Zanzibar yafikiria uamuzi wa kutumia sarafu ya kidijitali
- Yapokea elimu ya sarafu hiyo kabla haijaanza kutumika na raia wake.
- Ikianza kutumika itarahisisha huduma za kifedha na manunuzi.
- Wadau washauri Watanzania waelimishwe kwa undani kuhusu sarafu hiyo.
Dar es Salaam. Wakati matumizi ya sarafu ya kidigitali yakishika kasi duniani, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafikiria namna ya kuanza kutumia sarafu hiyo ili kurahisisha huduma za kifedha na kuongeza wigo wa ajira.
Kusudio hilo la Zanzibar limekuja baada ya kupita miezi mitano tangu Rais Samia aiagize Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza maandalizi ya kutumia sarafu ya kidijitali kutoka na kukua kwa teknolojia hiyo duniani.
Licha ya nchi mbalimbali duniani kuanza kutumia sarafu hiyo, Tanzania bado hajikubali teknolojia kutumika nchini.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakaa pamoja na wadau wa sarafu ya kidijitali (Digital currency) ili kuona kwa namna gani Zanzibar itaweza kuitumia sarafu hiyo.
Waziri Soraga aliyekuwa akizungumza ofisini kwake Mwanakwerekwe Unguja jana Novemba 8 wakati alipokutana na viongozi wa kampuni ya Hypertech Company Limited kutoka nchini South Afrika, ili kujadili namna ya kuitambulisha sarafu ya kidijitali visiwani Zanzibar.
Waziri Soraga amewahakikishia viongozi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar italichukulia suala hilo kwa umuhimu mkubwa ili kuona jinsi gani jambo hilo linaweza kufanikiwa.
Mwakilishi wa biashara hiyo kutoka kampuni ya Hypertech Company, Joe Chuene amesema muelekeo wa dunia kwa sasa ni kutumia sarafu ya kidijitali kufanya manunuzi ya vitu mbalimbali na inatumiwa na watu wengi pamoja na makampuni makubwa duniani.
Chuene amesema kuwa kwa sasa mzunguko wa sarafu ya kidijitali umefikia kiwango cha Dola za Marekani trillion 3.2 duniani kote, hivyo ameiyomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuitambua sarafu hiyo ili iweze kutumika kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi na serikali kwa ujumla.
Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Dk Charles Mwamwaja akizungumza na Mwanahamisi Mketo mmoja wa wajasiliamali kutoka kikundi cha Uwazi Makangarawe waliowezeshwa na TASAF alipotembelea mabanda mbalimbali yaliyoshiriki maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.
Wakati Zanzibar ikipokea elimu ya matumizi ya sarafu ya kidijitali, Serikali ya Tanzania imesema kuwa Watanzania chini ya asilimia 50 ndiyo waliofikiwa na huduma za fedha jambo ambalo limeifanya Serikali kuwa na Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ili kuongeza uelewa kwa wananchi kwa lengo la kuchochea ustawi wa jamii.
Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini, Dk Charles Mwamwaja amesema huduma za fedha zinarahisisha utaratibu wa kubadilishana bidhaa na huduma jambo ambalo ni muhimu katika maendeleo ya uchumi kwa nchi yeyote duniani ikiwemo Tanzania hivyo ni lazima kuwa na mkakati wa kutoa elimu kwa umma kuhusu uelewa wa huduma hiyo.
“Watu wanadhulumiwa na hawajui waende wapi, nani ni mtoaji wa huduma hiyo rasmi, mteja akidhulumiwa aende wapi na hawajui kuwa mteja wa huduma za fedha analindwa, hivyo Serikali imeamua kutoa elimu kwa umma ili kuondoa sintofahamu hiyo,” amesema.
Dk Mwamaja alikuwa akizungumza katika maonyesho ya Wiki ya Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam jana inayofanyika Novemba 8 hadi 14, 2021.
Amesema kuwa sekta ya fedha inarahisisha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji ndio maana vikundi vidogo vya kuweka na kukopa kama Vicoba, vinasaidia kukuza mitaji ambayo inaweza kutumika kuwekeza kwenye miradi ya ufugaji na mingine ambayo ina manufaa si tu kwa mtu mmoja mmoja bali kwa Taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema matokeo chanya ya sekta ya fedha hayawezi kufikiwa bila kuwekeza katika elimu ili wananchi waweze kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
Latest
