‘Startups’ zinavyoweza kuondokana na dhana potofu ya upatikanaji wa mitaji

February 8, 2019 5:56 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kuanza kutumia rasimali zinazowazunguka na kujenga mahusiano mazuri na wawekezaji wenye nia ya kuendeleza kampuni zinazochipukia.
  • Kujifunza kuwa na kikomo katika kupokea pesa za uwekezaji ili kuepuka mtego wa kuwa waajiriwa.

Dar es Salaam. Suala la kampuni zinazochipukia (Startups) kupata mitaji imekuwa changamoto katika ukuaji wa shughuli zao hasa kutokana na kuwepo kwa dhana hasi juu ya upatikanaji wa mitaji kuendeleza biashara zao. 

Mashirika na wataalam mbalimbali wanaohusika na uwekezaji wa mitaji katika taasisi na kampuni zinazotumia teknolojia, wameendelea kutoa elimu kwa vijana wabunifu wenye nia ya kuongeza mitaji ili kuwaondolea dhana potofu kuhusu uwekezaji. 

Mtalaam wa uwekezaji na ujasiriamali kutoka kampuni ya Chanzo Capital ya Ghana, Erick Osiakwan  aliyekutana na wajasiriamali wa teknolojia zaidi ya 50 wenye ‘startups’ Februari 6, 201 jijini Dar es Salaam, alieleza jinsi kampuni hizo zinavyoweza kujiimarisha na kuvutia uwekezaji katika biashara zao.  

Osiakwan ambaye ana uzoefu wa kufanya kazi katika kampuni mbalimbali za teknolojia anaeleza kwa undani ni mambo gani ya kuzingatia kwa ‘startups’ kufanikiwa kupata mitaji ya uwekezaji.  

Watumie watu wanaokuzunguka 

Mtaalam huyo anasema watu hawa ni kama ndugu, jamaa na marafiki. Hii ni kwasababu kama wamekuamini na kutoa msaada wowote kwa ajili ya kampuni yako basi unaweza  kupata pa kuanzia.

Msaada huo unaweza kuwa wa mali au kukuunganisha na watu ambao watakupa mwongozo wa nini cha kufanya ili ufike mbali zaidi. Angalizo unatakiwa usitumie pesa ya uwekezaji kwa matumizi binafsi kwa sababu unaweza kupoteza dhima ya kuaminiwa na kupata msaada tena.


Zinazohusiana: 


Wateja wako ni muhimu katika kujipatia mtaji

Fikiria umeanza na mtaji wa 100,000 kuuza chakula alafu mteja mmoja akakipenda na kukuunganisha na watu wengine wengi na mtaji wako ukaongezeka kwasababu tu ulimridhisha vizuri mteja huyo.

Osiakwan anaeleza kuwa mjasiriamali mzuri ni yule anayemtumia mteja wake katika kujipatia pesa na kumbuka kuwa ukimhudumia mteja vizuri anaweza kuwa mwekezaji wako baadaye.

Hivyo dhana ya kuhisi mteja ni mtu wa mwisho katika kupata mtaji au pesa iondoe akilini mwako, na kabla hujawaza kutafuta mwekezaji anza kufikiria utampata wapi mteja atakayenunua huduma na bidhaa yako.

Njia nyingine ya mjasiriamali kufanikiwa ni kujichanganya na wajasiriamali wengine ili kupata fursa ya kusaidiana mbinu mbalimbali za kujikwamua. Picha| Zahara Tunda.

Anza kujenga mahusiano  kabla ya kuomba msaada

Hapa ni baada ya kuanzisha kampuni yako, Osiakwan anashauri hata kama unashida kubwa ya mtaji usimfuate na kueleza shida yako kabla hujatengeneza mazingira mazuri na mahusiano.

Jenga uhusiano wa kawaida kama kumjua vizuri mwekezaji wako, kuhudhuria katika matukio au makongamano mbalimbali ambayo anashiriki na jinsi gani anavyofanya kazi. Hii itakusaidia kujua anasimamia nini na jinsi ya kumueleza hitaji lako. 

Onyesha upekee wa bidhaa yako

Kila wazo au biashara unayofanya sio mpya kama unavyofikiria ila kinachoitofautisha biashara yako na wengine ni upekee wake katika kutatua tatizo fulani lililopo katika jamii.

Hivyo ili kupata mitaji hasa kwa wawekezaji Osiakwan anashauri mjasiriamali kumshawishi mwekezaji jinsi utakavyokuza kampuni yako na kwa jinsi gani utafikia huko na yeye kupata matokeo anayokusudia.

Kumbuka mwekezaji anaweka pesa zake na anataraji kupata faida ukifanikiwa kuonyesha njia utakazotumia kukuza mtaji hakuna mwekezaji atakayegoma kuweka pesa zake kwako.

Tambua aina ya mwekezaji unayemtaka katika kupata mtaji

Unapomkaribisha mwekezaji katika kampuni yako, fahamu kuwa usipoweka mipaka kati yenu unaweza kupoteza dhana zima ya uwekezaji.

Hivyo lazima uje unataka mwekezaji ambaye utarudisha pesa yake mara baada ya mtaji kukua, utampa nafasi ya umiliki (share) katika kampuni au mtashirikiana katika mambo mengine yatakayowasaidia wote wawili?

Hivyo mtalaam anasema ukichukua sana pesa za wawekezaji utaondoka katika dhana ya ujasiriamali na kuwa mwajiriwa wake hivyo hata kama unahitaji sana mtaji jifunze kuwa na kikomo.

Huu ni mwanzo wa mfululizo wa njia za kukuza pesa kwa kampuni inayochipukia. usikose sehemu ya pili itakayokujia hapahapa Nukta kwa yanayokuhusu.

Enable Notifications OK No thanks