Watu 26 kati ya 43 waokolewa ajali ya ndege ya Precision Air
- Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amesema wanaendelea kuivuta ndege iweze kutoka
- Waokoaji bado wana mawasiliano na marubani
Dar es Salaam. Watu 26 wameokolewa kutoka ndani ya ndege ya Shirika la ndege la Precision Air iliyopata ajali katika Ziwa Victoria huku vikosi vya uokoaji vikiendelea na jitihada za kuwaokoa wengine 17 waliosalia katika ndege hiyo.
Ndege hiyo yenye namba PW 494 iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam imepata ajali leo asubuhi Novemba 6, 2022 wakati ikianza kutua katika uwanja huo uliopo kandokando mwa ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewaambia wanahabari leo kuwa ajali hiyo ilitokea kati ya Saa 2:20 na Saa 2:25 asubuhi katika eneo hilo lililopo karibu na uwanja wa ndege wa Bukoba.
Waokoaji wakiendelea kuwaokoa watu waliosalia ndani ya ndege ya Precision Air baada ya ajali iliyotikea leo asubuhi. Picha:Hisani/Twitter.
“Ndege hiyo ilikuwa na jumla ya watu 43. Kati ya hao 39 ni abiria, wawili ni wahudumu wa ndege na wawili ni marubani,” amesema Chalamila.
“Hadi sasa ninavyozungumza tumeshafanikiwa kuokoa watu 26 ambao wameshapelekwa moja kwa moja katika hospitali ya mkoa wa Kagera,” ameongeza.
Chalamila amesema Serikali itatoa taarifa za kina kuhusu hali ya watu waliowaokolewa kwenye ajali hiyo
“Mpaka sasa tuna mawasiliano ndani ya ndege kwa mantiki marubani wanaendelea kuwa na mawasiliano,” amesema Chalamila.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali hiyo na kuwatumia salamu za pole watu wote walioathirika na ajali hiyo.
“Tuendelee kuwa watulivu wakati huu zoezi la uokoaji likiendelea huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusaidie,” amesema Rais Samia.
Latest