Sababu za Uber kusitisha huduma zake Tanzania
- Yadai nauli mpya imeifanya ishindwe kutoa huduma kwa wateja wake.
- Yaahidi kurudi mazingira yakiwa rafiki.
Dar es Salaam. Baada ya kutoa huduma kwa takriban miaka sita nchini Tanzania, kampuni ya usafiri wa mjini kwa njia ya mtandao ya Uber imesitisha huduma zake rasmi leo kwa kile ilichodai mazingira magumu ya kuendesha biashara yaliyosababisha ishindwe kuendelea kutoa huduma kwa wateja wake.
Uber na kampuni nyingine ikiwemo Bolt imekuwa mkombozi wa ajira kwa madereva na abiria ambao wamekuwa wakipata usafiri wa taxi, bajaj na pikipiki katika majiji makubwa ikiwemo Dar es Salaam kwa bei rahisi.
Kampuni hizo hutumia teknolojia ya programu ya simu na kompyuta kuwaunganisha wateja na madereva na gharama zake zote za usafiri hukokotolewa na programu husika.
Uongozi wa Uber ambayo iliingia rasmi Tanzania mwaka 2016 imefikia uamuzi huo iliouita “mgumu” leo Aprili 14, 2022 ambapo imesitisha huduma zake nchini kwa sababu ya mabadiliko ya hivi karibuni ya nauli ambayo imesema “inakua ngumu kwetu kuendelea kutoa huduma.”
“Nauli elekezi iliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesababisha changamoto kubwa kwa mifumo kama Uber kuendelea kutoa huduma kwa wateja wetu,” imesema taarifa ya Uber Tanzania iliyotolewa jana.
Kwa mujibu wa LATRA, bei za usafiri huo zimeongezeka kutoka Sh450 kwa kilomita moja hadi Sh900 ili kuwawezesha madereva kuendesha shughuli zao kwa faida.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari Machi 15 mwaka alisema pia wameelekeza kampuni zinazotoa huduma za usafiri kwa njia ya mtandao kutoza asilimia 15 ya faida inayopatikana katika kila safari na siyo zaidi.
Zinazohusiana
- Uber yatoa masharti mapya kwa madereva wake
- Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify
- Idris alamba shavu Uber
Baada ya mabadiliko hayo, Uber ambayo inafanya kazi katika nchi 72 na miji 10,500 duniani imesema haiwezi kuendelea tena kutoa huduma na itarejea tena ikiwa mazingira ya biashara yataruhusu.
“Hatutaweza kutoa huduma mpaka pale mazingira yatakapokua rafiki kwa sisi kuendelea kutoa huduma,” imesema taarifa ya Uber huku akibainisha kuwa iko tayari kushirikiana na mamlaka husika katika kuunda kanuni ambazo zitawezesha teknolojia kunawiri, ili waanze tena kutoa huduma.
Kampuni hiyo imesisitiza kuwa siku zote, lengo lao ni kuwa mshirika muhimu katika miji mbalimbali kwa kutoa usafiri wenye ufanisi, kutengeneza fursa za kiuchumi zinazowapa madereva uhuru wa kujiingizia kipato kwa muda wanaotaka wao na kuchangia katika mapato ya Serikali.
Jana, madereva waliandamana hadi ofisi za LATRA jijini Dar es Salaam wakishinikiza viwango vipya vya nauli vianze kutumika kwa sababu bei ya mafuta imepanda ili kuwapatia ahueni ya maumivu wanayopata sasa.
Huenda, kusitishwa huduma za Uber kunaweza kuwa kicheko kwa mshindani wake Bolt kupata faida zaidi katika soko ambalo ushindani unaweza kuwa umepungua.
Hata hivyo, baadhi ya watu wamesema hilo siyo la kufurahisha kwa sababu vijana watakosa ajira.
Mtumiaji wa Twitter Lembrus Mchome amesema “Uber kusitisha huduma zake hapa Tanzania ni pigo kubwa sana kwa vijana wengi ambao walijiajiri kupitia huduma hii, wapo waliokopa ili wajiajiri najiuliza kuhusu marejesho yao.”
Watumiaji wa wengine wa mitandao ya kijamii wameshauri Serikali kukaa pamoja na wadau wa usafirishaji kuangalia namna ya kutatua changamoto zilizopo ili kuimarisha shughuli za usafiri nchini.
Latest
