Zaidi ya Sh1 trilioni zitakavyomaliza tatizo la maji miji 28
- Ni fedha za mkopo kutoka india.
- Mradi huo utasaidia kuondoa shida ya maji katika miji hiyo.
Dar es Salaam. Tatizo la uhaba wa maji huenda likawa historia katika miji 28 nchini Tanzania ukiwemo Muheza mkoani Tanga pale utakapokamilika mradi wa maji katika miji hiyo wenye thamani ya Sh1.2 trilioni.
Mradi huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na India ambapo India kupitia benki ya Exim imeikopesha Tanzania kiasi hicho cha fedha ambacho kitatumika kujenga mindombinu ya maji na kusambazwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kati ya fedha hizo zilizotolewa na india, Tanzania bara imepata Dola za Marekani milioni 465 (Sh1.1 trilioni) na kiasi kilichobaki kitapelekwa Zanzibar.
Miji iliyobahatika kupata neema hiyo ni Muheza, Handeni na Pangani mkoani Tanga, Makonde, Nanyumbu na Kilwa Masoko (Mtwara), Ifakara (Morogoro), Chunya na Rujewa (Mbeya) na Songea mkoani Ruvuma.
Miji mingine ni Njombe, Wanging’ombe na Makambako mkoani Njombe, Mafinga (Iringa), Mpanda (Katavi), Sikonge, Urambo na Kaliua (Tabora), Singida, Kihomboi na Manyoni (Singida), Chemba na Chamwino (Dodoma), Kasulu (Kigoma), Kayanga (Kagera) ,Geita na Chato (Geita), Rorya, Mugumu na Tarime (Mara).
Ikiwa mradi huo utatekelezwa kikamilifu utakuwa ndiyo mradi mkubwa zaidi Tanzania kuzidi miradi ya miradi ya Tabora- Igunga-Nzega uliojengwa kwa Sh617 bilioni na mradi wa Arusha wenye thamani ya Sh520 bilioni.
Viongozi mbalimbali, Wakandarasi walioshinda zabuni, pamoja na Wabunge wanufaika wa miradi ya Maji wakiwa katika viwanja vya Ikulu Chamwino kushuhudia utiaji Saini wa Mikataba ya miradi hiyo leo Juni 6, 2022. Picha| Ikulu.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyeshudia utiaji saini wa mradi huo leo Mei 6, 2022 jijini Dodoma ameishukuru India kwa ushirikiano wake mzuri na sapoti inayoendelea kutoa kwa Serikali ya Tanzania katika masuala ya biashara na elimu.
Pia ameipongeza Wizara ya Maji kwa kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji jambo lililosaidia mradi huo kunufaisha miji 28 tofauti na miji 16 tu iliyokuwa imekadiliwa awali.
Pamoja na pongezi hizo Rais Samia amewataka watendaji wa Wizara ya Maji kusimamia ipasavyo ujenzi wa mradi huo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu inajengwa ipasavyo na maji yanapatikana kwani mradi huo unajengwa kwa fedha za mkopo na unatakiwa kulipwa.
“Nendeni mkasimamie fedha zetu huu ni mkopo, kwa mara nyingine tumekuja mbele ya wananchi kuwaeleza tumepata mkopo wa dola milioni 500 na zote zinakwenda kwenye majivkwenye miji iliyotajwa.
“Na kwa sababu ni mkopo, Watanzania wote tutakuja kuulipa mkopo huu kwa hiyo nendeni kasimamieni mkopo ulete manufaa wanapokuja kuulipa wawe wanatumia matunda ya mkopo waliochukua,” amesema Rais.
Zinazohusiana:
- Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano utunzaji bonde la mto Nile
- Visima kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini?
Je miji mingine yenye uhaba wa maji itakuwaje?
Rais Samia amesema Serikali yake itaendelea kujenga miradi ya maji kwenye kila eneo nchini ili kuhakikisha ifikapo 2025 huduma ya maji na salama inafikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini
“Kuna dalili zote kwamba tutaweza,mpaka hapa tulipo kwa vijijini tupo asilimia 74, lakini miradi 1,000 inayoendelea vijijini Tanzania nzima itakuja kuchangia asilimia 4….lakini kwa upande wa mijini leo tupo asilimia 89.6…bado tuna miaka mingine miwili ya utekelezaji kwa hiyo kwa hakika tutafika au kupita tulikoelekezwa na ilani ya chama chetu,” amesema Rais.
Itakumbukwa Mei 12 mwaka huu Bunge liliidhinisha Bajeti ya Wizara ya Maji kwa asilimia mia moja ambapo Wizara hiyo iliomba Sh709.3 bilioni.
Kati ya fedha hizo, Sh657 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku vipaumbele vikiwa ni kuanza kwa miradi mipya pamoja na upanuzi na ukarabati wa miradi inayoendelea kutekelezwa.
Latest
