Wanawake katika mapambano dhidi ya Fistula Tanzania
- Baadhi wanachelewa kugundua huo, wanatengwa na jamii.
- Matibabu ya ugonjwa huo yaimarika, idadi ya wagonjwa ikipungua.
- Jamii yatakiwa kuwasaidia wanawake na kuimarisha mapambano dhidi ya Fistula.
Mwanza, Dar es Salaam. Kuzaa katika umri mdogo, ndiyo sababu iliyomfanya mama huyu wa watoto watano kupata ugonjwa wa Fistula.
Neema Mchele (30), mkazi wa Kijiji cha Buzigasoga Wilayani sengerema aliugua ugonjwa huo baada ya kubeba mimba yake ya kwanza akiwa kidato cha pili.
Licha ya kuhudhuria mahudhurio yote manne ya kliniki, lakini alipata shida siku ya kujifungua hali iliyosababisha kupata ugonjwa huo baada ya kuchanika vibaya.
Miezi mitano baadaye aligundua kuwa mwili wake hauko sawa hasa baada ya kuwa anatokwa na uchafu wa haja kubwa na ndogo wote ukipitia sehemu moja ya haja ndogo.
Pamoja na tatizo hilo bado hakutambua kama ni Fistula na aliendelea kuzaa watoto wengine wanne.
“Hadi baadaye nikiwa kiliniki mtu mmoja ambaye ni balozi wa Fistula alikuwa anatoa elimu kuhusiana na ugonjwa huo, ndipo nikagundua hali ninayopitia inachangiwa na tatizo hili na nikachukua hatua za kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu,” anasema Neema.
Neema anakiri kuwa kwa sasa hali yake ni nzuri baada ya kupata matibabu mkoani Mwanza.
“Kabla ya kutibiwa nilikuwa nimetengwa, ndugu walinikataa waliamini kuwa nimerogwa, sikuweza kushiriki shughuli zozote za kijamii na hata zile za maendeleo za nyumbani kwangu na wakati mwingine nilijinyanyapaa,” anasema mama huyo ambaye sasa amekuwa balozi.
Ugonjwa wa Fistula huwapata wanawake wakati wa kujifungua hasa wale wanaojifungua wakiwa na umri mdogo pamoja na kukosa msaada stahiki wakati wa kujifungua, ambapo viungo kama kibofu cha mkojo na njia ya haja kubwa hujeruhiwa na kusababisha mwanamke ashindwe kujizuia haja ndogo au kubwa.
Manusura wa Fistula wakipewa huduma ya afya katika kitu cha Mabinti Centre kilichopo katika hospitali ya CCBRT jijini Dar es Salaam. Picha| UNFPA Tanzania/Bright Warren.
Wagonjwa wapungua
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa Fistula wanaotibiwa katika vituo vinavyotoa huduma hiyo nchini imepungua kwa asilimia 30 ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita tangu mwaka 2015.
Licha ya idadi ya wagonjwa wenye tatizo la fistula kupungua kila mwaka, baadhi ya wanawake bado wana uelewa mdogo kuhusu ugonjwa huo jambo linalowafanya wachelewa kuundua na kupata matibabu.
Mmoja wa wanawake wanaopata matibabu katika hospitali ya CCBRT ya jijini Dar es Salaam Tanzania, Magreth Rubeni anasema kuwa baada ya kupata mtoto wa tatu ndipo alijulikana ana ugonjwa wa fistula.
“Wakati nipo Singida nilizaa mtoto wa kwanza nipo vizuri, nikazaa wa pili pia nilikuwa nipo vizuri, mtoto wa watu nikaambiwa yupo mgongoni wakamtoa, na nikaambiwa pia mtoto alipita na kukwaruza kibofu cha mkojo baada ya miaka miwili nikawa na maumivu makali nikarudi hospitali kupima na nikaambiwa na daktari nina Fistula,” anasema Magreth.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani (WHO) inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote, kwa upande wa Tanzania baadhi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.
Zinazohusiana:
- Simu za mkononi sasa kupima ugonjwa wa kifua kikuu
-
Simu benki inavyorahisisha matibabu kwa wanawake wenye fistula Tanzania
Sababu kupungua kwa wagonjwa wa fistula
Mkurugenzi wa Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Dk Paul Mhame aliyekuwa akizungumza leo Mei 23, 2021 katika maadhimisho ya siku ya kutokomeza ugonjwa wa fistula duniani yaliyofanyika katika hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza anasema kupungua kwa wagonjwa kunachangiwa na kuimarika kwa huduma za afya katika vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa wanawake wajawazito.
Amesema hivi sasa wanawake wajawazito wanapata mahuhurio yote manne ya kliniki sawa na asilimia 80 tofauti na mwaka 2015/ 16 ambapo mahudhurio yalikuwa kwa asilimia 41.
“Wanawake pia wameendelea kujifungulia kwenye vituo vya afya kwa asilimia 83 tofauti na miaka ya nyuma ambapo waliojifungulia kwenye vituo hivyo walikuwa ni asilimia 54,” anasema Dk Mhamed.
Vituo vya huduma ya dharura vimeongezeka kutoka 115 mwaka 2015/16 hadi kufikia 552 mwaka huu, amesema Dk Mhame.
Upasuaji nao wachangia Fistula
Pamoja na sababu mbalimbali zinazotajwa kuchangia ugonjwa huo ikiwemo uzazi pingamizi, pia upasuaji husababisha tatizo hilo kwa wanawake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Rufaa Bugando, Dk Fabian Massaga anasema mafunzo yanayotolewa vyuoni kuhusu upasuaji yatolewe kikamilifu ili kuzuia tatizo hilo.
“Upasuaji pia ni sababu nyingine kwa sasa ambayo inachangia kuwepo kwa wagonjwa wa Fistula, hivyo tunaomba wakufunzi wa vyuo vya afya waanze kutoa elimu sahihi ya kufanya upasuaji ili kupunguza ugonjwa huo,” anasema Dk Massaga.
Dk Massaga anasema katika hospitali hiyo kila mwaka hupokea wagonjwa kati ya 300 hadi 400 wa Fistula ambao wanatibiwa bure.
Kwa mujibu wa Dk Peter Mjinge kutoka hospitali ya CCBRT, Fistula ni tundu lisilo la kawaida ambalo linakuwa kati ya njia ya uke na njia ya kibofu cha mkojo lakini pia inaweza kuwa kati ya njia ya uke na njia ya haja kubwa na hili husababisha mama kutokwa na haja ndogo au kubwa bila hiari yake.
“Kisingi matatizo hayo zaidi yanasababishwa na mtu kupata maumivu au uchungu wa uzazi kwa muda mrefu wa zaidi ya saa 24 wakati wa kujifungua. Huwa tunawatibu wakinamama kutoka sehemu mbalimbali nchi Tanzania, na tunatoa tiba ya Fistula bure kwa wagonjwa wote,” anasema Dk Mjinge wakati akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa (UN).
Mikoa vinara wa Fistula
Awali daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake kutoka CCRBT, Dk Issa Rashid anataja mikoa inayoongoza kwa kupokea wagonjwa wa Fistula kuwa ni Rukwa, Kagera na Dar es Salaam kwa asilimia 20.
Dk Rashid anasema toka mwaka 2003 zaidi ya wagonjwa 8,000 wamepokelewa na kutibiwa na CCBRT na asilimia 96 ya watu hao hufuatiliwa na husaidiwa kwa mahitaji mbalimbali muhimu ikiwemo afya na mahitaji mengine ya familia.
Baadhi ya washiriki katika maadhimisho siku ya Fistula duniani yaliyofanyika jijini Mwanza leo Mei 23, 2022 ambapo kauli mbiu ilikuwa “Tokomeza Fistula wekeza, Imarisha Ubora wa Huduma ya Afya, Wekeza Kwenye Jamii”. Picha na Mariam John.
Msiwatenge wagonjwa
Pamoja na mafanikio hayo bado kuna changamoto ya wagonjwa kutengwa na ndugu zao, waume na kunyimwa stahiki zao.
“Tunaomba kila mmoja kuwa balozi wa kuwasaidia wagonjwa wa Fistula pamoja na kuondoa imani potofu kuwa wagonjwa hao wamerogwa,” anasema Dk Rashid.
CCBRT wameweza kuwasaidia wanawake hao, siyo tu kuwapa matibabu ya bure bali kuwa na kitengo cha Mabinti Centre ambacho kinasaidia kutoa huduma zaidi kwa wamama wenye Fistula wakati wakiwa hospitalini hapo.
“Wanawake hawa wenye Fistula wakiwa hapa Mabinti Centre huwa tunawapa ushauri na moyo wa kutokukata tamaa, huwa tunaimba nyimbo mbalimbali na kucheza kwa pamoja, tunawafundisha kushona na kama ikitokea mtu kapona huwa tunawasaidia kwa kuwawezesha biashara ndogondogo hasa kwa wale ambao wameachwa na wanaume zao kutokana na Fistula.
“Pia tunatoa kanga kama zawadi kwa kila mwanamke aliyepona Fistula.” anasema Mnasihi wa kituo hicho, Sababu Mwanjoka.
Nyongeza na Daniel Samson
Latest
