutona na utata huo, Rais Samia amemuagiza Majaliwa kuunza kuunda kamati huru kuchunguza tuhuma hizo huku akilitaka jeshi hilo kujitafakari kwa mambo ya mauaji yanayoendelea nchini.

“Nimemuelekeza Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), aunde kamati nyingine iende ikafanye uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi alafu watuletee taarifaa, lakini wakati huo huo, nataka Jeshi lako lijitafakari waone kama kinachotokea ni misingi ya jeshi la polisi.

“Kwa hiyo tutasubiri taarifa ya kamati huru itakayoundwa na Waziri Mkuu ituletee taarifa tulinganishe na ile ya Jeshi la Polisi tuone taarifa mbili zinasemaje tuchukue hatua mwafaka,” amesema Rais leo Februari 4, 2022 wakati akiwa wilayani Magu akielekea Katika Mkoa wa Mara katika sherehe za maadhimisho ya miaka 45 ya CCM.


Soma Zaidi:


Maswali zaidi

Sakata hilo limezua mjadala kwa sababu mmoja wa watuhumiwa hao, Grayson Mahembe alidaiwa kujinyonga akiwa katika mahabusu ya polisi Mtwara.

Inadaiwa Mahembe alijinyonga Januari 22 mwaka huu kwa kutumia tambala la kudekia akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Mtwara.

Baada ya kifo cha Mahembe kumekuwa na mjadala mpana hasa katika mitandao ya kijamii kuhusu mazingira ya kifo chake huku wengine wakihoji inawezekanaje mtu akajinyonga kwa tambala la kudekia.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi zaidi na kusisitiza kuwa askari huyo alijinyonga na siyo vinginevyo. 

“Picha hizo zinaonesha dalili zote za mtu aliyejinyonga. Mwili ulifanyiwa uchunguzi pia (postmoterm) na daktari wa kuweza kuthibitisha kama kifo kilitokana na kujinyonga au ni sababu zingine,” alisema Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime akieleza mazingira ya kujiua kwa askari huyo Januari 31, 2022.

Mwili wa Mahembe ulizikwa Januari 25 mwaka huu mkoani Iringa, huku wazazi wake wakilitaka Jeshi la Polisi kuchunguza kifo chake hicho chenye utata.

                            

Watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali wamejitokeza kwa nyakati tofauti na kutaka Taifa litafakari mfululizo wa mauaji ya watu huku Jeshi la Polisi likitakiwa kijitafakari kuhusu wajibu wake wa kulinda raia na mali zake.


Haina kusubiri

Saa chache baada ya Rais Samia kutoa agizo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa ameunda timu maalum ya watu tisa ambayo imepewa jukumu la kuchunguza tuhuma za mauaji zinazowakabili askari saba wa Mtwara na mauaji yaliyofanyika Kilindi mkoani Tanga yaliyotokea Januari 30, mwaka huu.

“Kamati hiyo inapaswa kuanza kazi yake kesho na inatakiwa iwe imekamilisha ripoti yake ndani ya siku 14,” amesema Waziri Mkuu. 

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kamati hiyo ina maafisa wenye dhamana kutoka mamlaka tofauti za Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais,  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Mwanansheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro awasimamishe kazi maafisa wa Polisi wa Mtwara na Kilindi ili kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.

Kuhusu sakata la Kilindi, watu watano akiwemo mtoto waliuawa baada ya kufuatia mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Elerai kilichopo wilayani humo.

Wakielezea chanzo cha mapigano hayo mashuhuda wa tukio hilo wamesema ni mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wakulima na wafugaji wa vijiji hivyo ambao vuguvugu zake zilianza muda mrefu bila kupata ufumbuzi wa kudumu, ambapo Januari 30 ndio ikatoa tukio la mapigano kati ya pande hizo mbili.

“Viongozi hawa wanapaswa wakae pembeni, watahojiwa na hii timu wakiwa nje ya ofisi,” amesema Waziri Mkuu na kuwataja maafisa hao kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara (RPC), Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mtwara (RCO) na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara cha eneo alilofia mfanyabiashara Mussa Hamisi Hamisi na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Mahenbe anayedaiwa kujinyonga.

Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kilindi na Afisa Upelelezi wa Wilaya nao pia wakae pembeni kupisha uchunguzi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW