Elimu ya saikolojia ilivyoboresha maisha ya watu wenye aulbino Tanzania
- Imewasaidia kujiamini na kufukuzia fursa za kiuchumi na elimu.
- Imeongeza thamani ya maisha yao kwenye jamii.
- Wadau, Serikali waendelea kuwalinda na kushirikiana nao.
Mwanza. Licha ya watu wenye ualbino nchini Tanzania kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za kiusalama, elimu na tiba ya kisaikolojia inaweza kuwaisaidia kujiamini na kutekeleza shughuli za kiuchumi ili kujiletea maendeleo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania Mkoa wa Mwanza (Shivyawata), Alfred Kapole amesema kwa sasa hali ya kimaisha ya watu wenye ualbino imeirika zaidi ikilinganishwa zamani.
Kapole ambaye pia ana ualbino amesema hiyo imechangiwa na tiba ya kisaikolojia inayoendelea kutolewa kwa kundi hilo.
“Tulionekana kama mizimu wakitupa majina mabaya zeruzeru kila mmoja na jina lake baya kulingana na kabila analotoka hii ilituathiri kisaikolojia ila sasa tunajua jinsi ya kujimudu,” amesema Kapole.
Kapole akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) amesema kuwa elimu ya kutambua maana ya ualbino na changamoto zinazowakabili imelifanya kundi hilo kutambua thamani yao katika jamii.
“Mwanzoni ilikiwa ukipishana na mtu anaweza hata kutema mate chini kuashiria Mwenyezi Mungu amuepusha kuzaa mtoto mwenye ualbino, lakini sasa hili limepungua.
“Tunatambua sisi ni binadamu kama walivyo wengine, tuna haki sawa kama wengine, tunaweza kugombea, kufanya biashara, kusoma na leo hii wapo waliyofika mbali zaidi,” amesema Kapole.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), mtu mmoja kati ya 1,400 ana ualbino nchini Tanzania. Hivyo kundi hilo ni lina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Watu wenye ualbino ni binadamu kama wengine. Wanahitaji kuthaminiwa na kupata haki zao ili kuboresha maisha. Picha | DW.
Hakuna kukaa nyuma
Kutokana na jitihada mbalimbali za kuboresha maisha ya watu wenye ulbino nchini katika miaka ya hivi karibuni wamewasaidia kujiamini na kupigania haki na ndoto zao.
Happiness Cleophace mwenye ualbino na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) kampasi ya Mwanza amesema kuwa elimu ya kisaikolojia imemjenga kuhuisha jitihada za kutafuta elimu na kujua kuwa ana haki ya kusoma kama watu wengine.
“Tulitishiwa sana usalama wetu, ila hali kiasi kikubwa imebadilika, miundombinu isiyo rafiki kwa baadhi ya taasisi za kutolea elimu ndiyo bado changamoto kwetu kwani baadhi yetu wana uono hafifu,” amesema Cleophace.
Cleophace ameiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa watu wenye imani potofu dhidi yao kwani kunarejesha nyuma juhudi za kuimarisha saikolojia ya kundi hilo.
Elimu ya kisaikolojia pia imewasaidia watu wenye ualbino kupata uwezo wa kutambua thamani yao katika jamii.
“Mwanzo ilikuwa ni aghalabu sana kuona mtu mwenye ualbino anashiriki jambo kubwa la kimaendeleo, mimi ni miongoni mwa wengi tunaozidi kubadilisha mtazamo huo,” amesema Richard Ferooz, mtu mwenye Ualbino na mchambuzi wa masuala ya kisiasa jijini Mwanza.
“Mimi naamini kuwa binadamu wote wana haki sawa, hili linanipa nguvu ya kushiriki shughuli nyingi na kwa ufanisi mkubwa,” amesema Ferooz.
Hata hivyo, elimu ya kisaikolojia bado haijaweza kuwafikia watu wote wenye Ualbino nchini wanaokadiriwa kufikia milioni 2, jambo ambalo linawaacha nyuma baadhi yao hasa kufaidika na fursa za kiuchumi na elimu.
Ferooz amependekeza kutolewa kwa elimu hiyo mara kwa mara ili watu wenye ualbino wazidi kuimarika kifikra na kuacha uwoga wakati wa kutekeleza shughuli zao.
Zinazohusiana:
-
Namna ya kupunguza gharama za manunuzi ya vyakula, vinywaji msimu wa sikukuu
-
Mzazi fanya haya kumuandaa mtoto na muhula mpya wa masomo mwaka 2023
- Namna bora ya kupanga, kutimiza malengo yako mwaka 2023
Aisha Mikingi, mkazi wa Kata ya Luchelele jijini Mwanza, akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) amesema kuwa anayaona mabadiliko makubwa kwa kundi hilo.
“Miaka ya nyuma watu wenye ualbino waliogopeka sana, hata kukaa nae karibu ilikuwa ngumu lakini wewe mwenyewe unaona imani mbaya zimebadilika tunawaamini na wao wanajiamini pia,” mesema Mikingi.
Kauli hiyo haikupishana na mkazi mwingine wa jijini hapa, Joan Christopher ambaye amesema kuwa daima husimama upande wao pindi panapotokea jambo hasi dhidi yao.
“Ili kuimarisha saikolojia zao kwanza nashirikiana nao, siwatengi, na changamoto yao naiona kama ya kwangu,” amesema Christopher huku akiiomba Serikali na wadau kushirikiana kutoa elimu kwa jamii izidi kutambua thamani ya kundi hilo kwenye maendeleo ya Tanzania.
Mwanasaikolojia na Mhadhiri wa SAUT, Leons Maziku amesema kuwa kuimarika kwa saikolojia ya binadamu yeyote ndiyo msingi wa maendeleo yake binafsi.
“Tunajikita kumtafakarisha mtu ajue yeye ni nani, ana hadhi gani na mchango wake ni upi katika taifa,” amesema Maziku.
Amesema ili kumjenga mtu kisaikolojia wanazingatia kubadili kwanza mtazamo wa mtu ili kumuweka katika njia sahihi.
“Matendo ni zao la fikra, huwezi kutenda bila kufikiri na sisi tunamjenga mtu kuwa na fikra chanya tukijua matendo yake yatakuwa mazuri pia,” amesema.
Mashirika ya Under The Same Sun na Standing Invoice yamekuwa mstari wa mbele kuchangia harakati za kuimaarisha saikolojia za watu wenye ualbino nchini ili kuwawezesha kuboresha maisha yao.
“Kuna kipindi Kanda ya Ziwa kulikuwa na matukio mengi ya mauaji ya watu wenye ualbino, mashirika haya yamechangia sana kututuliza kiakili na kupunguza hofu iliyokuwa miongoni mwetu,” amesema Kapole.
Latest