Walimu 8 wakamatwa kwa wizi wa zaidi ya Sh273 milioni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa akionyesha pikipiki zilizokamwatwa katika matukio ya uhalifu. Picha | Mariam John.
- Wanadaiwa kuiba fedha hizo katika benki ya Mwalimu Commercial.
- Walijihimishia katika akaunti zao kinyume na taratibu.
Mwanza. Jeshi la polisi mkoani Mwanza limefanikiwa kukamata watuhumiwa 1,100 wa matukio mbalimbali ya uhalifu pamoja na ya usalama barabarani wakiwemo walimu nane waliohusika utapeli wa mtandaoni.
Kati ya watuhumiwa hao, mmoja ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahina jijini Mwanza, George Shabani (35) ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya mtoto wake wa kiume aliyekuwa anamwadhibu kwa fimbo baada ya kwenda kuiba mahindi mabichi kwenye shamba la jirani.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbroad Mtafungwa amesema tukio hilo limetokea leo Machi 3, 2023 ambapo baba huyo alichukua fimbo na kuanza kumpiga mtoto wake maeneo mbalimbali ya mwili akiwa na lengo la kumuonya kutokana na kitendo alichokifanya ambacho kinafedhehesha familia.
Amesema wakati anaendelea kumchapa, ghafla hali ya mtoto ilibadilika na kuamua kumpeleka kituo cha afya Buzuga  lakini ilishindikana na kuhamishiwa Bugando ambako alifariki muda mfupi wakati anapatiwa matibabu.
Mtoto aliyefariki dunia ni Emanuel Shabani (14) aliyekuwa anasoma Shule ya Msingi Nyangurukuru.
Baada ya tukio hilo, baba mzazi alijisalimisha kwenye kituo cha polisi ambapo atapandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji hayo.
Tukio lingine ni walimu nane wa shule za msingi wilayani Sengerema ambao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za wizi wa fedha kwa njia ya mtandao kwenye benki moja ya Mwalimu Commercial iliyopo jijini Mwanza.
Kamanda Mtafungwa amesema tukio hilo liligundulika Februari 20 mwaka huu ambapo uongozi wa benki hiyo walibaini wizi wa fedha kwa njia ya mtandao.Â
Amewataja walimu hao kuwa ni Masaba Kiula, Gasper Maganga wa Shule ya msingi Kilabela, Marwa Mwita (Shule ya Msingi Nyitundu), Alodi Benard Shule ya Msingi Bungumbikiso), Cleva Gidison (Shule ya Msingi Nyamatongo) na Jastoti Diego wa Shule ya Msingi  Ishishsangoro.
Wengine ni Fredirick Diego kutoka Shule ya Msingi ya Pamba C na Steven Sambari  Nyagongwa ambao walifanikiwa kuingilia mawasiliano ya akaunti za hiyo benki na kufanikiwa kuchukua kiasi cha  Sh273.5 milioni na kuhamishia kwenye akaunti zao.
Walimu hao pia walikamatwa na pikipiki mpya ambazo zilinunuliwa kupitia hizo fedha walizoiba kutoka kwenye akaunti hiyo.
“Baada ya kupokea taarifa hizo, Jeshi la polisi lilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata walimu hao ambapo baada ya kufanya mahojiano na kupekua kwenye akaunti zao walikuta kiasi hicho cha fedha. Â
Kamanda Mtafungwa amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.