Safari ya kurudi kileleni: Lini Iyunga Tech itarudi kwenye 10 bora kitaifa ?

Daniel Mwingira 0920Hrs   Mei 02, 2018 Habari
  • Shule ya sekondari ya ufundi ya Iyunga imefanikiwa kuingia katika shule 100 vinara mara moja tangu mwaka 2012 ndani ya miaka sita iliyopita.
  • Shule hiyo inafanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne ukilinganisha na yale ya kidato cha sita.

Dar es salaam. Miakaya nyuma kidogo  ilikuwa ni matamanio ya kila mtoto au mzazi kumpeleka mtoto wake katika shule kongwe za serikali na zilizokuwa za vipaji maalumu.

Shule ya Ufundi ya Iyunga maarufu kwa vijana kama Iyunga Tech iliyopo  katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilikuwa miongoni mwa shule hizo zilizojijengea  majina nyakati hizo.  Iliwahi kuvuma miaka ya nyuma kama shule za Mzumbe, Ifunda na Ilboru.

Lakini hali sasa ni tofauti kidogo.  Shule hizo kongwe nchi nzima zimebaki kuwa ni historia tu ukiacha na na chache kama Kibaha. Ukitaka kuitafuta Iyunga kwenye orodha ya shule bora nchini katika matokeo ya kidato cha nne huenda ukakesha kuipata hata kwenye orodha ya 100 bora. 

Hata hivyo, Serikali inasema inaendelea na mkakati wa kuzifufua upya shule hizo  kwa kuanza kuboresha majengo yake sambamba na mazingira yake katika jitihada  za kuzirudisha makali yake ya zamani.

Nukta imefanya tathmini ya matokeo ya kidato cha nne na sita yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2012 hadi 2017 kitaifa kwa shule zenye wanafunzi 40 na zaidi ili kubaini mwenendo wa ufaulu katika shule hiyo maarufu Nyanda za Juu Kusini.


Hali ilivyo matokeo ya kidato cha nne

Katika uchambuzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne (CSEE), Iyunga imefanikiwa kuingia katika orodha ya shule 100 vinara mara moja tu kwa kipindi cha miaka sita. Ilifanikiwa kufanya hivyo mwaka 2012 ambapo ilishika nafasi ya 65.

Vile vile mwaka huo 2012 shule nyingine ya umma ya Mbeya Sekondari  kutoka katika jiji hilo nayo ilifanikiwa kuingia katika shule 100 vinara kwa kushika nafasi 63. Sasa ikiwa ni takribani miaka sita hakuna shule kongwe yakutoka Mbeya ama shule yoyote ya umma kama ilivyofanya Mbeya sekondari imefanikiwa kuingia katika shule 100 vinara.

Kitaifa nafasi ya juu kabisa kuwahi kushikwa na shule hiyo ni 65 mwaka 2012 na ya chini zaidi ni nafasi ya 228.

Matokeo ya kidato cha nne

Shule 201220132014201520162017
Iyunga
5/249
11/249
  13/209
 17/270
11/192

10/154
Mbeya Sekondari
6/249
9/249
24/209
34/270
33/192
16/154


Hata hivyo, uchambuzi zaidi wa Nukta umebaini kuwa katika ngazi ya mkoa, Iyunga imekuwa ikifanya vizuri ambapo nafasi ya juu kuwahi kushika ni namba tano mwaka  2012 na ya chini kabisa ni ya 17 mwaka 2015. Kwa maana nyingine shule hiyo haijawahi kutoka nje ya 20 bora katika mkoa wa Mbeya wenye zaidi ya shule 200. Takwimu za Msingi za Elimu Tanzania (Best) mwaka 2016 zinaonyesha mkoa wa Mbeya una  shule za sekondari za umma 160  na binafsi 64.


Je wazijua shule bora mkoani Mbeya umpeleke mwanao? Soma zaidi katika tovuti ya Elimu Yangu hapa.


 

Nini kinaendelea matokeo ya kidato cha sita?

Katika matokeo ya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita ya (ACSEE) hali si ya kuridhisha kwa Iyunga kwa kipindi chote cha kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.


Shule 201220132014201520162017
Iyunga
24/26
25/26
25/25
22/25
25/32
23/30


Mathalani Shule ya Ufundi ya Iyunga toka mwaka 2012 hadi mwaka 2015 imekuwa miongoni mwa Shule tano za mwisho kimkoa. Huku mwaka 2014 ilikuwa ndiyo shule ya mwisho kabisa ndani ya mkoa wa Mbeya kwa kushika nafasi 25 kati ya shule 25. 

“Ahueni” kidogo ilitokeamwaka 2016 baada ya kushika nafasiya nane kutoka mkiani na mwaka ulifuatia 2017 iliingia kwenye saba za mwisho kimkoa. Yote hayo yanatokea licha ya mkoa wa Mbeya kuwa mkoa wa sita kitaifa kwa ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2017

 Zinazohusiana:   SHULE 24 VIGOGO 'ZILIZOTEKA' 10 BORA KIDATO CHA NNE 

Serikali kuboresha zaidi shule kongwe

Serikali inasema inaendelea na mkakati wa kuziboresha shule kongwe mkoani humo kama Iyunga na Loleza ili kuzirudisha katika hadhi zao.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Pauliana Mbigeza ameiambia Nukta kuwa kuna mkakati unaendelea kutekelezwa na Serikali wa kuboresha elimu  na kuzifanya shule hizo kongwe kurudisha hadhi zao na kwamba tayari shule ya Iyunga imeshakarabatiwa majengo yake.

‘’Tunaishukuru Serikali inavyokarabati shule hizo kongwe za mkoa wa Mbeya maana ukarabati huo utachangiakuzifanya shule hizo zikarudishamakeke yake ya mwanzo. Hii ni kwa kuwa kwa sasa wanafunzi watakuwa wanajisomea katika mazingira bora na walimu watakuwa na sehumu nzuri za kufanyia kazi  ukilinganisha na hali ilivyo kuwa mwanzoni,” anasema Mbigeza.

“Pia shule Kongwe nyingine ya Loleza nayo serikali imeiwekea mkakati wa kuikarabati na kuiboresha kama zilizvyo shule nyingine kongwe hapa nchini hivyo nayo ukarabati wake ukikamilika tutegemee mabadiliko makubwa,’’ anaongeza. 

Ni lini Iyunga itarudi kwenye orodha ya shule 10 bora Tanzania? Ni suala la muda. 


Related Post