Yaliyomo ndani ya albamu mpya ya mwanamuziki John Legend
- Ni albamu nzuri kwa wanaofurahia nyimbo za mapenzi.
- Miondoko ya Legend imeendelea kuwa kwenye hali ya utulivu kama ilivyo kawaida yake.
- Hata hivyo, kama umemzowea kama mbembelezaji masikio, Legend safari hii ameimba tofauti.
Dar es Salaam. Huenda ulikuwa unajiuliza yuko wapi mwanamuziki maarufu wa Marekani John Legend tangu aachilie albamu yake ya mwisho zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Amerudi tena kwa kasi na albamu mpya ya “Bigger Love” ambayo imesheni nyimbo mbalimbali zenye ladha tofauti kuamsha hisia za mashabiki wake ambao walikuwa wanamngoja aje na vitu vipya kukonga mioyo yao.
Legend mwenye umri wa miaka 41 siyo kwamba alikuwa hasikiki kabisa, hapana! Alikuwepo lakini hakutoa albamu mpya.
Kudhihirisha alikuwepo, Januari mwaka huu aliachia wimbo wa “Conversations in the dark” ambao hadi kufikia Juni 26, 2020 umejinyakulia watazamaji milioni 11.7 kwenye mtandao wa YouTube.
Albamu mpya ya mwanamuziki huyo wa nyimbo za mapenzi hasa zile zenye vionjo vya kubembeleza imetoka Juni 19 ikiwa na nyimbo 16.
Wimbo wake wa “Bigger Love” ambao umebeba jina la albamu ndiyo umejipatia watazamaji wengi zaidi huko YouTube wanaofikia milioni 1.18 hadi jana Juni 26, 2020.
Wimbo mwingine wa staa huyo wa miondoko ya RnB ni “Actions” hadi jana Juni 26 umetazamwa na watu 1.16 milioni ikiwa ni wimbo uliofunga orodha ya nyimbo zake zenye watazamaji zaidi ya milioni moja YouTube.
Kati ya nyimbo hizo 16, mbili tu ndiyo ziko katika mfumo wa video na zilizobaki zina sauti tu.
Mwanamuziki wa Tanzania Frankie Maston ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa huenda albamu hiyo isitazamwe na watu wengi Youtube kwa sababu ina nyimbo nyingi za sauti na watu huvutiwa na kutazama zaidi nyimbo za video.
Zinazohusiana:
- Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka kimaisha
- Programu za mauzo zinazoweza kuwatoa wanamuziki Tanzania
- Kwangwaru ya Harmonize inavyotikisa Youtube
Albamu hiyo itakuwa na kishindo kikubwa?
Ingawa ni mapema kuzungumzia mafanikio ya albamu hiyo mpya, lakini inaweza isifikie umaarufu wa nyimbo yake ya “All of Me” aliyopo kwenye albamu ya “Love in Future” ya mwaka 2013 ambao hadi kufikia jana jioni, wimbo huo umetazamwa na watu bilioni 1.69 Youtube.
Kama ni mfuasi kindakindaki wa Legend basi utafurahia nyimbo zake mpya kama “Wild”, “Always” na “Don’t Walk Away”.
Kama wewe uliufurahia zaidi wimbo wake wa “All of Me” huenda ukafurahia nyimbo za “Ooh Laa”, “U move I Move” na “Focused”.
Kama umemzoea Legend kama mbembelezaji, utashangazwa na wimbo wa “Favorite Place” ambao ameuimba kwa miondoko ya kuchana fulani hivi.
Je, una maoni kuhusu albamu ya Legend? Tuandikie kupitia baruapepe: newsroom@nukta.co.tz na mitandao yetu ya kijamii ya Facebook/Twitter: @NuktaTanzania na Instagram: @nuktatz.
Latest