Muhimbili kuwachukulia hatua waliosambaza video ya Professor Jay
- Ni video inayomuonyesha msanii huyo akiwa ICU.
- Imesema haijahusika na usambazaji wa maudhui hayo.
- Yalaani tukio la kusambazwa video hiyo, kuchukua hatua kwa wahusia.
Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imelaani kitendo cha kusambazwa kwa video za msanii wa bongo fleva na mwanasiasa Joseph Haule maarufu kama Professor Jay huku ikisema itafuatilia kwa undani tukio hilo lisilo la utu kwa mgonjwa.
Professor Jay aliyelazwa katika hospitali hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja, video zake zilianza kusambazwa tangu jana mtandaoni zikimuonyesha akiwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU).
Baada ya video hiyo kusambaa, kumekuwa na maoni tofauti ya watu kuhusu suala hilo huku baadhi ya watu hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wakisema ni ukiukaji wa haki za mgonjwa hasa ya faragha.
Hata hivyo, wengine wamedai, Professor Jay ni mtu maarufu hasa katika tasnia ya muziki, hivyo watu kufahamu maendeleo ya afya yake ni muhimu.
MNH katika taarifa yake iliyotolewa leo Machi 10, 2021 imesikitishwa na imelaani kitendo cha mtu kurekodi video ya mgonjwa anayepigania uhai wake katika chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) na kuisambaza kinyume na taratibu za hospitali hiyo.
“Tunatoa pole kwa mke wa ProfJay, familia na jamii nzima iliyoguswa na tukio hili,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha.
Soma zaidi
- Kinachowakwamisha wanamuziki wa kike Tanzania kutamba kimataifa
- “Injili kwa flash”: Biashara haramu inayohujumu mapato ya wasanii, Serikali Tanzania
- Maumivu, kicheko kwa wasanii mabadiliko chati za muziki Youtube
MNH pia imekana madai ya baadhi ya watu ambao wanadai kuwa huenda video hiyo ilichukuliwa na wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa sababu siyo rahisi kwa mtu asiyehusika kuingia katika chumba cha ICU.
“Uongozi wa hospitali, unapenda kuutaarifu umma kwamba video hii haijarekodiwa na kusambazwa na hospitali. Tunahudumia wagonjwa takribani 3,400 kwa siku wakiwemo wananchi wa kawaida, viongozi wakuu wa Serikali, wanasiasa na watu wengine kwa kuzingatia taaluma, maadili, utu na faragha,” imesomeka taarifa hiyo.
MNH imesema inafuatilia kwa karibu tukio hilo ikiwemo kuwasiliana na mamlaka husika ili kubaini chanzo cha video hiyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Aidha, amewaomba wananchi na watumiaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) kuendelea kuwa na imani na hospitali hiyo pamoja na kuheshimu taratibu za hospitali.
Professor Jay ni miongoni mwa mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva ambaye amekuwa akiwavutia vijana wengi kuingia katika tasnia ya muziki huo.
Nguli huyo wa muziki aliyetamba zaidi na wimbo wa “Zali la Mentali” pia ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na alikuwa Mbunge wa jimbo la Mikumi kati ya mwaka 2015 na 2020.
— Muhimbili National Hospital (@MuhimbiliTaifa) March 10, 2022
Baada ya Jay kulazwa hospitali, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itagharamia matibabu yake mpaka atakapopona.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Februari 11, 2022 akiwasilisha salamu za Rais Samia baada ya kufika hospitalini hapo kumjulia hali msanii huyo.
“Nimefika kuleta salamu za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yupo safarini nje ya nchi, amesema kuwa anatambua mchango wa Profesa Jay akiwa Mbunge wa Mikumi lakini pia kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia muziki” alinukuliwa Waziri Ummy na vyombo vya habari.
“Hivyo kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu yake hadi hapo ataporuhusiwa kutoka hospitalini na ninauagiza uongozi wa Hospitali kuleta bili zote Wizarani kuanzia sasa”, amesema Waziri Ummy.