Ni historia: Watumiaji wa intaneti Tanzania sasa wafikia milioni 23

February 22, 2018 6:22 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi hiyo ni mara tatu zaidi ya watumiaji wa intaneti waliorekodiwa mwaka 2012.
  • Zaidi ya robo tatu ya watumiaji wa intaneti mwaka 2017 wanatumia intaneti isiyo na waya inayohamishika (mobile wireless).

Dar es Salaam. Tanzania imevunja rekodi katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano baada ya kufikisha watumiaji wa intaneti takriban milioni 23 mwaka 2017, kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu ya kile kilichorekodiwa miaka mitano iliyopita.

Takwimu mpya za robo ya mwisho wa mwaka 2017 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti ilipaa kwa asilimia 15 hadi watumiaji milioni 22.99 mwaka 2017 kutoka milioni 19.86 mwaka 2016.

Kati ya watumiaji hao waliorekodiwa mwaka jana, 83 kwa kila 100 wanatumia intaneti inayohamishika (mobile wireless) ambayo hutumika zaidi na simu za mkononi, tablet na kompyuta mpakato (laptop). Ni watumiaji wawili tu kwa kila 100 ndiyo wanaotumia intaneti ya waya isiyohamishika (fixed wired).

Idadi ya watumiaji wa intaneti ya waya isiyohamishika imekuwa na historia ya kupanda na kushuka ndani ya miaka mitano iliyopita. Kiwango cha juu kurekodiwa ndani ya kipindi hicho  ni watumiaji 984,198 mwaka 2014 na cha chini zaidi ni watumiaji 319,698 mwaka uliofuatia.

Ukuaji huo, kwa mujibu wa TCRA, unafanya upatikanaji wa intaneti nchini kufikia asilimia 45 kutoka asilimia 40 iliyorekodiwa mwaka 2016. Ikumbukwe kuwa mwaka 2012 upatikanaji wa intaneti ulikuwa asilimia 17 tu.  Upatikanaji wa intaneti nchini kwa sasa unazidi wastani wa Afrika ambao ni asilimia 31.2 hadi kufikia Juni 2017 kwa mujibu wa mtandao wa internetworldstats.com ambao hufuatilia matumizi ya intaneti duniani.

Ripoti ya mwaka 2018 ya Shirila la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) iliyotolewa mwishoni mwa Januari inaeleza kuwa jitihada za kuboresha sera zinazohusu Tehama na uwekezaji katika mkongo wa Taifa wa mawasiliano (NICTBB) ni baadhi ya mambo yaliyofanya Tanzania ifanikiwe kuchochea ukuaji wa matumizi ya intaneti.


Soma: Yanayofahamika, yasiyofahamika kuhusu app ya Vsomo

Njia ya kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia


Ripoti hiyo iitwayo kwa Kiingereza ‘Achieving universal and affordable internet in the least developed countries’ inaeleza kuwa Tanzania ilikopa Dola za Marekani milioni 170 (zaidi ya Sh377 bilioni) kwa awamu mbili kutoka benki ya Exim ya China ili kugharamia mkongo huo wa taifa wa mawasiliano uliosambaa nchi nzima.

Kasi hiyo ya ukuaji wa intaneti ni moja ya hatua muhimu ya Tanzania katika kufikia malengo ya ukuaji wa uchumi kwa kutumia Tehama ifikapo mwaka 2020 kama ilivyobainishwa katika lengo namba 9.c la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.  

Utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2009 ulibainisha kuwa ukuaji wa upatikanaji wa intaneti ya waya isiyohamishika kwa asilimia 10 tu utachangia kukua kwa Pato la Taifa (GDP) la nchi zinazoendelea kwa asilimia 1.4. Upatikanaji wa intaneti ya kasi na bei nafuu unachangia ukuaji wa sekta mbalimbali nchini zikiwemo mawasiliano, kilimo, afya, uchukuzi, elimu, afya na habari.

Pia, ukuaji wa intaneti ni fursa kwa wajasiriamali nchini ambao sehemu kubwa ya biashara zao zinategemea upatikanaji wa intaneti kuwafikia wateja wao.

Biashara kama za programu za simu na kompyuta na habari mtandao zinategemea kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa intaneti ili kukua zaidi na kuleta faida inayostahili.

Benki ya Dunia inaeleza kuwa chini ya robo ya kampuni zote Tanzania zilikuwa hazina tovuti mwaka 2013.

Pamoja na ukauji huo, bado baadhi ya wadau wamekuwa wakilalamikia kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo intaneti yake ni ghali zaidi.

Enable Notifications OK No thanks