Mfumuko wa bei ulivyoporomosha kiwango cha ujira duniani
-
Inakadiria kuwa kiwango cha ujira duniani kimepungua kwa asilimia hasi 0.9 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2022.
- Hali hiyo imechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kudorora kwa ukuaji wa uchumi duniani na vita ya Ukraine na Urusi.
- Hatua za haraka za kisera kusaidia kuendeleza uwezo wa watu wa kipato cha chini kununua bidhaa na kuhudumia familia zao zinahitajika.
Dar es Salaam. Inakadiria kuwa kiwango cha ujira duniani kimepungua kwa asilimia hasi 0.9 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2022, ikiwa ni mara ya kwanza katika karne hii kiwango hicho kuwa hasi, ripoti mpya imeeleza.
Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO) imesema hali hiyo inapunguza uwezo wa manunuzi wa watu wa vipato vya kati, huku kaya za kipato cha chini nazo zikiwa zimeathirika zaidi.
Ripoti hiyo ya Ujira duniani mwaka 2022-2023: Athari za mfumuko wa bei na Uviko-19 kwenye ujira na uwezo wa ununuzi. iliyotolewa Novemba 30, 2022 jijini Geneva, Uswisi imeeleza kuwa miongoni mwa wanachama wa kundi la nchi tajiri duniani (G20), ujira halisi ulipungua kwa asilimia hasi 2.2 (-2.2%).
Nchi 20 zinazoibuka kiuchumi, ujira halisi ulikua kwa asilimia 0.8 (0.8%) ikiwa ni pungufu kwa asilimia 2.6 (2.6%) ikilinganishwa na mwaka 2019, ambao ni mwaka mmoja kabla ya janga la Uviko-19.
Ripoti hiyo imesema hali hiyo imechangiwa na janga la mfumuko wa bei likichanganyika na kudorora kwa ukuaji wa uchumi duniani. Pia vita nchini Ukraine na janga la nishati duniani kwa pamoja vinasababisha anguko la viwango vya mishahara na ujira kwenye nchi nyingi duniani.
Mathalan, mfumuko wa bei nchini Tanzania kwa mwaka unaoishia Oktoba 2022 uliongezeka hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 4.8 mwaka unaoishia Septemba 2022 ambapo umekuwa ukipanda mfululizo tangu Aprili mwaka huu.
Vijana wa kike wakifungasha maharagwe kwenye shamba mjini Addis Ababa, Ethiopia. Picha | ILO/Sven Torfinn
Athari za ujira kupungua
“Majanga lukuki yanayokabili dunia yamechochea kuporomoka kwa ujira halisi. Hali hii imeweka makumi ya mamilioni ya wafanyakazi kwenye hali mbaya wakati huu wanakabiliwa na mustakabali wasiokuwa na uhakika nao,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert Houngbo.
Houngbo amesema ukosefu wa usawa kwenye kipato na umaskini vitaongezeka iwapo uwezo wa ununuzi kwa wale wanaopata kipato cha chini hautashughulikiwa.
“Hii inaweza kuchochea zaidi mizozo ya kijamii duniani kote na kuporomosha lengo la kufanikisha ustawi na amani kwa wote,” amesema bosi huyo wa ILO.
Gharama ya maisha inaongeza changamoto kwa wafanyakazi waliopoteza ajira na familia zao wakati wa janga la Uviko-19 hasa makundi ya vipato vya chini.
Ripoti inaonesha kuwa ongezeko la mfumuko wa bei unaongeza gharama ya maisha kwa watu wa kipato cha chini. “Hii ni kwa sababu wanatumia fedha waliyonayo kugharamia huduma na bidhaa muhimu ambazo kwa kawaida huongezeka bei kuliko bidhaa zisizo za lazima.”
Hata hivyo, ripoti hiyo imechambua takwimu kikanda na kitaifa ambapo kikanda inaonesha kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022, mfumuko wa bei ulishamiri zaidi katika nchi za kipato cha juu kuliko nchi za kipato cha chini na kati.
Zinazohusiana:
Suluhu hii hapa
Uchambuzi wa ripoti hiyo unapendekeza hatua za haraka za kisera kusaidia kuendeleza uwezo wa watu wa kipato cha chini kununua bidhaa na kuhudumia familia zao.
“Marekebisho ya viwango vya kima cha chini ya ujira au mshahara yanaweza kuwa mbinu madhubuti, kwa kuzingatia kuwa asilimia 90 ya nchi wanachama wa ILO wana mfumo wa kima cha chini cha mshahara,” inapendekeza ripoti hiyo.
Mapema Julai 2022, Serikali ya Tanzania ilipandisha kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa umma nchini humo kwa asilimia 23.3.
Nyongeza hiyo ilifanyika kwa kuzingatia Pato la Taifa (GDP), mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa katika mwaka wa fedha wa 2022/23 na hali ya uchumi wa ndani na nje ya nchi
Ripoti hiyo inapendekeza mazungumzo ya pande tatu: mwajiri, mwajiriwa na vyama vya wafanyakazi, yanaweza kuweka uthabiti kwenye mjadala wa kuongeza mshahara na hivyo kufanikisha marekebisho kwenye janga la ujira.
Sera nyingine zinazoweza kulegeza madhara ya ongezeko la gharama ya maisha kwa kaya ni pamoja na zile zinazolenga makundi maalum kama vile kutoa vocha kwa kaya za kipato cha chini ili ziweze kununua bidhaa za msingi au muhimu.
Kupunguza kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye bidha kunaweza pia kupunguza mzigo wa mfumuko wa bei na hivyo kuwapunguzia wananchi makali ya maisha.
Latest
