TCRA yawaonya wamiliki vyombo vya habari vya mtandaoni
- Ni wanaotumia udanganyifu kupata watu wa kuwafuatilia mtandaoni.
- Watakiwa kuripoti matukio katika uhalisia wake.
Mwanza. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wamiliki wa vyombo vya habari vya mtandaoni kuhakiki uhalisia wa habari zao kabla ya kuzitoa kwa umma ili kuepuka mkono wa sheria.
Makosa ya mtandaoni ikiwemo upotoshaji yanashughulikiwa na Sheria ya Makosa ya mtandaoni ya mwaka 2015, Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo amesema baadhi ya vyombo vya habari vya mtandaoni vinatumia udangajifu kuwavuta watu kuwa ikiwemo kutumia vichwa vya habari visivyoendana na maudhui ya habari husika.
“Huenda inasababishwa na mmiliki kutaka kurudisha haraka gharama zake alizotoa kwenye usajili, wengine wanatumia lengo ni kupata wafuasi wengi ili kutengeneza faida lakini hii siyo sawa tujitahidi kutoa taarifa zenye uhalisia,” amesema Mihayo wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya wanahabari kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo madhara ya habari za uzushi hivi karibuni jijini Mwanza.
Soma zaidi: CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Mkutano huo umeandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Internews.
Mihayo amewataka waandishi wa habari waliopata mafunzo hayo kuwa mabalozi wa kukemea habari za upotoshwaji zinazoripotiwa kwenye mitandao ya kijamii.
Awali Mwenyekiti wa MPC, Edwin Soko amesema lengo la mkutano huo ni kuwaleta pamoja waandishi wa habari kukumbushana jukumu kubwa la kusimamia maadili ya uandishi habari.
“Tunatamani kuona waandishi wa habari wakifanya kazi zao bila kuvunja sheri au kukumbwa kwenye mkondo wa sheria lakini pia waweze kubaini habari zisizo sahihi na kuziepuka,” amesema Soko.
Mwenyekiti huyo amesema wanakusudia kuwakutanisha waandishi wa habari za mtandaoni ili kuwafunda waweze kufanya kazi kwa weledi kupunguza changamoto za ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari.
Latest