Zigo linalomsubiri Ndejembi Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania
- Ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
Dar es Salaam. Hatimaye Tanzania imepata Makamu wa Rais mpya, baada ya kuapishwa kwa Deogratius Ndejembi, leo Agosti 29, 2026 ikulu ya Chamwino, Dodoma.
Ndejembi aliyekuwa Waziri wa Nishati kwa takribani miezi tisa anaziba nafasi ya Makamu wa Rais iliyokuwa wazi kwa siku mbili baada ya aliyekuwa akihudumu katika nafasi hiyo Dk Emmanuel Nchimbi kutangaza kujizulu kabla ya kufukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) suala lililomuengua katika nafasi hiyo.
Akizungumza katika hafla ya uapisho wa Ndejembi Rais Samia Suluhu Hassan amesema matarajio ya watanzania ni kuona mteule huyo analitumikia Taifa kwa kutanguliza mbele maslahi ya nchi.
“Matamanio na matarajio yetu sote Watanzania kama nilivyotangulia kusema ni kwamba utalitumikia Taifa hili kwa utii, uaminifu, uzalendo, busara, hekima, maarifa na uzoefu ulio nao ukimtanguliza mbele mwenyezi Mungu na kwa maslani ya Taifa,” amesema Rais Samia.
Punde baada ya kuapishwa Ndejembi ataanza rasmi kuwatumikia Watanzania katika nafasi ya Makamu wa Rais lakini ni masuala yapi makubwa yanayomsubiri kiongozi huyo?
Kusimamia utekelezaji wa Dira ya 2050
Kama msaidizi wa kiongozi mkuu wa nchi Ndejembi atawajibika kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo pamoja na mambo mengine inalenga kufikia uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja.
Zigo kubwa linalomsubiri Ndejembi katika utekelezaji wa dira hiyo ni presha kubwa ya kiuchumi inayosababishwa na vita vya mashariki ya kati, kati ya Israeli, Marekani na Irani vinavyosababisha bei ya mafuta pamoja na bidhaa muhimu kuendelea kupaa nchini.
Licha ya changamoto hizo mchambuzi wa uchumi kutoka Dar es Salaam Paul Chengula amesema kibarua pekee alichonacho ni kumshauri Rais namna bora ya utekelezaji wa dira hiyo pamoja na mipango mingine ya maendeleo.
“Tutegemee makubwa kwa sababu ni nguvu mpya inaingia, yale ambayo Rais pamoja na Serikali wamekwisha kuyaanza, yeye anaweza kuyaendeleza kwa kumshauri vizuri Rais pamoja na Serikali ili kufikia malengo ya Dira ya 2050,” amesema Chengula.

Kusimamia masuala ya muungano
Mchambuzi wa masuala ya siasa na diplomasia Efron Mkungilwa amesema Ndejembi anajukumu la kusimamia masuala ya muungano kwa kuwa yapo ndani ya ofisi yake.
“Mambo yanayokuwa yakizungumzwa ambayo yanataka kuigawa nchi anapaswa kuiangalia na kuwaweka watu watakaoisimamia ili muungano udumu na nchi isonge mbele katika maendeleo ya nyanja zote,” ameongeza Mkungilwa.
Kusimamia utekelezaji wa katiba iliyopo
Licha ya presha ya madai ya katiba mpya iliyopo kutoka kwa wanasiasa wakongwe na wanaharakati wa upinzani, Mkungilwa amesema Serikali bado ina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa katiba iliyopo.

Mchambuzi huyo amesiitiza kuwa wakati Serikali ikiendelea kutathimini utekelezaji wa madai hayo Ndejembi atawajibika kuisimamia katiba iliyopo ili itengeneze mifumo na watu bora.
Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya kisiasa Baltazar Komba amesema umri na uzoefu wa Ndejembi vinaweza kumsaidia kuelewa lugha na matarajio ya vijana, hususani kizazi cha Gen Z na kufahamu namna rahisi ya kushughulikia changamoto zao.
“Dunia nzima leo imekuwa inapambana na hili kundi kubwa la vijana wanaojiita Gen Z, matakwa yao makubwa ni kupata riziki zinazoweza kuwafanya wajione kwamba ni sehemu ya wanaofurahia matunda ya dunia kwenye nchi zao,” amesema Komba.
Hata hivyo, Komba amesema uteuzi wa Ndejembi unapaswa kuangaliwa pia kupitia mahitaji na matarajio ya Rais aliyemteua, kwa kuwa hayo ndiyo yatakayoamua kwa kiasi kikubwa majukumu na matokeo yanayotarajiwa kutoka kwake.