Mfahamu mvumbuzi wa ndege isiyo na rubani itakayoleta mapinduzi ya kilimo Tanzania

December 27, 2022 7:34 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mhitimu wa shahada ya uhandisi wa Kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tukupala Mwalyolo
  • Itasaidia kuboresha kilimo cha umwagiliaji na kudhibiti wadudu waharibifu mashambani. 

Dar es Salaam. “Familia yangu ni wakulima, tulikuwa tunapata changamoto wakati wa kupulizia dawa, baadhi zilikuwa zinatuathiri, nikajiuliza  je siwezi kutumia ujuzi wangu kuisaidia familia yangu na taifa kwa ujumla?,”.

Ni Tukupala Mwalyolo (23), mhandisi wa kompyuta, akielezea kile kilichomsukuma  kubuni ndege isiyo na rubani (drone) ambayo itatumika katika shughuli za kilimo ikiwemo kunyunyizia dawa kwenye mazao na umwagiliaji.

Drone hiyo  ina uwezo wa kubeba lita tano za dawa, kutembea mita 4,900 ndani ya dakika 15 na kukaa angani kwa wastani wa dakika 15 mpaka 20, kabla ya kuchajiwa tena.

Tukupala ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anaamini uvumbuzi huo utawasaidia wakulima wa Tanzania ambao hukabiliwa na matatizo wakati wa kunyunyiza dawa kwenye mazao ikiwemo kuathirika kiafya, kutofikia mazao marefu, na ugumu unaotokana na jiografia ya eneo husika hususani maeneo ya milimani.

“Drone hii itasaidia kuokoa muda, hususan watu wenye maeneo makubwa hulazimika kuajiri watu wengi na hivyo hutumia gharama kubwa pamoja na muda , drone itaweza kufanya hayo kwa muda mfupi,” anasema Tukupala.

Safari ya uvumbuzi

Tukupala alianza rasmi safari ya uvumbuzi wa teknolojia hiyo miaka minne iliyopita mara baada ya kupata nafasi ya kushiriki mafunzo kwa vitendo kutoka taasisi ya Resilience Academy ambako alijifunza kutengeneza drone kwa kutumia vifaa vya majumbani (local materials).

Mapenzi yake katika masuala ya anga ndiyo yalimsukuma kuendelea na mafunzo hayo ambapo alijikita  zaidi kujifunza  namna  teknolojia ya drone inavyofanya kazi pamoja na upatikanaji wa malighafi za kutengeneza kifaa hicho.

Januari 2022 kupitia programu ya OpenSkies Fellows alipata nafasi ya kuwasilisha wazo bunifu la teknolojia ambalo litakuwa na msaada kwa jamii kisha hufadhiliwa kiasi fulani cha fedha ili liboreshwe na kufanyiwa kazi.

“Taasisi niliyokuwa najifunza masuala ya drone ya Open Map Development Tanzania walianzisha programu ya OpenSkies Fellows iliyolenga vijana wenye mawazo yenye msaada kwenye jamii, ndipo nilipowasilisha wazo la kuja na drone itakayotumika kwenye shughuli za kilimo hususan kunyunyiza dawa, “ anasema Tukupala.

Kwa mujibu wa Tukupala Ilimchukua miezi 12 kukamilisha uundaji wa drone hiyo pamoja na kuiwekea teknolojia ya kunyunyizia dawa huku kutopatikana kwa baadhi ya vifaa hapa nchini kukichelewesha ukamilishaji wake.


Zinazohisiana: 


Milima na mabonde

Kama wasemavyo wahenga kwamba mtaka cha uvunguni sharti ainame ndivyo ilivyomlazimu Tukupala kuumiza akili yake kwa kufikiri  muda mwingi juu ya namna ya kuifanya drone hiyo ifanye kazi anayoikusudia.

“Safari haikuwa nyepesi, hususani kwenye kuiwekea teknolojia ya kuifanya imwagilie ikiwa angani na sio ikiwa chini au ikiwa inapaa, ni kitu ambacho kilituumiza sana kichwa kuna programu nyingi tu zimekataa, nilitumia uwezo wangu wote wa kufikiri hatimaye nikafanikiwa, “ anasema Tukupala huku uso wake ukiwa na tabasamu.

Tukupala akiwa katika shughuli za uundaji wa drone hiyo. Pichal Tukupala Mwalyolo

Itapatikanaje?

Kutokana na takwa la kisheria ambalo linamtaka mtu yoyote anayerusha drone kuwa na kibali maalumu , Tukupala anasema amejiandaa kutoa huduma kwa wakulima ambapo yeye kwa kushirikiana na timu yake watawafuata wakulima mahali walipo na kutoa huduma hiyo.

“Kwa sasa nimelenga kutoa huduma kwa wakulima, ili urushe drone lazima uwe na ujuzi pamoja na leseni ambayo si wote wanayo, ili kuwafikia walengwa mimi nitaenda kuwapatia huduma kwa gharama tutakazokubaliana,” anasema. 

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe lipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 alisema mpango na bajeti ya wizara kwa mwaka 2022/23 unalenga kujenga msingi imara wa ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kiwango cha asilimia 10 ifikapo 2030.

Ili kufikia kiwango hicho, Serikali itashirikiana na wadau kuchagiza matumizi ya teknolojia za kisasa za uzalishaji mazao, kilimo cha umwagiliaji na kuwawezesha wakulima kupata masoko ya mazao yao. 

Tukupala ameiambia www.nukta.co.tz kuwa teknolojia hiyo itachochea na kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo kwani uzalishaji utaongezeka kutokana na kutumia muda mchache katika eneo kubwa, kuokoa afya za watu pamoja na kufika maeneo yasiyofikika kiurahisi.

Kwa sasa Tukupala anaendelea na maboresho ya mapungufu madogo aliyoyabaini katika drone hiyo ambapo pia ametoa wito kwa Wizara ya Kilimo kumuunga mkono kwa kumuwezesha vifaa ili aunde nyingi zaidi na kuwasaidia wakulima.

“Naomba Serikali iutazame ubunifu huu, kisha itazame namna gani inaweza ikachangia ili kuongeza tija ya teknolojia hii kwa wakulima binafsi hata mashamba ya Serikali,” anasema Tukupala.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo,  sekta ya kilimo hutoa ajira kwa asilimia 65.5 na huchangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa, pamoja na asilimia 65 ya malighafi za viwanda.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW